Dar es Salaam. Umoja wa Nchi za Afrika (AU) umetoa heshima na kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kuita jina lake moja ya majengo yake katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mwalimu Julius Nyerere anapewa heshima hiyo kwa mchango wake katika ukombozi na kuliondoa Bara la Afrika katika ukoloni.
Uamuzi wa kuliita Jengo la Baraza la Amani na Usalama la Umoja huo, Mwalimu Julius Nyerere Hall ulifikiwa juzi wakati wa kikao cha ndani cha marais wa nchi wanachama wa AU kilichofanyika Addis Ababa, Ethiopia.
Akizungumza baadaye kwenye kikao hicho, Rais Jakaya Kikwete aliwashukuru viongozi wenzake, wakiongozwa na Rais wa AU, Robert Mugabe kwa kutoa heshima hiyo kwa mwanzilishi wa Taifa la Tanzania. Hoja ya kuliita jengo hilo Mwalimu Nyerere iliwasilishwa na Rais wa Namibia, Hifekepunye Phohamba katika kikao cha Baraza la Amani na Usalama na kufafanuliwa na Rais Mugabe.
Rais Mugabe alisema, “Sote tulikuwapo pale Tanzania, kila mtu akiwa na kambi yake ya kufanyia mafunzo ya kijeshi. Wengine tukagawanyika palepale, lakini shughuli za ukombozi zikaendelea. Sisi katika Zimbabwe tulikwenda pale chini ya Chama cha Zapu lakini hatimaye kikazaliwa Chama cha Zanu na hivyo tukawa na vyama viwili, Msumbiji ilifika na chama kilichoongozwa na mchungaji mmoja sikumbuki jina lake lakini hatimaye ikazaliwa Frelimo.”
Aliongeza: “Namibia walifika na Chama cha Sswano lakini hatimaye kikazaliwa Chama cha Swapo na Afrika Kusini ilikuwa na vyama vya African National Congress (ANC) na Pan African Congress (PAC), Angola ilikuwa na vyama vitatu vya MPLA, Unita na kile cha Holden Roberto na hata Chama cha Guinea Bissau na Cape Verde kilikuwapo pale Tanzania.”
Rais Mugabe aliongeza kuwa, Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika ilizaliwa na kufanyia kazi zake Dar es Salaam na wao walipewa kila kitu, chakula na mafunzo ya kijeshi. “Tulianza bila kujua hata aina zipi za bunduki, lakini tukajifunza aina ya bunduki na mbinu za vita ya msituni na vita ya kawaida.”
Alisisitiza: “Wakati sisi tunafanya mazoezi, Mwalimu Nyerere alihangaika dunia nzima kuomba fedha za kuendesha shughuli za ukombozi. Alipata misaada kutoka China na Urusi wakati huo na nchi za Ulaya Mashariki, kutoka Algeria, kutoka Misri na hata kutoka hapa Ethiopia.”
Akizungumza katika lugha ya kuvutia ya Kiingereza na mifano mingi ya kuchekesha, Rais Mugabe alisema: “Naweza kuandika kitabu hata hapahapa kuhusu mchango wa Mwalimu na Tanzania katika ukombozi wa Bara letu, hasa Kusini mwa Afrika.” “Nchi gani ingeweza kubeba mzigo mkubwa kiasi hiki? Idadi ya vyama vya ukombozi na vijana wake na vurugu zao za kawaida, idadi ya wakimbizi kutoka nchi mbalimbali na wala siyo nchi tajiri. Kamwe hatutasahau mchango huu mkubwa waliotufanyia,” alisema.
No comments:
Post a Comment