October 23, 2012

Elimu bila Maktaba wanafunzi hawatafaulu kwa viwango bora

Mh Mbunge wa jimbo la Ngara Deogratias Ntukamazina wakati akizungumza na ngarakwetublogspot


Na: Shaaban Ndyamukama. Ngara
Mbunge wa jimbo la Ngara mkoani Kagera  Deogratias Ntukamazina ameitaka halmashauri ya wilaya ya Ngara kutafuta jengo kwa ajili ya kuanzisha maktaba ili wanafunzi na jamii kwa ujumla wapate sehemu ya kupata taarifa za kitaaluma
Bw Ntukamazina alisema hayo hivi karibuni katika kikao cha dharula cha Halmashauri ya wilaya ya Ngara wakati wa kujadili walaka wa TAMISEMI kutoka Ofisi ya waziri mkuu Mizengo Pinda kuhusu mabadiliko ya kanuni za kufanya vikao kwa baraza la madiwani kote nchini
Alisema kuwa wanafunzi wengi na taasisi mbalimbali hukosa taarifa za msingi kwa kukosa maktaba na hatimaye kupoteza kumbukumbu pasipokuwa na mahali pa kufanyia rejea ikiwa ni pamoja na walimu wa shule za msingi na sekondari
Alidai kuwa halmashauri ifanye jitihada ya kutafuta jingo hilo kuwekeza katika elimu ili baadaye watakaotumia maktaba hiyo wawe ni wataalamu wa baadaye katika Halmashauri yao
“Wanafunzi wengi wanakosa maarifa kitaaluma na kusababisha kufanya vibaya katika mitihani yao kwa kuwa hakuna  maktaba zilizo na  nyaraka mbalimbali  ambazo baadhi yake hutumika katika kujibia mitihani kwenye ngazi Fulani ya elimu”.Alisema Ntukamazina
Alisema kwamba kwa sasa ameshatafuta wafadhili wa kuleta vitabu vya masomo ya sayansi kwa shule za sekondari na tayari kampuni ya Kabanga nickel imeonesha mfano kwa kugawa vitabu mbalimbali kwa shule zilizoko eneo la mradi wao kwa shule za msingi na sekondari na yeye amegawa vitabu 1500 kwa baadhi ya shule wilayani humo
Aidha aliongeza kuwa juhudi zake ni kutafuta  walimu wa sayansi ambapo hadi sasa ameleta walimu kutoka marekani wanaofundisha shule ya sekondari Muyenzi, Nyakisasa  Ngara ,Murugwanza  pamoja na Bukiriro  kwa somo la Mathematics, Physics, Chemistry, English na Biology.
Aliwasihi wanafunzi na wananchi kwa ujumla kujenga tabia ya kujisomea vitabu mbalimbali vinavyotolewa na serikali na taasisi mbalimbali wakiwemo wadau wa elimu ili kujifunza maarifa  ya ndani na nje ya nchi
Katika kikao hicho madiwani wa halmashauri zote nchini yameongezewa muda wa kufanya vikao  na kuboresha kanuni za vikao hivyo ili kuleta ufanisi katika kuteleleza miradi ya maendeleo ya wananchi
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngara mkoani Kagera John Shimilimana alisema waraka   kutoka ofisi ya waziri mkuu unafafanua kuwa vikao vya baraza la madiwani vitakuwa vya siku mbili badala ya siku moja na kila diwani atatoa taarifa ya shughuli mbalimbali zinazofanyika katika kata yake kwenye kikao cha kwanza cha baraza. Shimilimana alisema kuwa  diwani atakayeshindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo atawajibishwa kwa kukatwa asilimia 10 ya posho yake ya mwezi na kuzuiwa kuhudhuria baadhi ya vikao ambavyo atakuwa ni mjumbe
  Aidha alidai kuwa serikali imeboresha posho za madiwani kutoka shilingi laki moja na elfu 20 hadi laki mbili na nusu ikiwa ni pamoja na posho za madaraka kwa wenyeviti wa halmashauri na wale wa  wenyeviti wa kamati za kudumu walioboreshewa posho kulingana na ngazi ya halmashauri husika
Naye Diwani wa kata ya Ntobeye Bw John Ruzige aliongeza kwa madiwani wenzake akiwashauri kuwajibika kusimamia maendeleo ya wananchi kwa kukagua na kujiridhisha na miradi mbalimbali kwa kushirikiana na wataalam bila kupata taarifa za mdomo na tayari seikali imekubali kuwakopesha vyombo vya usafiri hadi eneo la miradi katika kata zao

No comments:

Post a Comment