Waziri wa ujenzi wa Tanzania John Pombe Magufuli ameshinda
kinyang'anyiro cha urais kwa 58% ya kura huku Edward Lowassa, mpimzani
wake wa karibu, akipata 39%.
.........................................................................................................................................................
Jina la Dk. John Pombe Magufuli, au JPM kama linavyofupishwa, halikuwa
hata miongoni mwa majina matano yaliyopewa nafasi ya usoni kuteuliwa na
chama cha mapinduzi kupeperusha bendera yake katika uchaguzi wa Oktoba.
Lakini wapo ndani ya chama hicho waliyomuona kama karata ya kati, katika
wakati ambapo chama hicho kinatafuta kujisafisha kutoka na mkururu wa
kashfa za rushwa na kile kinachoelezwa kuwa kasi ndogo ya kuleta
maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Safari yake ya kisiasa
Magufuli mwenye umri wa miaka 55, mwalimu wa hesabati na kemia aliegeuka
mwanasiasa amekuwa mwanachama mtiifu kwa CCM tangu mwaka 1977.
Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuingia bungeni mwaka 1995 kuliwakilisha
jimbo Biharamulo Mashariki -sasa Chato - na baada ya kuchaguliwa kwake
aliteuliwa na rais Benjamin Mkapa kuwa naibu waziri wa ujenzi, nafasi
aliyoishikilia hadi mwaka 2000, alipopandishwa na kuwa waziri kamili wa
wizara hiyo.
Mwaka 2005, rais Jakaya Kikwete alimteuwa kuwa waziri wa Ardhi, Nyumba
na maendeleo ya Makaazi, aliyoitumikia kwa miaka mitatu kabla ya
kuhamishiwa kwenye wizara ya maendeleo ya mifugo na uvuvi kati y amwaka
2008 na 2010. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2010, alirejeshwa kwenye wizara
ya ujenzi anayoiongoza hadi sasa.
Marafiki na hata maadui zake hawasiti kuelezea kuridhishwa kwao na
utendaji wa Magufuli katika nafasi zote alizozishikilia serikali, mara
kadhaa wakimtaja kwa jina la "jembe" ikimaanisha mchapakazi - na hata
kwenye kampeni zake, kaulimbiu yake ya "hapa Kazi tu" inaakisi utayarifu
wake wa kuendeleza uchapaji kazi.
"Siyo jambo la aibu kutambua jambo jema la kimaendeleo linapofanywa,
bila kujali limefanywa na mtu kutoka chama gani cha siasa," alisema
mwenyekiti wa taifa wa chama cha Demokrasia na MaendeleoFreeman Mbowe,
akisifu utendaji kazi wa Magufuli, wakati wa uzinduzi wa barabara
iliyotengenezwa katika jimbo lake la Hai, mkoani Kilimanjaro.
Mtendaji kuliko mwanasiasa
Dk. Magufuli ni mtendaji asiyeruhusu uzembe na anapotaka jambo
litendeke, analisimamia na kuhakikisha matokeo yanaonekana. Anakumbukwa
kwa hatua yake ya kuikataa barabara mpya iliyojengwa kwa ufadhili wa
serikali ya Japan, baada ya kubaini kuwa haikuwa kwenye kiwango
kinachotakiwa, na hakuna alielalamika miongoni mwa wananchi na hata
serikali.
Hakusita hata kuamuru majengo ya serikali kuvunjwa, pale ilipobainika
kuwa yamekiuka sheria za ujenzi, kama vile kujengwa katika maeneo ya
hifadhi za barabara.
Baadhi hata hivyo wanahofu kuwa kwa mwendo huu alio nao, huenda
akaliongoza taifa kibabe, lakini wafuasi wake wanasema Tanzania kwa hali
iliyo nayo inahitaji si tu kiongozi Jasiri , lakini pia mwenye kasi ya
utendaji atakaesaidia kuiondolea nchi matatizo yanayoikabili yakiwemo
rushwa iliyoota mizizi, na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na
kijamii.
Wakati wa kampeni zake, Magufuli amekiri kuwa yeye ni mkali, na hasa
linapokuja suala la kuwaletea wananchi maendeleo, ambayo amekuwa
akisisitza kuwa hayana itikadi za vyama. "Nitakuwa dikteta wa
maendeleo," aliwahi kusema katika moja ya mikutano yake ya kampeni.
Duru ndani ya CCM zinasema uamuzi wake wa kuchukuwa fomu za uteuzi
ulishawishiwa na rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, rafiki yake wa
karibu ambaye hakusita hata siku moja kumuunga mkono na kumtetea wakati
alipojikuta kwenye matatizo. Hata rais wa awamu ya pili mzee Ali Hassan
Mwinyi alimsifu magufuli akimtaja kuwa yeye ni simba wa kazi.
Dk. Magufuli ni mtu wa takwimu, ana kumbukumbu imara na linapokuja suala
la kutoa tarakimu, hapati shida kutaja kwa tarakimu pale anapouliwa na
ama waandishi wa habari kwenye korido za wizara yake au kwenye shughuli
za uzinduzi wa miradi ya ujenzi wa barabara.
Wakati wa mkutano mkuu wa chama mwaka 2010, Magufuli yalitakiwa na
mwenyekiti rais Jakaya Kikwete aeleze utendaji wa chama na serikali yake
katika sekta ya ujenzi wa barabara, na alijibu kwa kutaja makhsusi
idadi ya zinazojengwa na zilizokamilika tayari. Na hakuishia hapo,
alitaja pia maeneo - yaani mikoa, wilaya na hata vijiji zinakojengwa.
Kampeni ya mabadiliko
Kama ilivyo na muungano wa vyama vya upinzani, Magufuli anaendesha
kampeni ya mabadiliko, akiahidi kushughulikia tatizo la rushwa kwa
kuanzisha mahakama ya kuwashtaki wala rushwa. "Kiama cha mafisadi
kimewadia," amekuwa akisema Magufuli kaktika karibu kila mkutano wa
kampeni aliyouhutubia.
"Sikuomba nafasi hii kwa majaribio, niliomba kwa ajili y akufanya kazi
na kuwatumikia watanzania. Naijua vizuri historia ya nchi hii, najua
tulikotoka, tiulipo sasa na tunakoelekea," alisema mgombea huyo, na
kusisitiza yeye ndiye mtu sahihi wa kuiongoza Tanzania kuelekea huko.
Pamoja na uchapakazi, amekosolewa kwa uamuzi wake wa kuuza nyumba za
serikali kwa wafanyakazi na umma. Baadhi pia wanamkosoa kwa kuchukuwa
maamuzi ya haraka ambayo wakati mwingine yameigharimu serikali mamilion
ya pesa - wakitolea mfano uamuzi wake wa kuikamata meli iliyodaiwa
kufanya uvuvi haramu kwenye bahari ya Tanzania - na kisha mahakama
kuamua kuwa meli hiyo ilikuwa inavua kihalali na kuiamuru serikali
kuwafidia wamiliki kiasi cha shiligi bilioni 2.8.
Wakati fulani Magufuli pia amepishana kauli na wakubwa zake wa kazi,
alipokaidi agizo la waziri mkuu Mizengo Pinda kuhusiana na magari
yaliyozidisha uzito kuhuruhiwa kupita kwenye barabara za Tanzania,
akisema maagizo hayo ya waziri mkuu hayakuwa yanatekelezeka na hayakuwa
pia katika maslahi ya nchi.
Dk. Magufuli amepokea tuzo kadhaa ndani na nje ya Tanzania, na ameandika
vitabu na makala za majarida katika maisha yake ya kikazi. Na kwa vile
aliwashinda wanawake wawili kwenye kinyanganyiro cha uteuzi, aliamua
kuwafidia wanawake kwa kumteuwa mwanama Samia Hassan Suluhu kuwa mgombea
mwenza wake - na kuweka uwezekano wa kuwa na mwanamke wa kwanza mwakamu
wa rais katika historia ya nchi hiyo.
SOURCE:-DW
No comments:
Post a Comment