July 28, 2012
Kuunganishiwa umeme sasa kuanzia Sh180,000
NI KWA WALE WASIOHITAJI NGUZO, WA NGUZO MBILI KUTOZWA SH 800,000, WAZIRI MUHONGO, ASEMA MGAWO SAFARI HII HAUKUBALIKI
Boniface Meena, Dodoma
SERIKALI imetangaza kushusha gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo kwa viwango ambavyo ni kati ya asilimia 60 na 77 kwa wakazi wa vijijini na kati ya asilimia 29 na 65 kwa wananchi waishio sehemu za mijini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliliambia Bunge jana kuwa gharama za kuunganishiwa umeme kwa wateja walioko kwenye umbali usiozidi meta 30 (single phase) ambao hawahitaji nguzo sasa zitakuwa Sh177,000 kwa wateja wa vijijini na mijini itakuwa Sh320,960 badala ya Sh455,108 ambazo zilikuwa zikilipwa awali bila kujali mteja aliko.
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake ya 2012/2013 bungeni Dodoma jana, waziri huyo alisema punguzo hilo ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja waishio mijini.
Profesa Muhongo alisema pia Serikali imeshusha gharama za uunganishaji wa umeme kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) na kuwekewa nguzo moja katika maeneo ya vijijini ambao sasa watalipa Sh337,740 na mijini Sh515,618 badala ya Sh1,351,884 zilizokuwa zikilipwa awali.
“Punguzo hilo la pili ni sawa na asilimia 75.02 kwa wateja wa vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja waishio mijini,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini watalipa Sh454,654 na mijini watalipa Sh696,670 badala ya Sh2.001 milioni zilizokuwa zikilipwa awali.
“Punguzo hili ni sawa na asilimia 77.28 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 65.19 kwa wateja waishio mijini,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza. “Viwango hivyo vya gharama vitaanza kutumika Januari mwakani bila kisingizio.”
Chimbuko la Punguzo
Hatua ya kushushwa kwa gharama za kuunganishiwa umeme zimekuja zaidi ya mwaka mmoja tangu Rais Jakaya Kikwete alipolilekeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupunguza gharama hizo ili kupata wateja wengi zaidi.
Machi 18 mwaka jana, Rais Kikwete aliitaka Tanesco, kupunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi ili wengi wapate huduma hiyo sambamba na kuongeza wateja wanaotumia umeme kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.
Akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini, Rais Kikwete alisema gharama hiyo ikipunguza, itaiwezesha Tanesco kupata wateja wengi ikilinganishwa na sasa.
Kauli ya Rais ilitokana na maelezo ya Mkurugenzi wa Shirika hilo, William Mhando (ambaye sasa amesimamishwa kazi) kuwa Tanesco ilikuwa ikifanya mazungumzo na Benki za Akiba na Azania ili zitoe mikopo kwa wateja kwa ajili ya kuunganishiwa umeme.
Kadhalika Mei 16 mwaka huu, akizungumza na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt Profesa Muhongo alisema: “Kipaumbele cha wizara kwa sasa ni kupata umeme wa uhakika wa bei nafuu na unaotabirika. Ni muhimu kuongeza watumiaji wa umeme kwa kuwa kwa sasa kwa takwimu za Tanesco ni asilimia 18.4 tu ya Watanzania wanaopata huduma hii.”
Wizi Tanesco Profesa Muhongo aliwataka wezi wa umeme kujisalimisha kabla hawajakamatwa kwani hata wakijificha watakamatwa tu. Alisema upotevu wa umeme unafanywa na baadhi ya wananchi wanaoshirikiana na wafanyakazi wa Tanesco kwa kushirikiana na vishoka. “Kuna rushwa iliyokithiri Tanesco, kuna wezi wanaowaunganishia watu umeme na kuliibia shirika, wakae chonjo kwani watakamatwa tu,” alisema Profesa Muhongo. kuhusu wizara hiyo, alisema mambo mengi yatafanyika kwa uwazi na haoni sababu za kila jambo kuwa ni siri. “Mnakaribishwa wizarani kila mtakapoona mambo yanakwenda ndivyo sivyo, hatutakuwa na mambo ya kuficha tutakuwa wawazi,” alisema Profesa Muhongo.
Mgawo wa Umeme
Kuhusu suala la mgawo wa umeme, alisema hautakuwepo tena na haukubaliki kamwe.
“Waheshimiwa wabunge, suala la mgawo haliwezekani na halikubaliki,” alisema Profesa Muhongo. Alisema katika mwaka 2011/12, wizara iliendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuboresha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini. Profesa Muhongo alisema hadi Juni, 2012 uwezo wa mitambo ya kufua umeme (installed capacity) ulikua megawati 1,375.74 (gesi asilia ikiwa ni asilimia 40, maji asilimia 41 na mafuta asilimia 19).
“Uwezo huo ni ongezeko la megawati 367 sawa na asilimia 36 ikilinganishwa na uwezo wa megawati 1,013.74 uliokuwepo Juni, 2011. Mahitaji ya juu ya umeme kwa mwaka 2011/12 yalifikia wastani wa MW 820.35 ikilinganishwa na MW 730 kwa mwaka 2010/11,” alisema.
Alisema Julai, 2011 wakati wa Bajeti ya wizara hiyo ilipowasilishwa, nchi ilikuwa katika mgawo wa umeme... “Mgawo huo ulitokana na upungufu wa umeme wa takriban megawati 300 uliosababishwa na upungufu wa maji katika mabwawa kwenye vituo vya kufua umeme. Kutokana na hali hiyo, Serikali ililazimika kuandaa mpango wa dharura wa kuondoa mgawo wa umeme nchini ulioridhiwa na bunge.” Alisema katika mpango huo, megawati 572 zilipangwa kuzalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya taifa. Alisema hadi kufikia Juni, mwaka huu uwezo wa ufuaji wa umeme kutokana na mpango huo wa dharura ulifikia megawati 422.
“Mitambo hiyo inajumuisha Symbion megawati 137, Aggreko megawati 100, IPTL megawati 100 na mtambo wa gesi asili wa Ubungo megawati 150," alisema. Alisema kutofikiwa kwa kiwango kilichokusudiwa, kunatokana na kukosekana kwa mitambo ya megawati 150 ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) iliyokadiriwa kugharimu Dola za Marekani 162 milioni sawa na Sh256.20 bilioni. Alisema hadi kufikia mwishoni mwa Juni, mwaka huu lengo la kuondoa mgawo wa umeme lilifikiwa kwa asilimia 100.
“Kwa sasa hakuna mgawo wa umeme kwa kuwa upungufu ulikuwepo ulikuwa ni kati ya megawati 260 na megawati 300 ikilinganishwa na uwezo wa megawati 422 ulioongezeka,” alisema. Kamati ya Bunge
Kwa upande wake, Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Suleiman Zedi alisema pamoja na kamati yake kuishauri Serikali njia bora za kupunguza tatizo la umeme, bado hali ya upatikanaji wa umeme siyo ya kuridhisha.
“Sababu hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha ukosefu wa mvua za kutosha na hivyo kuathiri mitambo ambayo inatumia maji,” alisema Zedi. Alisema katika mwaka wa fedha 2011/12, uzalishaji wa mitambo ya maji ulikuwa asilimia 45 ya umeme wote uliozalishwa nchini ikilinganishwa na uwezo wake wa asilimia 51.
“Kamati ina hofu kuwa ifikapo miezi ya kiangazi ya Agosti mpaka Oktoba hatutaweza kuzalisha sehemu kubwa ya umeme utokanao na maji na hivyo kutegemea umeme unaozalishwa kwa gesi na mafuta tu,” alisema Zedi. Alisema kuwa kamati hiyo inaamini kuwa vyanzo vya umeme nchini vikitumiwa ipasavyo, upungufu wa umeme nchini utakuwa historia.
source:Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment