Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu |
WATUHUMIWA watatu wa ujambazi wameuawa baada ya kurushiana risasi na
polisi katika eneo la Igogo jijini Mwanza, katika jaribio la kuvamia Kituo cha
Mafuta cha GBP.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, alisema jaribio hilo lilifanyika
juzi kati ya saa 2 na 3 usiku, katika kituo hicho cha mafuta kilichopo katika
barabara ya Kenyata.
Alisema majambazi ambao idadi yake haikufahamika mara moja, baada ya
majibizano ya risasi na polisi, wengine walitoroka lakini askari Polisi walifanikiwa
kukamata bunduki moja aina ya SMG, yenye namba ya usajili 2916 pamoja na risasi
saba.
Akifafanua, Mangu alisema walipokea taarifa kutoka kwa raia wema juu ya
kuwepo kwa majambazi kutoka Ngara yaliyopanga njama ya kuvamia kituo hicho cha
mafuta.
Alisema majambazi hayo yalipofika katika eneo la tukio na kujiandaa
kuvamia kituoni hapo, polisi nao walijitokeza, ndipo walipoanza kurushiana
risasi na majambazi hao, ambapo watuhumiwa watatu waliuawa huku wengine
wakitokomea kusikojulikana.
Katika eneo la tukio kwa mujibu wa Kamanda Mangu, yaliokotwa maganda ya
risasi 22 huku miili ya watuhumiwa ikihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya
Bugando na Polisi mkoani hapa linaendelea na uchunguzi.
Kamanda Mangu ametoa mwito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri
kwa jeshi hilo, ili lizuie matukio ya uhalifu.
Katika tukio lingine, watu wasiojulikana wameteketeza kwa moto nyumba
tisa za nyasi za familia moja katika kijiji cha Nyehunge wilayani Sengerema
mkoani Mwanza.
SOURCE:Habari Leo
No comments:
Post a Comment