January 2, 2013

Hotuba ya Rais December 2012



Utangulizi
Ndugu zangu, Watanzania Wenzangu;         
Ni furaha na faraja kubwa kuifikia siku hii adhimu ya kuuaga mwaka wa 2012 na kuukaribisha mwaka 2013. Ni jambo la bahati ambayo hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuumaliza mwaka huu salama.  Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao wangependa kuiona siku hii lakini hawakujaaliwa. Wametangulia mbele ya haki.  Tuendelee kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awape mapumziko mema.  Amin.   Nasi tumuombe Mola wetu atujaalie fanaka tele katika mwaka ujao.

Mapitio ya Mwaka 2012
Ndugu wananchi;
Mwaka tunaoumaliza leo ulikuwa wenye mambo mengi mazuri na mafanikio makubwa, lakini, pia, ulikuwa na changamoto zake. Baadhi zilikuwa ngumu na zipo zilizokuwa za kusikitisha na kuhuzunisha. 
Ajali za barabarani na majini ziliendelea kupoteza maisha ya watu wengi na kusababisha majeraha na ulemavu kwa maelfu.  Ajali mbaya kuliko zote kutokea, mwaka huu, ilikuwa ile ya meli ya MV Skagit iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012 ambapo watu 144 walipoteza maisha.  Ajali za barabarani zilizosababisha vifo nazo ziliongezeka kutoka 3,012 mwaka 2011 hadi kufikia 3,144 na kusababisha vifo vya ndugu zetu 3,714. 
Ndugu Wananchi;
  Kufuatia ajali ya MV Skagit ambayo ilitokea miezi 11 baada ya ile ya MV Spice Islander, Serikali zetu mbili zimekuwa zikishirikiana kwa karibu kuhusu masuala ya usafiri wa majini kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.  Kwa ajili hiyo SUMATRA na Zanzibar Maritime Authority zinafanya kazi kwa karibu zaidi na kanuni za usafirishaji wa abiria na mizigo na za usajili na ubora wa meli zimewianishwa.  Ni matumaini yetu kuwa hatua hizo zitasaidia kumaliza ajali zinazotokana na makosa ya wanadamu.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa ajali za barabarani tuliendelea na tutaendelea kuwahimiza madereva kuheshimu Sheria za Usalama Barabarani, waepuke uzembe na hasa ulevi wakati wa kuendesha.  Tutaendelea kuwakumbusha wenye magari kuhakikisha kuwa uzima wa magari yao unakuwa wa kiwango cha juu.  Hali kadhalika, tumewataka Polisi waongeze ukali na kuwabana ipasavyo madereva na wamiliki wa magari ili watekeleze wajibu wao na wasipofanya hivyo wawajibishwe inavyostahili. 
                                        Hali ya Usalama
Ndugu wananchi;
Tunaumaliza mwaka huu nchi yetu ikiwa shwari, salama na tulivu.  Tuombe Mungu hali hii iendelee mwaka 2013 na idumu milele.  Mipaka ya nchi yetu ipo salama na uhusiano na majirani na nchi zote duniani ni mzuri.  Tunaendelea kutafuta suluhu ya mgogoro wa mpaka kati ya nchi yetu na Malawi katika Ziwa Nyasa kwa njia ya mazungumzo. Suala hilo limewasilishwa kwa pamoja na Serikali zote mbili kwa Mheshimiwa Joaquim Chissano, Mwenyekiti wa Umoja wa Viongozi Wastaafu wa Afrika kwa ajili kuzisaidia nchi zetu kupata ufumbuzi.  Matumaini yetu ni kuwa viongozi hao watalishughulikia suala hili mapema iwezekanavyo.
Ushirikiano wa Kanda
Ndugu Wananchi;
Ushirikiano wetu wa kikanda katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) unaendelea vizuri.  Mwaka huu nchi yetu imepewa heshima kubwa ya kuwa Mwenyekiti wa Chombo cha SADC kinachoshughulikia masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama.
  Jukumu hilo ni zito na hasa katika kipindi hiki ambapo kuna changamoto za kisiasa na kiusalama katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Madagascar na Zimbabwe.  Nchi yetu inatarajiwa kuongoza juhudi za kupata ufumbuzi wa migogoro hiyo migumu.  Ndiyo maana tulifanya Mkutano  Maalum wa Wakuu wa Nchi za SADC hapa Dar es Salaam tarehe 7 na 8 Desemba, 2012.  Mwaka ujao, kwa kushirikiana na wenzetu, tutaendeleza juhudi zetu.  Ni matumaini yangu kuwa tukipata ushirikiano wa viongozi na wananchi wa nchi husika na jumuiya ya kimataifa tutapata ufumbuzi tunaotaka.
Ndugu Wananchi;     
Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, tumeendelea kushuhudia Jumuiya hiyo na harakati za utangamano zikizidi kustawi.  Jengo la Makao Makuu ya Jumuiya limekamilika na kuzinduliwa rasmi tarehe 28 Novemba, 2012.  Siku hiyo hiyo kule Athi River, Kenya, barabara ya kutoka Arusha hadi Athi River ilizinduliwa.  Barabara hii ni moja ya miradi kadhaa inayotekelezwa kwa pamoja na nchi wanachama wa Jumuiya wa Afrika Mashariki. 
Mchakato wa utangamano wa kiuchumi wa Afrika Mashariki unaendelea kwa kasi.  Tanzania ikiwa sehemu kamili ya mchakato huo, lazima tuhakikishe kuwa tunakwenda nao sambamba.  Tusikubali kuachwa nyuma wala kuwa chanzo cha kuuchelewesha mchakato huo bila ya sababu za msingi.  Utangamano una maslahi kwa nchi yetu na manufaa yake ni makubwa.  Kwa mfano, mauzo yetu katika soka la Afrika Mashariki yameongezeka sana kutoka dola za Kimarekani milioni 58.6 mwaka 2000 hadi kufikia dola za Kimarekani milioni 409 mwaka 2011.
 Jumuiya imekuwa kichocheo muhimu cha kukuza uzalishaji, ajira na uchumi hapa nchini.  Kwa ukubwa wa nchi yetu na rasilimali tulizonazo tuna matumaini makubwa ya kunufaika zaidi siku za usoni.  Naweza kuthubutu hata kusema kuwa Tanzania inaweza kunufaika zaidi kuliko nchi nyingine wanachama wa Jumuiya hiyo.  Kinachotakiwa ni sisi kujipanga vizuri kwa sera na mipango ili tuzitumie fursa tulizonazo kwa maslahi ya uchumi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Tuache woga, tujiamini.
Matishio ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Licha ya kumaliza mwaka nchi ikiwa shwari na yenye amani na utulivu, yalikuwepo matukio yaliyotishia usalama wetu.  Bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa matukio hayo yalisababishwa na baadhi ya viongozi wa dini na siasa na wafuasi wao.  Kwa kweli kwa mara ya kwanza nchi yetu ilifikishwa kwenye hatari ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa Watanzania au hata mapigano ya raia kwa misingi ya dini zao.  Bahati nzuri hilo halikutokea na Mungu aliepushe lisitokee kamwe.
Nimeshalisemea jambo hili siku za nyuma na napenda kurudia tena leo kuwasihi Watanzania wenzangu kupima athari za kauli zetu na matendo yetu kwa mustakabali wa jamii yetu, nchi yetu na watu wake.  Viongozi wa dini, waumini na viongozi wa siasa na wafuasi wao wanao wajibu maalum wa kuhakikisha kuwa Watanzania wanaendelea kuishi kwa upendo, amani na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zao, makabila yao, rangi zao au maeneo watokako.  Hiyo ndiyo sifa ya nchi yetu tunayoijua sote ambayo ni njema na watu wengi wanataka kuja kujifunza kwetu na wale wenye shida wanatamani wawe kama sisi.  Hii ni tunu muhimu ya taifa ambayo tusikubali kuipoteza kwa maslahi binafsi ya watu wachache.
Ndugu Wananchi;
Wakati wo wote, lazima tutambue umuhimu wa kuvumiliana na kuheshimiana kwa tofauti zetu za kidini, rangi, kabila, tutokako na ufuasi wa vyama vya siasa.   Lazima pia tuhakikishe kuwa tunaheshimu sheria na taratibu zinazotawala mikutano na maandamano.   Tukiyazingatia hayo nchi yetu itakuwa haina tishio lo lote kwa amani na usalama wake.  Yasipozingatiwa tunaiweka nchi yetu hatarini.  Sisi katika Serikali tutakuwa hatuna la kufanya bali kutimiza wajibu wetu wa kulinda usalama wa raia na nchi yetu.  Wahusika watachukuliwa hatua na vyombo vya usalama na kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi.  Tulifanya hivyo mwaka huu na hatutakuwa na ajizi kufanya hivyo siku yo yote kama hapana budi.
Uhalifu Unapungua
Ndugu Wananchi;
  Inatia moyo kuona kuwa mwaka huu makosa ya jinai yalipungua na kufikia 66,255 yakilinganishwa na makosa 69,678 ya mwaka jana au 94,390 ya mwaka juzi.  Hii inathibitisha kuimarika kwa kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi wakishirikiana na wananchi na vyombo vingine vya usalama.  Pamoja na hayo lazima tuongeze juhudi za kupambana na uhalifu kwani bado matukio ni mengi mno na upungufu bado ni mdogo.  Tutaendeleza kazi tuifanyayo sasa ya kuliimarisha Jeshi la Polisi kwa rasilimali watu, zana na vitendea kazi husika.
Uhalifu wa Kimtandao
Ndugu Wananchi;
Tutaongeza nguvu katika kupambana na uhalifu unaoendeshwa na mitandao ya uhalifu ndani na nje ya nchi.  Mitandao hiyo hasa imekuwa inajihusisha na biashara ya kusafirisha wanadamu, biashara ya dawa za kulevya na biashara ya nyara za Serikali. 
Mapambano dhidi ya uhalifu wa kimtandao yametuwezesha kukamata wahamiaji haramu 4,765 na tayari 1,611 wamerudishwa kwao.  Kwa upande wa dawa za kulevya watuhumiwa 6,929 walikamatwa mwaka huu ukilinganisha na 209 mwaka 2011. Kilo 55,285 za dawa za kulevya zilikamatwa mwaka huu ukilinganisha na kilo 17,752.4 mwaka jana.  Kwa upande wa nyara za Serikali, zilizokamatwa ni 1,416 nakati ya hizo 736 ni meno ya tembo.  Watuhumiwa 1,037 walikamatwa na kesi 746 zipo Mahakamani katika hatua mbalimbali. 
Ndugu Wananchi;
Taarifa hizi zinathibitisha kuimarika kwa jitihada za kupambana na uhalifu wa kimtandao.  Tutaimarisha zaidi jitihada zetu mwaka 2013 ili tupate mafanikio zaidi.  Tutaviongezea uwezo wa rasilimali watu, zana, vifaa na fedha za uendeshaji vyombo vyetu vya usalama vinavyoongoza mapambano haya. 
Tutaimarisha na kuendeleza ushirikiano baina ya nchi yetu na nchi jirani na nyinginezo duniani.  Hii itasaidia kutuongezea uwezo wa kupambana na mitandao ya uhalifu ndani ya nchi, kikanda na kimataifa.  Pia tutazipitia upya sheria za kupambana na makosa haya kwa nia ya kuziboresha.
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013, tutapanua na kuimarisha huduma ya matibabu kwa watu walioathirika na dawa za kulevya kote nchini.  Tutakamilisha ujenzi wa kituo cha Dodoma na kujenga kingine kipya Dar es Salaam.  Natoa wito kwa wale wote walioathirika au watu wenye watoto au rafiki au jamaa walioathirika waende hospitali kupatiwa matibabu kwani matibabu hayo ni bure.
Hali ya Uchumi
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2012, tunaoumaliza leo,  uchumi wa nchi yetu uliendelea kukua na kuimarika licha ya kuwepo kwa changamoto za upatikanaji wa umeme, kupanda kwa bei za mafuta na chakula duniani na uhaba wa mvua katika maeneo mengi nchini uliosababisha kupungua kwa uzalishaji na kupanda kwa bei za vyakula nchini.  Pia, licha ya kuendelea kwa msukosuko wa uchumi wa dunia na hasa katika Bara la Ulaya ambako ni soko kuu la bidhaa zetu na watalii.  Mategemeo yetu ni kuwa, mwaka huu, uchumi wetu utakua kwa asilimia 6.8 na  mwakani (2013) utakua kwa asilimia 7.0 ukilinganisha na asilimia 6.4 mwaka 2011. 
Kwa jumla, ukilinganisha na makadirio ya IMF ya kiwango cha ukuaji wa uchumi wa dunia kuwa asilimia 3.3 mwaka huu, ni dhahiri kuwa uchumi wetu unakua kwa kasi nzuri na kuifanya Tanzania iendelee kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa.
Hali hii ya uchumi wetu ina maana kubwa mbili.  Kwanza, kwamba uchumi wetu umejenga uhimilivu dhidi ya misukosuko ya uchumi wa dunia.  Na pili, kwamba shughuli za uzalishaji na huduma zinazidi kukua na mauzo ya bidhaa ndani na nje ya nchi yameongezeka.  Kuongezeka kwa mauzo ya nje kumefanya akiba yetu ya fedha za kigeni kufikia dola za Marekani bilioni 3.9 mwezi Novemba, 2012 kiasi ambacho kinatuwezesha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi minne.
Ndugu Wananchi;
Makusanyo ya mapato ya Serikali yatokanayo na kodi yalifikia shilingi bilioni 580.3 mwezi Oktoba, 2012 ikilinganishwa na shilingi bilioni 479.3 mwezi Oktoba 2011.  Matarajio yetu ni kufanya vizuri zaidi mwaka 2013 kwa mapato yatokanayo na kodi na yale yasiyotokana na kodi ambayo bado ni chini ya lengo. 
Ndugu Wananchi;
Mfumuko wa bei kuwa juu ni changamoto ambayo tunaendelea kuikabili ili kuleta utulivu uliokamilifu kwa uchumi wetu na kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wa Tanzania.  Serikali imechukua hatua kadhaa kudhibiti hali hiyo na mafanikio ya kututia moyo yameanza kuonekana.  Kwa mfano, mfumuko wa bei umepungua kutoka asilimia 19.8 mwezi Desemba 2011 hadi asilimia 12.1 mwezi Novemba, 2012.  Kiwango hicho bado ni cha juu na hakikubaliki.  Tutaendelea kuchukua hatua zaidi ili tuweze kufikia lengo letu la mfumuko wa bei kuwa chini ya asilimia 10 ifikapo mwezi Juni, 2013.
Miongoni mwa mambo tuliyopanga kufanya ili kupunguza mfumuko wa bei ni kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme na kudhibiti mwenendo wa bei ya mafuta.  Kufanya hivyo kutasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na uchukuzi wa bidhaa. Aidha, tutaendelea kutekeleza mipango na mikakati ya kukuza na kuboresha kilimo nchini kwa lengo la kujihakikishia usalama wa chakula, kukuza pato la taifa na kupunguza umaskini hasa miongoni mwa wakulima.   
Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo
Ndugu wananchi;
Mwaka huu tunaoumaliza leo ulikuwa na mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa utekelezaji wa miradi ya kuendeleza miundombinu nchini.  Tumeshuhudia miradi ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege, reli, bandari, umeme na maji ikikamilika, au kuanzwa au utekelezaji wake ukiwa unaendelea.  Hakika lengo la kuunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara kwa barabara za lami siyo ndoto tena bali ni jambo la uhakika na litatimia muda si mrefu ujao. 
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa reli, mwaka huu tumeendelea kukarabati reli ya kati na kurejesha usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na Kigoma.  Mwaka ujao (2013) tutaendeleza kazi ya ukarabati wa reli hiyo muhimu na kuzidi kuboresha huduma.  Tumekamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege vya Mpanda na Songwe na tunaendelea kuboresha viwanja vya Tabora, Kigoma, Bukoba, Mafia, Mwanza na Zanzibar.  Tumeendelea kujenga na kupanua miundombinu ya maji nchini na kuboresha upatikanaji wa maji salama kwa Watanzania. Kwa mwaka huu usambazaji wa maji salama umefikia asilimia 87 kwa watu wa mijini na asilimia 61.5 vijijini.   Tutaendeleza kazi hiyo mwaka 2013.
 
 
 
Msongamano wa Magari Dar es Salaam
Ndugu Wananchi;
Katika Jiji la Dar es Salaam tumeendelea na tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza msongamano wa magari unaozidi kuongezeka.  Barabara mpya zimejengwa na zinaendelea kujengwa ndani na kuzunguka Jiji.  Barabara kadhaa zimepanuliwa na nyingine zitaendelea kupanuliwa.  Ujenzi wa miundombinu (barabara na vituo) ya mabasi yaendayo haraka umeanza.  Mwaka 2013 ujenzi wa barabara za juu ya nyingine katika makutano ya TAZARA utaanza na matayarisho ya kufanya hivyo kwa makutano ya Ubungo yatakamilishwa. 
Tumetimiza ahadi yetu ya kutumia treni kusafirisha abiria katika jiji la Dar es Salaam.  Usafirishaji umeanza na unaendelea kati ya Stesheni na Ubungo na kutoka Stesheni ya TAZARA hadi Pugu – Mwakanga.  Mwaka ujao tutaendelea kuimarisha usafiri huo kwa kuongeza treni na idadi ya safari.  Tayari Mshauri Mwelekezi ameshateuliwa kufanya upembuzi yakinifu na kushauri kuhusu kupanua huduma hiyo mpaka ifike Tegeta, Bunju, Kimara, Luguruni, Kibaha, Mbagala-Rangi Tatu na Kongowe.  Ushauri huo pia utahusu kuwa na huduma bora ya usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam kwa maana ya aina ya njia, vichwa vya treni na mabehewa.  Tuliamua kuanza na reli na treni iliyopo, lakini nia yetu ni kufanya vile hasa inavyotakiwa iwe kwa usafiri wa treni mijini. 
Umeme
Ndugu Wananchi;
Mwaka tunaoumaliza leo haukuwa rahisi kwa upande wa upatikanaji wa umeme.  Mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kidatu, Kihansi, Mtera, Pangani na Nyumba ya Mungu yameendelea kutokuwa na maji ya kutosha kwa sababu ya uhaba wa mvua.  Hivyo basi taifa limelazimika kutegemea umeme wa kukodi unaozalishwa kwa kutumia mafuta.  Umeme huo umekuwa wa gharama kubwa na hivyo kuwa mzigo mkubwa kwa TANESCO na taifa. Serikali imeendelea kushirikiana na TANESCO na kuisaidia kubeba mzigo huo.  Tutaendelea kufanya hivyo mwaka ujao na mpaka tutakapofikia hatua ya kutokuwa na ulazima wa kutumia umeme wa kukodi.
Ndugu Wananchi;
Mtakumbuka kuwa tulipopata tatizo la ukame na upungufu wa umeme mwaka 2006/2007, Serikali yetu iliazimia kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na vyanzo vingine vikiwemo gesi asili, makaa ya mawe, upepo na jua.  Nafurahi kusema kuwa, tangu wakati ule Serikali imeiwezesha TANESCO kujenga vituo vitatu vinavyozalisha MW 245 kwa kutumia gesi. 
  Hatukuweza kuongeza zaidi uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi kwa sababu ya kiasi cha gesi kinacholetwa Dar es Salaam kutoka Songo Songo kuwa kidogo.  Ndiyo maana tukaamua kujenga bomba jipya kubwa la kusafirisha gesi kutoka Songo Songo hadi Dar es Salaam.
Ndugu Wananchi;
Kwa nia ya kutaka kuhakikisha kuwa kutakuwa na gesi ya kutosha kuzalisha umeme mwingi zaidi pale inapohitajika, ikaamuliwa bomba hilo liendelezwe mpaka visima vya gesi vya Mtwara.  Ujenzi wa bomba hilo umeanza mwezi Novemba, 2012 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18.  Gesi itakayopatikana ina uwezo wa kuzalisha MW 3,000 za umeme.  Tayari mipango inaendelea ya kujenga mitambo ya kuzalisha MW 900 pale Kinyerezi ili mara gesi itakapofika umeme uzalishwe.  Hatua hiyo itatuwezesha kuung’oa mzizi wa fitina wa mgao wa umeme na mzigo wa kununua umeme ulio ghali. 
Utafutaji wa Gesi
Ndugu Wananchi;
          Tangu mwaka 2010 gesi nyingi imegundulika baharini na nchi kavu katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani. Utafutaji bado unaendelea na tuna matumaini kuwa gesi nyingi zaidi huenda ikagundulika.  Hivi sasa Serikali inaandaa sera na sheria mpya ya gesi ili kuboresha zinazotumika wakati huu.  Nia yetu ni kutaka kuhakikisha kuwa rasilimali hii adhimu inasimamiwa vizuri kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake pamoja na kulinda maslahi ya wawekezaji. 
Napenda kutumia nafasi hii kuwahakikishia ndugu zetu wa kule gesi ilipogunduliwa au popote itakapogundulika, kuwa watanufaika sawia na katu hawatasahaulika.  Rai yao ya kutaka na wao wanufaike inakubalika na Serikali inajiandaa hivyo. Viongozi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa mfano, wanajua maelekezo niliyotoa kuhusu kuiandaa miji ya Mtwara na Lindi kupokea uchumi wa gesi.  
Lakini, sharti la kutaka gesi isisafirishwe kwenda kokote na kwamba kila kitu kifanyike kwao halikubaliki. Rasilimali inayopatikana po pote katika nchi hii ni mali ya taifa zima na hutumika kwa manufaa ya taifa.  Katu siyo mali ya watu wa pale ilipogundulika au pale shughuli hizo zinapofanyika. Jumla ya makusanyo ya mapato yatokayo sehemu zote za nchi yetu na kutokana na vyanzo mbalimbali ndiyo yanayotumika kuhudumia watu wote po pote walipo.
Ndugu Wananchi;
 Huu ni msingi mzuri, ni sera nzuri na ni jambo jema la tunu, tulilorithi kwa waasisi wa Taifa letu, ambalo hatuna budi kulienzi na kulidumisha.  Nawasihi wanasiasa wenzangu tusiwaelekeze kwenye mambo mabaya wananchi tunaodai kuwapenda. Kutafuta umaarufu kwa agenda zinazopandikiza chuki kwa watu na kuligawa au kulibomoa taifa, ni upungufu mkubwa wa uongozi na uzalendo.  Tuache siasa za ubarakara na kuwapa watu matumaini yasiyotekelezeka.  Nawaomba wananchi msiwasikilize, si watu wanaowatakia mema na wala hawaitakii mema nchi yetu.
Elimu
Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio katika utekelezaji wa sera yetu ya kupanua fursa ya elimu kwa Watanzania katika ngazi zote.  Mwaka huu vijana wetu wengi zaidi walijiunga na elimu ya msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu.  Hivi sasa tunaelekeza juhudi zetu zaidi katika kuongeza ubora wa elimu.    Kwa ajili hiyo, tumechukua hatua za makusudi za kupanua mafunzo na ajira za walimu wa shule za msingi na sekondari.  Kwa mfano,  mwaka huu walimu 24,621 wapya waliajiriwa kati yao 11,379 wa shule za msingi na 13,242 wa shule za sekondari.  Januari, 2013 tunategemea kuajiri walimu 28,746 kati yao 14,606 wa shule za msingi na 14,060 watakuwa wa shule za sekondari.
 Kwa sababu hiyo, uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi umeendelea kuwa mzuri.  Hivi sasa kwa shule za msingi uwiano umefikia 1:46 ukilinganisha na 1:56 mwaka 2005. Uwiano unaostahili ni 1:40. Kwa upande wa sekondari uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi hivi sasa ni 1:29 ukilinganisha na 1:20 unaostahili.  Kutokana na upanuzi wa vyuo vya kufundisha walimu nchini, bila ya shaka baada ya miaka mitatu hivi upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari haitakuwa kilio tena. 
Ndugu Wananchi;
Upatikanaji wa vitabu nao unazidi kuwa bora.  Hivi sasa uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi ni 1:3 kwa shule ya msingi na sekondari 1:3 ukilinganisha na 1:5 kwa shule za msingi na sekondari 1:4 mwaka 2009.  Hata hivyo, tutaendelea kuongeza mgao wa fedha katika bajeti ya elimu ili kuongeza upatikanaji wa vitabu na vifaa vingine vya kusomea na kufundishia.  Tunataka katika muda mfupi ujao uwiano uwe 1:1. 
Kwa upande wa maabara za sayansi, tarehe 4 Novemba, 2012, nilipokuwa kwenye ziara ya Mkoa wa Singida, nilitoa agizo la kutaka ndani ya miaka miwili, kuanzia mwaka 2013, kila shule ya sekondari ya kata nchini iwe na majengo ya maabara yaliyokamilika.  Yawe pia yanatumika kwa maana ya vifaa na mahitaji muhimu.  Nimewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa agizo hili linatekelezwa kwa ukamilifu.  Kuanzia sasa, katika ziara zitakazofanywa Mikoani na mimi, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu tutapenda kupata taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wake. 
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa ufundishaji imedhihirika kwamba mkakati maalum unahitajika kuboresha ufundishaji wa masomo ya hisabati, kiingereza na sayansi katika shule za msingi na sekondari.  Matokeo ya mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne kwa miaka mingi sasa yanathibitisha haja hii.  Sasa wakati umefika kwa suala hili kulipa uzito unaostahili.  Tutafanya hivyo kuanzia mwaka 2013. 
Afya
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2012 ulikuwa na mafanikio mengi ya kutia moyo kwa upande wa sekta ya afya nchini pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali. Kazi ya kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi watu kwa maana ya kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali mpya na kuimarisha zilizopo iliendelea kutekelezwa kwa mafanikio kote nchini.  
Hali kadhalika, uwezo wetu wa ndani wa uchunguzi na tiba ya magonjwa makubwa umezidi kuimarika mwaka huu. Upatikanaji wa dawa, vifaa vya uchunguzi na vifaa tiba umeendelea kuboreshwa.  Aidha, mafunzo na ajira za madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa afya vimeendelea kuongezwa.  Kituo cha Tiba ya Maradhi ya Moyo kimekamilika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mwaka ujao (2013) shughuli za upasuaji na nyinginezo husika kutibu maradhi ya moyo zitakuwa zimeboreshwa sana.  Upanuzi mkubwa wa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road umekamilika.  Kwa ajili hiyo, huduma zitakuwa bora zaidi na msongamano wa wagonjwa hospitalini hapo utakuwa umemalizika.  Ujenzi wa hospitali kubwa ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma unaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika mwaka 2014.  Hospitali hiyo itatumika kufundishia wanafunzi wa udaktari na uuguzi. 
 
Ndugu Wananchi;
  Mwaka huu pia, tumekamilisha matayarisho ya kuanza ujenzi wa hospitali kubwa na ya kisasa kabisa kule Mlonganzila, Dar es Salaam.  Ujenzi utaanza Februari 2013 na kukamilika Februari, 2015.  Hospitali hii pia itakuwa ya kufundishia wakati Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kitakapohamishia sehemu kubwa ya shughuli zake huko Mloganzila.  Mchakato wa ujenzi wa Chuo hicho nao unakaribia kuanza.  Kuwepo kwa hospitali hizi kutaongeza sana uwezo wetu wa ndani wa uchunguzi na tiba.  Sasa naweza kuthubutu kusema kuwa safari ya kupunguza wagonjwa tunawaopeleka nje tumeianza  kwa dhati.    
Ndugu Wananchi;
 Tumeendelea kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya magonjwa makubwa yanayosababisha vifo vingi kama vile UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.  Maambukizi na vifo vinazidi kupungua.   Pia vifo vya kina mama na watoto vinaendelea kupungua.
Kwa mujibu wa taarifa za mwaka huu za Shirika la Afya Duniani, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano hapa Tanzania vimepungua kutoka vifo 81 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka 2009 hadi kufika vifo 65.2 mwaka 2011 na vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 51 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa hai mwaka 2009 na kufikia vifo 45 mwaka 2011. Mafanikio haya yanaiweka Tanzania katika orodha ya nchi 10 zinazofanya vizuri duniani katika kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Ndugu Wananchi;
   Hatuna budi kufahamu kuwa haya ni matokeo ya kufanya vizuri kwenye chanjo kwa watoto ambayo imefikia wastani wa asilimia 90.  Pia imechangiwa na mafanikio yetu katika kupunguza maambukizi ya malaria na UKIMWI kwa watoto.  Naamini tutapata mafanikio makubwa zaidi kuanzia mwaka 2013 tutakapoanza chanjo dhidi ya kichomi (pneumonia) na ugonjwa wa kuharisha kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.  Aidha, tukiendelea kutekeleza kwa dhati mpango wa kila mtoto kulala kwenye chandarua kilichotiwa dawa na ule Mpango Kabambe wa Kuzuia Maambukizi ya Mama Kwenda kwa Mtoto niliouzindua kule Lindi tarehe 1 Desemba, 2012, mambo yatakuwa vizuri zaidi.     
Sensa ya Watu na Makazi
Ndugu wananchi;
 
          Leo asubuhi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja nilitangaza matokea ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti, mwaka 2012.  Matokeo haya yanaonyesha kwamba idadi ya watu nchini Tanzania ni milioni 44,929,002 kati yao watu milioni 43,625,434 wanaishi Tanzania Bara na milioni 1,303,568 wanaishi Zanzibar.  Ukilinganisha na Sensa ya mwaka 2002 tulipokuwa na watu milioni 34.4, hili ni ongezeko la watu milioni 10.5 au wastani wa asilimia 2.6 kwa mwaka.
Matokeo haya yana maana kubwa kwa Serikali na kwa kila mmoja wetu.  Kwa kasi hii ya ongezeko la watu ifikapo mwaka 2016 Tanzania itakuwa na watu milioni 51.6.  Hiini idadi kubwa sana ya watu inayoleta changamoto kwa Serikali na jamii.  Hatuna budi kutambua maana ya idadi hiyo ya watu na kujipanga vyema kukidhi mahitaji yao na hasa kuhakikisha kuwa maskini hawaongezeki na huduma zinatosheleza mahitaji na zina ubora wa juu.  Kazi hiyo lazima ianze sasa na ionekane katika Mipango ya Maendeleo. 
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, sisi wananchi, taarifa hii inamlazimu kila mmoja wetu atambue kuwa kwa kasi hii, siku za usoni nchi yetu itakuwa na watu wengi, hivyo ushindani kwa rasilimali utakuwa mkubwa.  Watakaofanikiwa wakati huo ni wale wenye familia ndogo au zile ambazo zimepanga uzazi.  Tukipanga uzazi tunajipa nafasi ya kutunza na kulea vizuri watoto wetu na kuwapatia mahitaji yao muhimu ya maisha.  
 
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kurudia kuwashukuru wananchi wenzangu wote kwa ushirikiano wenu uliowezesha zoezi zima kufanikiwa kiasi hiki.  Aidha, nawashukuru kwa dhati viongozi, watendaji wakuu na maofisa wote waliopanga, kuratibu, kusimamia na kutekeleza zoezi la kuhesabu watu.  Natoa shukrani maalum kwa Kamati ya Kitaifa ya Sensa, Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Jamhuri ya Muungano na Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar na makarani wote wa sensa.  Penye nia pana njia.  Tumeweza kushinda changamoto zote na kuwapatia Watanzania nyenzo muhimu ya kupanga mipango ya maendeleo yao.
Vitambulisho vya Taifa
Ndugu wananchi;
Mwaka huu tumeanza zoezi la kusajili watu na makazi kwa ajili ya kuandaa kutoa Vitambulisho vya Taifa kuanzia mwaka 2013.   Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ilifanya zoezi la majaribio katika mkoa wa Dar es Salaam na wilaya ya Kilombero ambalo lilifanikiwa.  Hivi sasa wanaendelea na zoezi hilo Zanzibar. Maandalizi kwa ajili ya kutekeleza zoezi la kutoa vitambulisho nchi nzima kuanzia mwaka 2013 yanakwenda vizuri.   Napenda kuwasihi wananchi wenzangu wakati utakapofika kutoa ushirikiano unaostahili kwa maafisa watakaohusika na kukusanya taarifa na kutoa vitambulisho ili zoezi lifanikiwe ipasavyo.  Nawaomba muitumie vizuri fursa hii ya kujisajili na kupata vitambulisho.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu wananchi;
Mtakumbuka kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nililiyoiunda tarehe 1 Mei, 2012 ilianza kazi yake rasmi tarehe 29 Juni, 2012 na inaendelea vyema.  Mpaka sasa Tume imekamilisha hatua ya kwanza ya kukusanya maoni ya mtu mmoja mmoja katika Mikoa yote nchini.  Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kutoa maoni.  Zoezi linalofuata ni la kukusanya maoni ya makundi maalumu kuanzia mwezi  Januari, 2013.  Natoa wito kwa makundi hayo nayo kushiriki vizuri kwenye hatua hii muhimu.  Baada ya hatua hiyo kukamilika, Tume itaandaa Rasimu ya Katiba ambayo wanategemea itakuwa tayari mwezi Mei, 2013. 
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume, rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Vikao vya Mabaraza ya Katiba vitakavyofanyika kati ya mwezi Juni na Agosti, 2013.    Tume itatangaza muundo na namna ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza hayo na utaratibu utakaotumika wakati wa kujadili na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba wakati huo ukiwadia. 
Baada ya kukamilika kwa Vikao vya Mabaraza ya Katiba, Tume itakamilisha Rasimu ya Katiba ambayo itachapishwa kwenye Gazeti la Serikali kama yalivyo matakwa ya Sheria.  Aidha, itachapishwa katika magazeti ya kawaida kwa wananchi kusoma.  Mwezi Novemba, 2013 rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Bunge Maalum kujadiliwa na kupitishwa.  Baada ya Bunge Maalum kupitisha Rasimu ya Katiba, Rasimu hiyo itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni.
Ndugu Wananchi;
   Matarajio yetu ni kwamba kama kila kitu kitakwenda kama inavyotarajiwa nchi yetu itakuwa na Katiba Mpya iliyotokana na maoni na matakwa ya wananchi ifikapo mwaka 2014.  Mwaka huo Muungano wetu utakuwa unatimiza miaka 50 hivyo hiyo itakuwa zawadi ya tunu kubwa.  Tukifanikiwa kupata Katiba mpya wakati huo, tutafanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia Katiba hiyo.  Inshallah, Mwenyezi Mungu atajaalia baraka zake, nia yetu njema itatimia.  Pamoja na hayo, natoa wito kwenu wananchi wenzangu kushiriki kwa ukamilifu katika hatua zote za mchakato ili tuweze kujenga muafaka kuhusu Katiba tunayoitaka.
 
Marekebisho ya Sheria
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi wa Februari, 2012, nilieleza kwamba katika mazungumzo baina ya Serikali na  vyama vya siasa na wadau wengine juu ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tulikubaliana tushughulikie marekebisho ya Sheria hiyo hatua kwa hatua.   Tulikubaliana kuanza na mambo yanayohusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi ili Tume iundwe na ianze kazi.  Baada ya hapo tuangalie vipengele vinavyohusu Bunge Maalum na Kura ya Maoni.    
Tulifanya hivyo kuhusu Tume ya Katiba na sasa tunajiandaa kuanza mazungumzo kuhusu ngwe iliyobaki yaani, Bunge Maalum na Kura ya Maoni.  Kama mazungumzo yatakamilika mapema kunako Januari, 2013 mapendekezo hayo yatafikishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano katika kikao cha Februari   kwa uamuzi.  Vinginevyo itakuwa katika Bunge la Aprili, 2013.
Ndugu Wananchi;
Kuhusu Kura ya Maoni, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza kuwa Kura ya Maoni itatungiwa Sheria yake maalum.  Ni matumaini yangu kuwa matayarisho yake yataanza mapema iwezekanavyo.  Nawasihi wananchi wenzangu, viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kijamii tuwe watulivu, tuendelee kushirikiana katika mchakato huu wa Katiba mpaka tulifikishe jahazi ufukweni salama kwa mustakabali mwema wa nchi yetu na watu wake. 
Mfumo wa Dijitali
Ndugu wananchi;
Bila ya shaka mtakumbuka taarifa za Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Tume ya Mawasiliano kwamba kuanzia tarehe 1 Januari, 2013 nchi yetu itahamia katika mfumo wa mawasiliano unaotumia teknolojia ya dijitali (au kidijiti kwa tafsiri ya BAKITA) badala ya huu wa sasa wa analojia. Uamuzi huu unakuja kufuatia uamuzi wa kimataifa kwamba nchi zote duniani ziwe zimeingia kwenye mfumo huu ifikapo mwaka 2015.  Pia unazingatia uamuzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa nchi zetu kuanza safari hiyo tarehe 1 Januari, 2013.
  Hapa nchini zoezi hili litafanyika kwa awamu.  Litaanza katika mikoa saba ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mbeya, Kilimanjaro, Mwanza na Tanga na mingine itafuata kwa mujibu wa ratiba itakayopangwa.
Ndugu Wananchi; 
 Teknolojia ya dijitali katika mfumo wa mawasiliano hufanya picha za televisheni kuwa nzuri na hazina chenga chenga.  Mawasiliano ya simu yatakuwa mazuri zaidi.  Vile vile, itakuwa rahisi kupata huduma za televisheni kwenye simu za mkononi na huduma ya intaneti kwenye televisheni.
Ndugu Wananchi; 
Ili kuweza kutumia teknolojia hii, kila televisheni inatakiwa iwe na kifaa kiitwacho king’amuzi. Vifaa hivi vipo kwa wingi madukani na wengine tayari wanavyo. Naomba niwatoe hofu kwamba kwa kuingia katika mfumo huu siyo lazima kununua televisheni mpya. Televisheni yo yote yenye vitundu vitatu vya rangi za njano, nyeupe na nyekundu itaweza kufanya kazi kwenye mfumo wa dijitali. Hata wale ambao hawana televisheni za namna hiyo wanaweza kununua kifaa cha kuunganishia king’amuzi na mambo yakawa mazuri.
Uhusiano wa Kimataifa
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2012, uhusiano wetu na washirika wetu wa maendeleo ulikuwa mzuri na uliendelea kuimarika.  Wote wanaridhika na kusifu kazi nzuri inayofanywa na Serikali yetu na ndiyo maana wanaendelea kushirikiana nasi na kutoa misaada ya maendeleo.  Aidha, wameonesha nia thabiti ya kuendelea kushirikiana nasi na kutusaidia katika harakati zetu za kujiletea maendeleo. 
Napenda kutumia nafasi hii kwa niaba yenu nyote kutoa shukrani za dhati kwa washirika wetu wa maendeleo kwa mchango mkubwa wanaoendelea kutoa kwa maendeleo ya nchi yetu.  Nawahakikishia kuwa tunathamini sana ushirikiano wao na misaada yao na tutafanya kila tuwezalo kudumisha ushirikiano baina yetu. 
Mkutano wa Smart Parntership
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu nchi yetu ilipata bahati ya kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa ya kikanda na kimataifa.  Mikutano hiyo ni pamoja na Mkutano Mkuu wa Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mkutano Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Chanjo (GAVI) na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za  SADC. 
Bahati nzuri mwaka 2013 Tanzania itakuwa mwenyeji wa mikutano mingine ukiwemo ule wa Global 2013 Smart Partnership Dialogue utakaofanyika Dar es Salaam kuanzia tarehe 24 – 28 Mei, 2013.  Huu ni mkutano unaohusisha nchi nyingi duniani na kutoka takriban mabara yote.  Mkutano huu hukutanisha na kushirikisha viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa sekta binafsi wakiwemo wa makampuni makubwa ya kimataifa, wasomi  na wawakilishi wa asasi za kiraia na watu binafsi. 
Kwa kawaida katika mkutano kama huu huwepo agenda maalum, aghalabu kuhusu masuala ya uchumi, biashara na maendeleo.   Mkutano wa mwaka 2013 utazungumzia “Matumizi ya Sayansi na Teknolojia kwa Ajili ya Maendeleo ya Afrika” (Leveraging Science and Technology for Africa’s Development).  Kwa kweli ni kipaumbele muafaka kabisa, ndiyo maana na sisi tumefarijika kuukaribisha.
 
Ndugu Wananchi;
Kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huu wa watu zaidi ya 500 mashuhuri, ni heshima kubwa kwa nchi yetu.  Ni nafasi nzuri ya kuitangaza Tanzania na fursa zake za uwekezaji, biashara na utalii. Pia, ni nafasi nzuri kwa wafanyabiashara wetu kutangaza shughuli zao na fursa za biashara na uwekezaji wanazotaka kushirikisha wafanyabiashara wa nje.  Naomba tuitumie vyema fursa hiyo adimu kwa manufaa ya taifa na ya waanyabiashara wetu.   Tuwaonyeshe wageni wetu upendo na ukarimu kama ilivyo sifa yetu Watanzania ili waondoke na kumbukumbu nzuri za nchi yetu na watamani kurudi tena kutembea au kuwekeza.    
Hitimisho
Ndugu wananchi;
          Tunatarajia kuwa mwaka 2013 utakuwa mwaka wa mafanikio makubwa zaidi katika nyanja zote kuzidi mwaka 2012.  Mambo yaliyokwama mwaka 2012 yatakwamuliwa.   Ajira zitaongezeka kwa uwekezaji vitega uchumi kuongezeka na kuwajengea uwezo wajasiriamali wazalendo, ili waweze kujiajiri wenyewe na kuajiri wengine.  Kwa ajili hiyo, Mifuko ya kusaidia wajasiriamali wadogo, wanawake na vijana itafufuliwa na kutengewa fedha nyingi katika bajeti ya Serikali.
 Mwaka 2013 ni mwaka wa matumaini, hivyo kila mmoja wetu anatakiwa kujituma na kutimiza wajibu wake.  Maisha bora yatakuja kwa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake ipasavyo.  Kama kila mtu atafanya kazi kwa bidii na maarifa, na, kama kila mmoja wetu atajivunia matokeo ya kazi yake na siyo uhodari wa maneno yake ya uchambuzi wa hali.  Kila mtu achukie uvivu na tabia ya kulalamika pasipo kufanya kazi. 
Ndugu Wananchi;
          Mimi na wenzangu Serikalini tunawaahidi ushirikiano wa hali ya juu na kwamba tutawatumikia kwa moyo wetu wote, kwa nguvu zetu zote na kwa maarifa yetu yote.  Tunataka kukidhi matarajio na imani ya wananchi kwa Serikali yao. Tutaendelea kuimarisha utendaji kazi Serikalini na kuhimiza uwajibikaji katika ngazi zote za uongozi. Tutaendeleza mapambano dhidi ya rushwa bila ajizi na watumishi wasio waaminifu, wazembe, wabadhirifu wa mali ya umma watawajibishwa ipasavyo.  Wananchi pia wanao wajibu wa kuwa raia wema na wazalendo wa kweli kwa nchi yao. Kila mmoja wetu ajiulize ataifanyia nini jamii yake na nchi yake badala ya kuuliza itamfanyia nini.
Ndugu zangu,Watanzania Wenzangu;
          Nawatakieni nyote heri na fanaka tele katika mwaka mpya wa 2013. Tusherehekee pamoja kwa amani na utulivu.
 
Mungu Ibariki Afrika!
   Mungu Ibariki Tanzania!
        Asanteni sana kwa kunisikiliza

No comments:

Post a Comment