August 4, 2012

Wanaharakati waendelea kupinga kufungiwa Mwanahalisi

 Wanaharakati waendelea kupinga kufungiwa Mwanahalisi
Pichani:-Mkurugenzi Mkuu wa Gazeti la Mwanahalisi, Saed Kubenea akizungumza na wanaharakati jana jijini Dar es Salaam juu ya hatua ya serikali kufungia gazeti lake likidaiwa kuchochea wananchi kujenga chuki dhidi ya serikali. Kulia Mratibu wa Mtandao wa kutetea Haki za Binadamu Tanzania (THRDs) Onesmo Olengurumwa Picha na Michael Matemanga




MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDs), wamepinga kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi huku wakiitaka Serikali kuacha kutumia Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kwa lengo la kuvifunga mdomo vyombo vya habari.

Mtandao huo unajumiisha wadau 22 ambao ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Haki madini Arusha, Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla (Sahringon), Kituo cha Msaada wa Sheria Zanzibar (ZLSC), Taasisi ya vyombo vya Habari vya Kusini mwa Afrika (MISA), Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela).

Wengine ni Jukwaa la Jamii ya wafugaji (TPCF), Waandishi wa Habari wa Haki za Binadamu, (Paicodeo)-Morogoro, (Tufae)- Songea, (Mvuha)-Shinynga, (Chaumta)-Geita, (Mfuma)-Shinyanga, (Jawawavi)-Rukwa, (SNDF)-Shinyanga.

Pamoja na Jukwa la Wahariri (TEF), Chama cha Maalbino Tanzania (TAS), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jumuia ya Elimu ya Haki za Binadamu na Amani- Mbeya, na PINGOS Forum-Arusha.

Akisoma tamko hilo mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam ,Mratibu wa mtandao huo, Onesmo Olengurumwa alisema ni wazi kwamba kulifungia gazeti la Mwanahalisi ni lengo la  Serikali kutaka kuleta hofu na  kuwanyamazisha wapigania haki za binadamu.

“Tunapinga kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi na kwamba tunaitaka Serikali kulifungulia gazeti hilo kwani hiyo ni njama ya kutaka kuwanyamazisha watetezi wa haki za binadamu,” alisema Olengurumwa na kuongeza:

“Tunawataka maofisa wa Serikali ambao wapo kwenye vyombo nyeti vya Serikali kufuata maadili ya kazi na kwamba wasikubali kutumiwa kwa lengo la kutaka kuwanyamazisha watetezi wa haki za binadamu,”alisema.

Olengurumwa alifafanua kwamba THRDs wameamua kuingilia suala hilo kwani wameona nia ya Serikali ni kuvizua vyombo vingine vya habari kutozungumzia masuala nyeti yenye maslahi ya umma.

“Ukiachilia mbali kuwapo kwa Mikataba ya Kimataifa,  Katiba ya nchi yetu inatoa uhuru wa kutoa maoni ila bado Serikali yetu imejifanya haioni jambo hilo kwani sheria ya 1976 ni kandamizi na inaondoa Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa kumpa  waziri mamlaka ya kufungia gazeti lolote jambo ambalo sio haki kwa vyombo vya habari,” alisema.
Kuchukua hatua
Akizungumzia hatua ambazo zitachukuiwa na Mtandao huo , alisema wao kama watetezi wa haki za binadamu wataendelea kudai haki mpaka pale gazeti hilo litakapofunguliwa.

“Hatuwezi kusema kwamba tutaenda Mahakamani au vipi kwani bado hatujashindwa kudai haki ya msingi ya kufunguliwa kwa gazeti hili na kwamba tutaendelea kupiga kelele kupitia watetezi wa haki za binadamu mpaka pale Serikali itakapolifungua,”alisema.

Waomba msaada UN.
Mtandao huo uliutaka Umoja wa Mataifa (UN), na Mawakala wake ikiwa pamoja na Balozi mbalimbali Tanzania na asasi za kikanda na Kimataifa kuchukua hatua katika suala hilo.

Akizungumizia msaada huo alisema ni wakati kwa Umoja wa Mataifa kuliona jambo hilo kuwa ni la msingi na wanatakiwa kuchukua hatua kwani hiyo ni moja ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kuwanyiwa watanzania uhuru wa kupata habari.

“Tunaamini kwamba UN itachukua hatua dhidi ya jambo hili kwani kumnyima Mtanzania uhuru wa kupata habari ni kinyume na haki za binadamu,” alisema.

Taasisi za Dini
Alisema kwa upande wa Taasisi za dini, wanahabari, watetezi wa haki za binadamu, asasi za kiraia wanapingana na rushwa, ukiukwaji wa haki na utendaji mbovu wa Serikali.

 “Tunaomba Taasisi za dini kuungana pamoja kuwatetea watetezi wa haki za binadamu kwani jambo la kulifungia gazeti la Mwanahalisi kwa madai ya kuandika habari za uchochezi sio za kweli,” alisema.
Kubenea anena
Akizungumza  na waandishi wa habari jana akiwa kama miongoni wa wadau wa Mtandao wa haki za binadamu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali halisi , inayochapisha Gazeti la Mwana Halisi, Saed Kubenea, alisema siyo vyema kulifungia gazeti hilo kwani habari zinazoandikwa zinafuata maadili na taaluma ya uandishi wa habari.

“Mimi sioni kama gazeti la Mwanahalisi linaandika habari za uchochezi kama zinavyo daiwa lakini hiyo ni njama ya mtu ambaye analengo la kutaka kuwafunga mdomo waandishi wa habari ili wasieleze mambo ya kweli jambo ambalo  halikubaliki,” alisema na kuongeza:

“Nipo tayari kufa lakini nitaendelea kutetea haki za watanzania mpaka mwisho wangu,” alisema.
Mwisho.

Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment