Mgonjwa aambukizwa Zika kupitia ngono Marekani
Maafisa wa afya nchini Marekani wanasema mgonjwa katika jimbo la Texas
ameambukizwa virusi vya Zika kupitia ngono Na sasa watalaamu wamo mbioni
kutengeneza chanjo ya kupambana na virusi hivyo.
Maafisa katika jimbo hilo wamesema virusi hivyo vimeambukizwa kupitia
mgonjwa ambaye amerejea hivi karibuni kutoka Venezuela. Zachary Thompson
ni Mkurugenzi wa Huduma za Afya mjini Dallas "Tuliangalia jinsi
alivyowauma watu Amerika ya Kusini ambao wamesafiri kuingia Marekani, na
kisha jinsi wanavyouma na kuambukiza virusi hivyo. Sasa tunazungumza
kuhusu kuambukizwa virusi hivyo kupitia ngono. Inazusha wasiwasi kwa
sababu ya watu ambao wanasafiri kwenda mataifa ya Amerika ya Kusini, na
kushiriki ndono bila kinga, wanaoweza kuleta virusi hivi nyumbani na
kuwaambukiza wengine"
Virusi vya Zika kwa kawaida husambazwa kupitia mbu anapomuuma binadamu.
Lakini wachunguzi wamekuwa wakiangalia uwezekano kwamba virusi hivyo pia
vinaweza kusambaa kupitia ngono.
Kuna kitisho kikubwa katika uhusiano kati ya virusi hivyo na matatizo ya
watoto kuzaliwa wakiwa na ulemavu. Virusi hivyo vimepatikana zaidi
katika mataifa ya Amerika kusini ambako watoto wengi wameripotiwa
kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo kuliko kawaida.
Zika inahusishwa na watoto kuzaliwa na ulemavu
Kuna ripoti ya mtalaamu mmoja wa Colorado aliyepata virusi hivyo barani
Afrika na kisha akamwambukiza mkewe nyumbani mwaka 2008, na pia
vikapatikana katika mbegu za kiume za mwanamme mmoja katika kisiwa cha
Tahiti.
Shirika la Afya ulimwenguni siku ya Jumatatu lilitangaza hali ya hatari
duniani kote kuhusiana na kusambaa kwa virusi vya Zika, likisema ni
“tukio lisilo la kawaida” ambalo linaweka kitisho kikubwa kwa ulimwengu
mzima.
Kufikia sasa hakuna ushahidi kuwa Zika inaweza kusababisha kifo, lakini
baadhi ya matukio yameripotiwa ambapo wagonjwa wamekuwa na matatizo
makubwa.
Watu wanaougua ugonjwa wa Zika kawaida hujiskia kuwa na homa, upele,
maumivu ya misuli na viungo na uchovu dalili ambazo zinaweza kudumu kwa
siku mbili hadi saba. Lakini karibu asilimia 80 ya watu walioambukizwa
huwa hawapati dalili hizo. Dalili za ugonjwa huo ni sawa na zile za homa
ya dengue ambayo husababishwa na mbu sawa na anayeambukiza Zika.
Ni vipi ugonjwa wa Zika unavyoweza kudhibitiwa?
Juhudi za kudhibiti usambaaji wa virusi zinaangazia zaidi katika
kuyaangamiza maeneo ya kuzaana mbu na kuchukua tahadhari dhidi ya kuumwa
na mbu kama vile kutumia dawa za kuuwa mbu na vyandarua vya kuzuia mbu.
Maafisa wa Afya wamesema visa vya Zika vimeripotiwa katika zaidi ya nchi
30 kuanzia mabara ya Amerika hadi Ireland na Australia. Brazil ndio
nchi iliyoathirika kwa kiasi kikubwa.
Miripuko wa ugonjwa wa virusi vya Zika awali iliripotiwa barani Afrika,
Amerika, Kusini mwa Asia na Pasifik Magharibi. Virusi hivyo
viligundulika kwa mara ya kwanza nchini Uganda mwaka wa 1947 katika aina
Fulani ya tmbili na ikatambuliwa katika watu mwaka wa 1952 nchini
Uganda na Tanzania kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef
No comments:
Post a Comment