Wafuasi wa Weah waanza kusherehekea ushindi Liberia
Mwanasoka wa zamani wa kimataifa wa Liberia ameanza
kutumiwa ujumbe wa kumpongeza hata kabla matokeo rasmi ya uchaguzi wa
rais hayajatolewa. Wafuasi wa Weah wanasema mgombea wao amepata zaidi ya
asilimia 60 ya kura.
Maafisa wa tume ya uchaguzi hawakuthibitisha taarifa hizo kutoka timu
yake ya kampeni, na mpinzani wa Weah, makamu wa rais Joseph Boakai,
amelimbia shirika la habari la Reuters kuwa hajaona hesabu zozote za
kura na kwa hivyo bado ana matumaini ya ushindi.Matokeo yasiyo rasmi yaliyotolewa na vyombo vya habari vya ndani yameendelea kumuonyesha Weah, mchezaji wa zamani wa klabu za AC Milani na Paris Saint-Germain, akiwa mbele katika kura hiyo ya duru ya pili, ambayo inanuia kuleta mabadiliko ya kwanza ya kidemokrasia tangu mwaka 1944.
Tume ya uchaguzi ya Liberia ilisema ingetangaza matokeo ya kwanza jioni ya Alhamisi, ingawa mchakato huo umekumbwa na ucheleweshaji. Kituo cha Carter cha nchini Marekani kimesema kumekuwepo na maboresho kadhaa katika usimamizi wa kura ya Jumanne kutoka ile ya mwanzo iliyofanyika mwezi Oktoba, kikirejea tathmini chanya iliyotolewa na waangalizi wengine wa kimataifa.
Katibu Mkuu wa chama cha Weah, Janga Kowo, amesema wanatumai kupokea simu ya pongezi kutoka kwa Boakai ingawa hawajasikia chochote kutoka kwake mpaka sasa. Kowo amesema takwimu za timu yake zimekokotolewa kutoka asilimia 60 ya kura zilizopigwa, ambazo zinamuonyesha akiwa mbele katika kaunti 14 kati ya 15.
'Tunasubiri tangazo la ushindi'
"Kwa sasa, nadhani kiongozi wetu George Weah yuko katika nafasi ya ushindi, kwa hivyo tumesimama, tunasubiri tume ya uchaguzi kutupa matuokeo," alisema mfausia wa Weah Francis IT, mfanyabiashara mjini Monrovia.
Katika mahojiano nyumbani kwake nje kidogo ya mji mkuu wa Liberia Monrovia, Boakai alisema anadhani atashinda. Lakini alionyesha wasiwasi iwapo uchaguzi huo utakuwa huru na wa wazi.
Weah, mwanasoka pekee wa Kiafrika aliewahi kuchaguliwa kuwa mwanasoka bora wa shirikisho la Kandanda duniani FIFA, alikuwa akipewa nfasi kubwa ya kuibuka mshindi na kumrithi rais anaemaliza muda wake, mshindi wa tuzo ya Nobel Ellen Johnson Sirleaf.
Liberia ndiyo jamhuri kongwe zaidi barani Afrika, na ilianzishwa na watumwa walioachwa huru kutoka Marekani mnamo mwaka 1847. Makabidhiano yake ya mwisho ya madaraka kwa njia ya kidemokrasia yalitokea mwaka 1944, na yalifuatiwa na mapinduzi ya kijeshi mwaka 1980 na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 14, na kumalizika tu mwaka 2003.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe
Mhariri: Daniel Gakuba
www.ngarakwetu.blogspot.com
No comments:
Post a Comment