June 21, 2017

Anaandika Dkt.Kigwangala-Naipenda Tanzania Yangu, Nasimama na Rais Wangu

Naipenda Tanzania Yangu, Nasimama na Rais Wangu! 
----------------------------
Na Dkt. Hamisi Kigwangalla 

Kila siku nashuhudia wananchi wenzangu wakikalamika. Natamani kujibu. Naacha. Natamani kuwakumbusha wananchi wenzangu. Naacha. Nasema mbona sisi ni wepesi kusahau? Natamani kuwakumbusha wabunge wenzangu. Naacha. Nasema na mimi sasa nipo kwenye Serikali. Ni mtunga sera, ni mfanya maamuzi, nikisema watasema huyu ni 'Naibu Waziri'. Lakini kiukweli nina hamu na shauku ya kuzungumza na wananchi wenzangu. Nami nitoe yangu ya moyoni. Kama mwananchi mwingine yeyote yule tu. Nina haki hiyo. Na mimi haki yangu inalindwa na katiba na sheria za nchi yetu. 

Leo nimeona acha nipumue kidogo. Niseme. Niuvue userikali wangu. Niseme kama mwananchi mwingine yeyote yule. Nianze kwa kuweka wazi kabisa hapa, kwamba; haya ni yangu. Si ya Serikali.   

Serikali ni ya Rais Magufuli, tumempa dhamana, ndiyo. Hili halibishaniwi. Tumempa kazi, ndiyo. Hili pia halibishaniwi. Lakini kazi hii anaifanyaje?  Tunazijua changamoto anazokumbana nazo? Je, ana nia ya kuzitatua? Ni maswali ambayo yanastahili majibu. Kwenye makala hii nitajaribu kuyafafanua kidogo kwa mtazamo wangu kadri nitakavyojaaliwa.

Pamoja na kumpa dhamana Rais wetu, ni lazima tufahamu kuwa na sisi tuna wajibu wa kutimiza kwa Taifa letu. Tuna kazi ya kufanya kumsaidia Rais wetu kubeba mzigo wa kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii kwenye Taifa letu. Tusimuachie huu mzigo peke yake. Tuubebe sote. 

Nchi ina changamoto nyingi sana, siyo kwamba Rais ama Serikali yake haizifahamu ama haina nia ya kuzitatua, ama Rais Magufuli amesinzia, ama anastarehe; kila siku anahangaika kukuna kichwa, usiku na mchana kuzitafutia ufumbuzi. Nadhani hili halina ubishani sana kwa mpenda kweli. Binafsi, sina shaka kabisa juu ya uwepo wa nia thabiti ya kuleta mapinduzi. Sina. 

Kwenye biashara ya kujenga nchi changamoto haziishi siku moja. Ukimaliza moja, nyingine inaibuka, na nyingine zinazaliwa kutokana na majawabu ya changamoto uliyoitatua.  

Juzi juzi hapa nilisema kuhusu mfumo wa afya wa nchi kubwa kama ya Marekani kuwa na changamoto ya kuwabagua watu maskini na wale wa tabaka la kati na kwamba unajenga matabaka makubwa sana yanayowanyima fursa sawa baadhi ya watu kwenye Jamii. Na kwamba ObamaCare inajaribu kutoa majibu yanayolenga kuleta usawa kwa kuwabana wenye kipato cha juu ili kuwahudumia wenye kipato cha chini. Tayari imeonekana kuwa kuna changamoto za kuwakamua zaidi watu wa daraja la kati, badala ya wale wa tabaka la juu kama 'design' na muundo wa awali ulivyolenga, kwa kuwatwisha mzigo wa watu maskini, na kwamba mpango huu kwa baadaye hautohimilika. Bado wanaendelea kubishana! Juzi tumeshuhudia Rais Trump amekwama kwenye jaribio la kuurekebisha. Kazi ya kutatua changamoto ipo na inaendelea kwenye Taifa kubwa la Marekani lenye miaka zaidi ya 200 ya demokrasia. 

Mfano, tazama changamoto mpya iliyokuja na sera ya CCM kutoa elimu bure mpaka kidato cha nne. Tamko hili la kisera limeleta changamoto nyingi za kiutekelezaji. Kwanza, limeleta urahisi kwa familia nyingi kuona hakuna sababu ya watoto wao, hata mmoja, kukosa elimu hii ya msingi. Wakati tunapitisha sera hii hatukujua kuwa kuna watoto wengi kiasi hiki tunachoshuhudia sasa walikuwa wakikosa fursa (missed opportunity) ya elimu kwa sababu ya vigharama vidogo vidogo. 

Tumeondoa gharama hizi tumekutana na ongezeko kubwa la watoto kuandikishwa shule. Mlipuko wa wanafunzi kuingia darasa la kwanza kwenye shule za msingi kwa wingi umezaa changamoto mpya za upungufu wa madawati, vyumba vya madarasa, idadi ya matundu ya vyoo, idadi ya walimu nk.   Wakati tukumbukeni vizuri kuwa juzi tu hapa Serikali ilikuwa inaajiri walimu kwa kipaumbele cha juu kabisa kwa miaka mitano mfululizo, ambapo walimu wote waliohitimu waliajiriwa! 

Uchumi wetu unakua kwa kasi nzuri, kama ni ndege ndiyo inaongeza spidi ili ipate nguvu ya kupaa; bado uchumi hauna uwezo wa kuhimili mahitaji yetu 'yote' ya matumizi ya kila siku kama tunavyotamani, achilia mbali ya kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kadri tunavyodiriki kuota ndoto zetu. Mfano: Kwenye ajira bajeti ya watumishi (wage bill) inaongezeka kila siku. Hili tu ni hitajio kubwa na nyeti sana la uchumi wetu. 

Zamani nilipokuwa Mbunge - bila userikali, kilichokuwa kinanikera ni kwamba, pamoja na changamoto tulizonazo watu wengine walikuwa wanaishi kama wako peponi na wengine wanaishi kama wako motoni, hawa wa peponi walifika huko kwa wizi, rushwa, ufisadi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi za umma, siyo kwa uchapakazi wala ubunifu. Tena bila huruma kwa waliokuwa wakiishi kama vile wapo motoni. Huku wakiwa na dhamana ya kuwaondoa motoni wananchi wenzetu waliobaki huko! 

Leo Rais JPM anakosolewa kwa kubana mianya ya rushwa, wizi, ubadhirifu wa mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka na uchumi wa ujanja ujanja, mambo ambayo nakumbuka mimi na wenzangu kwenye bunge la 10 tuliyapigia kelele kwa nguvu sana, tena kwa uzalendo wa hali ya juu na bila hata kuogopa kuwa tunapowashughulikia hawa ndugu wa peponi tunashusha imani ya wananchi kwa chama chetu pia. 

Sisi tuliamini kwamba hawa ni lazima tushughulike nao. Tuwaondoe ili kukisafisha Chama. Tulikuwa wachache sana. Tulipigana kuwaondoa watu wa aina hiyo na tuliwatoa. Na kwa kiasi kikubwa tulimkataa mwanaCCM mwenzetu, Ndg. Edward Lowassa, kwa sababu tuliamini yeye na kundi lake (lilikokuwa kubwa ndani ya CCM) wangeigawana na kuimaliza nchi yetu. Ilihitaji uwe mwendawazimu kumkataa ndugu huyu. Lakini tulikita mguu waziwazi na kumkataa. 

Tulionekana wasaliti wenye kustahili kufukuzwa Chamani. Na wengine tukifikia kufukuzwa Chama na baadhi ya viongozi wapuuzi, wakiamini viongozi wa aina yetu hatukutakiwa, mpaka vikao vya juu vilipopuuzia ndipo tulipona. Tulifika huku sababu kulikuwa na kundi la wachache waliokuwa wanafaidika na mfumo uliokuwepo, hivyo waliona sisi tunachafua maji yao ya kuogelea. Mpaka alipokuja Kanali Kinana na kutupongeza wabunge wa aina yetu akisema, jitengeni na ushenzi wa baadhi ya watu wanaochafua taswira ya Serikali ya Chama chetu ndipo tulipumua. 

Kuna njia mbili tu unaweza kutatua changamoto zinazotukabili nchini kwa 'uhakika'. Nasema kwa uhakika maana ni aibu kubwa kuinjika chungu cha ugali nyumbani kwako na kuwapa wanao uhakika wa ugali kumbe unategemea unga wa kuomba ama kuazima toka kwa jirani! Vipi akikunyima? 

Ukichaguliwa kuwa Rais, una ahadi na dhamana kubwa mabegani mwako, una hamu na shauku kubwa ya kuanza kuzitekeleza, una ndoto nyingi za kutaka kuleta mapinduzi kwenye nchi yako kwa heshima kubwa uliyopewa, unataka kuacha alama isiyofutika! 

Unachungulia hazina unakutana na madeni, mahitaji, utaratibu na masharti; unatazama makusanyo uliyonayo. Unachoka kabisa! Nguvu zinakuisha kabisa. Hamasa yako inavurugwa na uhalisia. 

Unakumbuka ushauri wa wabunge kila siku bungeni - 'tubane matumizi...tukate matumizi yasiyo ya lazima...tuweke kodi hii...ile...Serikali ni dhaifu kwenye kukusanya kodi....tutanue wigo wa kodi....kwa nini Tanzania na utajiri wote huu bado tunategemea misaada kutoka nje kwenye bajeti yetu - mwishowe tutapewa pesa zenye masharti magumu (mambo ya ushoga nk)...tuanzishe mahakama maalum ya mafisadi, nk!'

Unaanza kutekeleza yote haya kama yalivyo - unalaumiwa! Tusiwe wepesi wa kusahau. Tusiwe wanafiki. Ni nani hakuwahi kukerwa na watumishi hewa? Ni nani hakukerwa na safari za nje? Ni nani alilalamika kuhusu uwepo wa uwiano wa bajeti ya matumizi ya kawaida mkubwa kuliko bajeti ya maendeleo? Rais Magufuli toka aingie madarakani, haya ndiyo maswali anayojaribu kuyapatia majawabu. 

Njia za kupata fedha za kutatua changamoto kwa uhakika ni hizi mbili: moja - ubane matumizi, ili unacho-save ukipeleke kwingine kikasaidie kupunguza changamoto zako. Ndicho anachokifanya Rais Magufuli kila siku toka amechaguliwa. Sisi wenye macho ya kizalendo na kiuhalisia tunaona jitihada zake.

Mbili, ukusanye zaidi na ubane mianya ya kuvuja kwa mapato. Ndicho kinachofanyika. Kwa mwaka unaoisha makusanyo ya mapato ya Serikali yamepita malengo. 

Kuna njia nyingine za kupata fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji yetu. Japokuwa haina washabiki wengi na inapigwa vita sana na watunga sheria na wanaharakati mara nyingi. Hii ni ile ya misaada kutoka kwa wafadhili na mikopo (ya ndani na nje). Hizi njia mbili zote zinapigiwa kelele sana sababu; Moja, kwamba itasababisha tupewe pesa zenye masharti magumu tusiyoyaweza, na nyingine, kwamba deni letu linakua sana - mwisho halitohimilika! Njia ya mikopo ya ndani wanasema inaumiza uchumi wetu nk. 

Kwa sasa tunachotakiwa kufanya ni kuongeza uzalishaji ili wigo wa serikali kukusanya kipato chake utanuke zaidi. Na hili si la Rais peke yake, ni letu sote. Kila mtu awe mzalishaji. Shime twende shambani, twende viwandani, twende sokoni! 

Kwangu mimi, kama hali inakuwa ngumu kwetu sote na iwe tu, ili mradi wasiwepo kati yetu wanaofaidika na serikali ya watu huku wengine hawana chakula, hawana dawa, hawana madawati nk. Napenda usawa, haki na uwajibikaji. Namuunga mkono Rais wangu kwa sababu analeta usawa kwa watu wetu. Nasimama na Rais wangu.

Kwangu hili la usawa, haki na uwajibikaji kwa wote ni kubwa sana. Linagusa historia ya machozi, jasho na damu ya makuzi yenye maumivu makali na furaha nyakati nyingine kipindi cha makuzi yangu na watoto wengine wa maskini kwenye Tanzania ya miaka ya 70 na 80. Maana mimi ni zao la mfumo uliotoa haki na usawa kwa wote. Bila Tanzania hiyo mtoto wa maskini kama mimi, hata ningekuwa na bidii na kipaji cha namna gani, nisingefikia kusoma mpaka kuwa Daktari, na hata kufikia kutamani kugombea nafasi ya ubunge. Sitaki kufikiri labda ningekuwa wapi mimi leo! 

Tufanye kazi kwa bidii na maarifa, zama zimebadilika. Hakuna mtu atakayethubutu kutuibia kwenye zama hizi. Walau hili ni la uhakika. 

Na zile kesi za rushwa, wizi wa mali ya umma, matumizi mabaya ya ofisi na ubadhirifu wa mali ya umma sasa zifike kwenye mahakama yake na kesi zikimbie ili tuone haki ikitendeka. 

Huwezi kupanda mchicha ukasubiria ukuwe kwa matarajio ya kuvuna bangi. Tulimpa kura zetu Ndg. Magufuli, mwenye rekodi ya uchapakazi, uaminifu na uadilifu, basi tutarajie uchapakazi, uaminifu na uadilifu; mwenye rekodi ya kuacha alama ya kazi yake, basi ni lazima tutarajie kuona kazi itakayoacha alama. Si vinginevyo.

Tungempa mla rushwa, tungeshuhudia rushwa. Tumevuna tulichopanda. Tumevuna kazi tu. Tutulie tuone kazi. Tuamke tufanye kazi. Tushiriki kujenga Tanzania Tuitakayo. 
___________________________________

Imeandikwa na Dkt. Kigwangalla. Mwandishi ni Mwanafalsafa aliyegeuka kuwa Daktari, Mjasiriamali, Mwanasiasa na Mtunga Sera
www.ngarakwetu.blogspot.com

No comments:

Post a Comment