Source:Mwananchi
Dodoma/Dar. Baadhi ya wajumbe wa Bunge la
Katiba waliopiga kura za hapana wamelazimika kuondoka Dodoma na kurudi
Zanzibar kwa madai ya vitisho walivyopata kutoka kwa wenzao.
Mmoja wa wajumbe hao, Salma Said alisema jana
jioni kuwa yeye na wajumbe wenzake wamekataa kuitikia wito wa Mwenyekiti
wa Bunge, Samuel Sitta kwenye Kamati ya Mashauriano ili kuhojiwa kuhusu
kura hiyo na kutokana na vitisho wanavyopata kutoka kwa wajumbe wenzao
wameamua kuondoka Dodoma.
Vitisho hivyo vimeripotiwa muda mfupi baada ya
Sitta kuunda Kamati ya Mashauriano ya watu tisa inayoongozwa na Makamu
Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan kushughulikia kura hizo zilizopigwa na
wajumbe saba zinazoweka njiapanda uwezekano wa kupatikana akidi ya
kupitisha Katiba inayopendekezwa.
Wajumbe waliopiga kura za wazi za hapana kwa ibara
zote ni Adil Mohamed Adil, Dk Alley Soud Nassor, Fatma Mohamed Hassan,
Jamila Ameir Saleh, Salma Hamoud Said, Mwanaidi Othman Twahir na Ali
Omary Juma.
Kwa upande wa Tanzania Bara aliyepiga kura ya
hapana kwa rasimu nzima ni Mbunge wa Mpanda Kati (Chadema), Said Arfi na
wajumbe 30 kutoka Zanzibar wakipiga kura ya siri.
“Baada ya kupiga kura za hapana leo (jana),
walijitokeza wajumbe akiwamo (jina tunalihifadhi kwa sasa) wakaanza
kutuzongazonga,” alisema Salma.
“Walituambia kuwa tumebaki hadi dakika ya mwisho
halafu tunasema hapana kwa rasimu nzima ili kula fedha za bure, wanasema
bora tungeondoka na Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi).”
Hata hivyo, alipopigiwa simu yake ya mkononi mmoja
wa watuhimiwa, alipokea na baada ya mwandishi kujitambulisha alikata
simu na alipopigiwa mara ya pili alijibu alisema; “Mimi ni mheshimiwa
mwana na niko Sudan.”
Salma alisema miongoni mwa wajumbe hao wakiwamo
baadhi ya mawaziri waliwafuata hadi nje ya ukumbi wakiwatishia kuwa
watawafanyia hujuma kwa kukataa kuunga mkono rasimu hiyo.
“Sisi tumeamua kuondoka kurudi kwetu, hatutaingia tena bungeni maana hivi vitisho vimezidi sasa,” alisema Salma.
Juhudi za kuwapata wajumbe wenzake kuzungumzia
vitisho hivyo hazikuzaa matunda, lakini Katibu wa Bunge hilo, Yahya
Khamis Hamad alikiri kupokea malalamiko hayo na kwamba amelichukulia
kama suala la kisiasa.
Alisema wajumbe hao hawajasema wametishiwa
kufanyiwa kitu gani, bali walimweleza kuwa wameambiwa kuwa wamekaa pale
(bungeni) kwa ajili ya kupata pesa.
No comments:
Post a Comment