CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO Idara ya Habari ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), tangu ilivyopokea kwa masikitiko na
mshituko mkubwa taarifa za Serikali ya CCM, kufungia magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania, imeendelea kufuatilia kwa ukaribu hatua zinazochukuliwa na kauli
mbalimbali zinazotolewa na pande zote mbili, serikali na wadau wa uhuru wa
habari na vyombo vya habari.
Ni wazi bila shaka yoyote kuwa kwa mara nyingine tena,
serikali hii, imeendelea kutumia sheria mbaya, kutumia madaraka vibaya kufanya
uamuzi mbaya, kila inapokosa hoja na uwezo wa kukabiliana na sauti mbadala au
maoni kinzani.
Suala hili limekuwa dhahiri zaidi baada ya Serikali kuamua
hata kuanza kuingilia uhuru wa habari na maoni kwenye mitandao ya kompyuta (on line)
na pia kutishia kulifungia Gazeti la Rai, linalotolewa na Kampuni ya New Habari
(2006) Limited, kwa sababu limeanza kuchapiswa kila siku.
Wakati wamiliki wa gazeti hilo wametoa ushahidi unaotokana na
nyaraka za serikali hiyo hiyo iliyotoa idhini kwa chombo hicho kuchapishwa kila
siku, Serikali yenyewe kwa upande wake imetoa utetezi wa ajabu juu ya tishio
lake hilo ikijitetea kuwa kibali hicho kilitolewa kwa Kampuni ya Habari
Corporation iliyouza hisa zake kwa Kampuni ya New Habari (2006) Limited.
Katika hili serikali inajichanganya. Hii ni dalili ya wazi
kwamba uamuzi wake huo ni mwendelezo wa maamuzi ya kibabe, yasiyofanywa kwa
masilahi ya Watanzania, ndiyo maana yanaanza kuipatia tabu jinsi ya kujibu na
kujenga hoja za kutetea uovu wake.
CHADEMA, inapinga na itaendelea kupinga kwa kauli na vitendo,
hatua hii ya serikali yenye lengo ovu dhidi ya umma wa Watanzania.
Ni suala linalohitaji tafakuri yetu sote, kwa nini serikali
imeamua kuchukua hatua hii wakati huu ambapo nchi nzima iko kwenye mjadala wa Katiba
Mpya ambayo ni fursa adhimu ya taifa kujiumba upya na kuachana na sheria mbovu
kama hiyo ya mwaka 1976 inayompatia mamlaka waziri husika kufungia gazeti kadri
anavyoona 'yeye' inafaa.
Hoja si maudhui
Kama kawaida yake, serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Habari
Maelezo, Asa Mwambene, imeamua kuja na hoja ya 'maudhui' kuwa ndiyo uwe msingi
mkubwa wa kuhalalisha kitendo hicho kibaya cha kufungia magazeti kwa kutumia
Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.
Tunasema hapa hoja haiwezi kuwa maudhui yaliyosababisha
magazeti hayo kufungiwa kama ambavyo serikali ya CCM siku zote imejaribu
kuonesha kila inaposhughulikia vyombo vya habari, suala la msingi ni utaratibu
unaotumiwa kuvifungia.
Serikali haiwezi kuwa hakimu wa kesi yake yenyewe.
Halikadhalika haiwezi kufanya kazi zote; kulalamika, kutuhumu, u-polisi
(kupeleleza), kuendesha mashtaka na kisha kuhukumu. Hii ni kinyume kabisa cha
misingi ya haki ya asili. Ni ukiukwaji mkubwa wa haki.
Kama serikali ilifikiri vyombo hivyo vya habari vimekosea au
vimesema uongo, ilipaswa kusema ukweli ni upi, la sivyo ilipaswa kufungua
mashtaka kwa vyombo huru vinavyoweza kushughulikia masuala hayo; ama ingepeleka
malalamiko yake Baraza la Habari Tanzania (MCT), kama haina imani nalo (kinyume
na imani waliyonayo Watanzania wengi juu ya baraza hilo) basi ingeenda kushtaki
mahakamani.
Kinyume cha hapo ni kuendeleza uharamia dhidi ya uhuru wa
habari, vyombo vya habari na utoaji wa maoni.
Kitendo cha kutisha na kufungia vyombo vya habari kimekuwa ni
moja ya mbinu ya serikali hii kupambana na sauti mbadala, uhuru wa habari na
maoni. Safari hii, kimekuja wakati nchi na umma wote wa Watanzania, kupitia
taasisi, asasi na makundi mbalimbali ya kijamii, ukiwa umeungana kuhoji dhamira
ya watawala kutaka kuharibu na kukwamisha mchakato wa Katiba Mpya.
Hivyo hapa kuna masuala kadhaa;
• Vyanzo vyetu vya taarifa vimedokeza kwamba zipo njama za
baadhi ya watendaji wa serikali kufanya vitendo vya kutaka kuzuia sauti mbadala
zinazojaribu kupiga kelele kuuhabarisha umma juu ya uchakachuaji unaofanyika kwenye
mchakato wa katiba mpya.
• Hatua ya kufungia vyombo vya habari sasa hivi ni jaribio la
kuleta Kutia hofu vyombo vya habari visiripoti kwa uhuru mchakato wa Katiba
Mpya, hasa habari zenye mwelekeo wa kusema ukweli dhidi ya serikali au watawala
wanaotaka kukwamisha na kuharibu mchakato wa katiba mpya.
• Kutaka kuhamisha mjadala (diversion of discussion) mkali wa
katiba mpya unaoendelea kwa sasa, ili wananchi na taifa zima lianze kujadili
suala jingine, badala ya kuibana serikali, kisha watawala wapate ahueni ya
kupita katikati kutekeleza dhamira yao kwenye mchakato huo nyeti.
• Pia kitendo hiki kinakwenda sambamba kabisa na msimamo wa
CCM kwenye Rasimu ya Katiba Mpya, ambapo chama hicho, kimekuwa kikipinga
masuala mengi ya msingi na muhimu kwa wananchi, likiwemo suala la haki za
binadamu lisiwe jambo la muungano na uwazi usiwe miongoni mwa tunu za taifa
kwenye katiba mpya.
Serikali ilipaswa kuonesha au kuiga mfano katika uwajibikaji.
Mathalani, itakumbukwa kuwa Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya CHADEMA, ndiyo
taasisi pekee ya kisiasa nchini iliyosaini Azimio la Dar es Salaam Juu ya Uhuru
wa Uhariri na Uwajibikaji, lililopitishwa na Baraza la Habari la Tanzania
(MCT). Pamoja na ubora na upekee wa azimio hilo, barani Afrika na dunia nzima
kwa ujumla, si serikali wala viongozi wake ambao wameonesha kuunga mkono, ili
kuepuka vitendo kama hivi vya kidhalimu.
Idara ya Habari ya CHADEMA inapenda kutoa wito kwamba;
Makundi na wadau mbalimbali walioathirika na
kufungiwa kwa magazeti haya wajitokeze wazi, wapaze sauti zao
kuungana na makundi mengine ya kijamii, asasi za kiraia na kitaaluma
zinazopinga vitendo hivi. Hasa yale ambayo habari zilizoandikwa na Magazeti
hayo ya Mwananchi na Mtanzania, zilikuwa zikiyahusu, mathalani;
• Vyama vya wafanyakazi (Habari ya Mwananchi).
• Madhehebu ya dini (Habari picha ya Mwananchi).
• Wale wote walioathirika na vitendo ambavyo vyombo vya dola
vinatuhumiwa kuvifanya au kuzembea kuchukua hatua kubaini ukweli (habari ya
Gazeti la Mtanzania).
Mjadala huu wa kuitaka serikali kuacha kutumia sheria
mbovu na kandamizi na kuyafungulia magazeti haya mawili, utiwe uzito na uende
sambamba na ule wa kulifungulia Gazeti la Mwanahalisi ambalo serikali hii
iliyoamua kugeuka kuwa tishio kwa uhuru wa habari na vyombo vya habari, iliamua
kulifungia kwa muda usiojulikana.
Makundi mbalimbali ya kijamii ambayo yameungana
kwa dhati kwenye mchakato wa Katiba Mpya hasa kupinga dhamira ya serikali na
CCM, kutaka kuuharibu na kuukwamisha, kuzidi kuunganisha nguvu zao, kwani
mchakato bora utatupatia katiba mpya bora, ambayo itaondoa sheria mbovu kama
hii ya magazeti ambayo serikali imeendelea kuitumia kukandamiza umma wa
Watanzania.
Tutalaani na kuchukua hatua
Watawala baada ya kufungia vyombo vya habari kadhaa na jamii
kukaa kimya, mfano Gazeti la Kulikoni, Redio Imani, Redio Kwa Neema Fm, vingine
kwa muda usiojulikana mf; Gazeti la Mwanahalisi, sasa wamefikia mahali
wanafikiri wanaweza kuendelea na jamii ikakaa kimya.
Tutachukua hatua. Tutapinga kwa kauli na vitendo. Wakati
tukilaani na kutoa wito kwa makundi mengine ya wadau wote wa masuala ya habari
kushikamana kwa dhati kupinga jambo hili kwa namna wanazoona zinafaa, CHADEMA
kwa upande wake, kwa kuanzia, kinaunga mkono wabunge wake (Zitto Kabwe na John
Mnyika) ambao wameonesha nia ya kuchukua njia za kibunge, ili kufuta sheria
yote ya magazeti ya mwaka 1976 au baadhi ya vifungu vyake vinavyotoa mamlaka
mabovu yanayotumiwa vibaya na watawala kwa ajili ya malengo mabaya.
Hivyo, katika kufanikisha hatua hiyo, tunatoa wito kwa watu
wote walioguswa na kitendo hiki cha ukandamizaji, wakiwemo wabunge waunge mkono
njia itakayochukuliwa na wabunge wa CHADEMA.
Imetolewa , Oktoba 2, 2013, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene, Ofisa Mwandamizi wa Habari
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
No comments:
Post a Comment