August 8, 2014
Warioba atia hofu CCM
SOURCE:Tanzania daima
KITENDO cha wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba, kujitokeza katika mdahahlo na kujibu upotoshwaji ulioyokuwa ukifanywa na baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali ya CCM katika rasimu ya katiba mpya, kimetia hofu na sasa chama hicho kimetangaza kupambana nao.
Badala yake tume hiyo ambayo iliwajumisha makada wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), imegeuziwa kibao kwamba inaonesha hasira zao kwa kutumia kauli za dharau na kejeli kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.
Akizungumza na waandishi habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema kuwa mdahalo huo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere na kurushwa na kituo cha runinga cha ITV, ulitumika kuishambulia CCM.
Kwa mujibu wa Nape, wajumbe wa tume hiyo wamekuwa wakitumia muda mwingi kujaribu kupotosha umma na kuwashambulia wale wenye misimamo tofauti na mitazamo yao.
Alisema kuwa CCM hawatakaa kimya dhidi ya wajumbe hao na kwamba watawajibu kulingana na nguvu zilizotumiwa katika kufikisha ujumbe wanaoukusudia.
“Inaelekea Mzee Warioba na Tume yake wanaigeuza rasimu kuwa mradi binafsi ulioshikamanishwa na maisha yao, historia yao na heshima yao tofauti kabisa na utamaduni mwingine wa tume nyingine za katiba hapa nchini na duniani kote.
“Wajumbe hao wamekuwa walitumia lugha kali na hata vitisho kwa kutumia uzee wao kama walivyofanya mdahalo uliyopita, kusema wale wote wenye mitazamo tofauti na wa kwao,”alisema.
Nape alisema katika mdahalo huo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere wajumbe hao walimshambulia wazi wazi Rais Kikwete kwa maneno waliyodai kuwa hayakuwa na staa wala ustaarabu kwa madai ya kuingilia mchakato wa katiba na kuuharibu.
Katibu huyo aliongeza kuwa wajumbe wa tume wasitumie mgongo wa Tume kupenyeza ajenda zao na kwamba wanapaswa kuwa watulivu kama walivyovumiliwa wakati wakifanya kazi ya kukusanya maoni ya tume hiyo.
Kuhusu madai ya Rais kuingilia mchakato wa katiba kwa kulihutubia Bunge na kuonyesha msimamo wa chama chake, Nape alisema Rais hakuingilia mchakato huo bali alitekeleza wajibu wake na kwamba alichoongea ni matokeo ya namna alivyoona inawafaa wajumbe wa katiba.
Akizungumzia kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba kwamba ni wakati wa Bunge hilo kusitishwa kwa ajili ya kuokoa kodi za watanzania, Nape alisema haihusiani na chama na achukuliwe kama mjumbe mwingine yeyote.
“Mwiggulu aliongelea suala hilo bungeni, sisi kama chama tunataka bunge liendelee kwa kuwa hatuwezi kuacha masuala ya msingi kwa sababu ya uamuzi wa watu wachache kususa na ni kwamba hata akidi inayotakiwa inawezekana kwa kuwa kuna wabunge 148 kutoka Zanzibar walio bungeni kwa sasa,”alisema Nape
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment