Israel yashambulia makao makuu ya HAMAS |
Ndege za Israel
zimeshambulia majengo ya serikali ya chama cha Hamas huko Gaza
ikiwemo ofisi ya waziri mkuu baada ya baraza la mawaziri la Israel kuidhinisha kuitwa kwa wanajeshi wa akiba
75,000 kuvamia Gaza.
Ndege hizo za Israel
zimeshambulia wizara ya ulinzi na jengo la ofisi ya Waziri Mkuu Ismail Haniyeh
ambapo hapo Ijumaa alikutana na Waziri Mkuu wa Misri. Kwa siku kadhaa miripuko
mizito imekuwa ikilitingisha eneo la Gaza
linalokaliwa na idadi kubwa ya watu na kusababisha kufuka kwa moshi mzito
angani.Wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu nao wamekuwa wakiendelea kuvurumiosha maroketi nchini Israel. Licha ya machafuko hayo,waziri wa mambo ya nje wa Tunisia amewasili Gaza leo hii kuonyeshamshikamanona na Wapalestina na kushutumu mashambulizi hayo ya Israel kuwa sio halali na yasiokubalika.Maafisa huko Gaza wanasema Wapalestina 41 wakiwemo raia 20 watoto wanane na mwanamke mmoja mjamzito wameuwawa katika huko Gaza tokea Israel ilipoanza operesheni zake siku nne zilizopita.Raia watatu wa Israel wameuwawa na shambulio la roketi hapo Alhamisi.
Jeshi la Israel limesema kikosi chake cha anga kimeshambulia takriban maeneo 180 waliokuwa wameyalenga jana usiku ikiwa ni pamoja na makao makuu ya polisi majengo ya serikali,vikosi vya kurusha maroketi na kituo cha mafunzo cha Hamas katika Ukanda huo wa Gaza uliozongwa na umaskini.Jengo la ghorofa tatu la afisa wa Hamas Abu Hassan Salah pia lilishambuliwa na kuharibiwa kabisa mapema leo alfajiri. Waokoaji wamesema takriban watu 30 wametolewa kwenye kifusi cha jengo hilo.
Waziri wa mambo ya nje wa Tunisia Rafik Abdelsslem amesema kile inachokifanya Israel sio halali na hakikubaliki.Wakati akitembelea makao makuu ya Haniyeh yalioharibiwa amesema nchi hiyo haina kinga ya kujifanyia mambo inavyotaka bila ya kuchukuliwa hatua na kwamba haiko juu ya sheria.Israel ilianzisha mashambulizi mazito ya anga hapo Jumatano kwa lengo la kuwazuwiya Hamas kuvurumisha maroketi kunakoliandama eneo la kusini mwa Israel kwa miaka kadhaa sasa.
Wapalestina wamevurumisha mamia ya maroketi kutoka Gaza ambapo moja limeshambulia mji wa Jerusalem na matatu yameshambulia mji mkuu wa kibiashara wa Tel Aviv. Jerusalem ilikuwa haikuwahi kulengwa kwa njia hiyo tokea mwaka 1970 na Tel Aviv tokea mwaka 1991.
Juu ya kwamba kumekuwa hakuna repoti za maafa na uharibifu kwa miji hiyo mashambulizi hayo ya maroketi ya masafa marefu yamesababisha fadhaa na kuzusha uwezekano wa Israel kuvamia Ukanda wa Gaza kwa kutumia vikosi vyake vya nchi kavu.Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman amekiambia kituo cha televisheni cha Israel cha Channel One kwamba mashambulizi hayo yataendelea kwa kadri yatakavyohitajika na kwamba hawajajiwekea kikomo kwa uwezo wao au kwa wakati.
Hamas imejizatiti kuendelea kupambana na Israel na imesema shauku yake ya kufanya hivyo imezidi kuwa kubwa.Kundi hilo la Waislamu wa itikadi kali la Hamas limekuwa likiutawala Ukanda wa Gaza tokea mwaka 2007.Israel iliwahamisha walowezi wake wa Kiyahudi kutoka Gaza hapo mwaka 2005 lakini imeendelea kulizingira eneo hilo kwa vikwazo.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa na mkutano wa kupanga mikakati wa saa nne hapo Ijumaa na mawaziri kadhaa waandamizi kujadili kutanuwa mashambulizi yao ya kijeshi.
Duru za kisiasa zinasema baraza hilo limeamuwa kuongeza zaidi ya maradufu fungu la hivi sasa la wanajeshi wa akiba kwa ajili ya uvamizi wa Gaza hadi kufikia 75,000.Hata hivyo haimaanishi kwamba wanajeshi hao wote wataitwa.
Waziri Mkuu wa Misri Hisham Kandil alifanya ziara huko Gaza iliopigiwa debe hapo Ijumaa na kushutumu kile alichokielezea kuwa ni uchokozi wa Israel na kusema kwamba serikali ya Misri iko tayari kusuluhisha usitishaji wa mapigano.Serikali ya itikadi kali za Kiislamu nchini Misri ilioshika madaraka baada ya uchaguzi huru kufuatia uasi uliomn'gowa madarakani dikteta mkongwe Hosni Mubarak ni mshirika wa Hamas lakini pia ni mshirika wa mkataba wa amani na Israel wa mwaka 1979.
Katika ishara nyengine kwamba Netanyahu huenda akawa anajitayarisha kwa uvamizi wa Gaza vikosi vya Israel vimeamuru kufungwa kwa barabara kuu inayoelekea Gaza na barabara nyengine mbili zinazopakana na Ukanda wa Gaza kwa matumizi ya magari ya kiraia.
Takriban Wapalestina milioni moja na laki saba wanaishi katika Ukanda wa Gaza.
Mwandishi: Mohamed Dahman/RTR
Mhariri:Mnette,Sudi
Source:-DW RADIO
No comments:
Post a Comment