November 12, 2012

Akutwa amekufa kwenye shamba Darasa-Ngara



 Na Shaaban Ndyamukama- Ngara

 Mtu mmoja ambaye hakutambulika jina lake anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya  45 hadi 50 amekutwa amekufa katika mji mdogo wa Rulenge wilaya ya Ngara mkoani kagera jumapili  mwishoni mwa wiki iliyopita

Diwani wa kata ya Rulenge wilayani Ngara Bw Hamisi Baliyanga amesema mtu huyo wa jinsia ya kiume alikutwa amekufa katika shamba darasa la kilimo katika mji wa Rulenge bila kuwa na majeraha yoyote kwenye mwili wake.  Bw Baliyanga amesema mara baada ya kutolewa taarifa za mtu huyo katika kituo cha polisi Rulenge viongozi wa kijiji walimtafuta mganga ambaye alifanya uchunguzi na kubaini kuwa chanzo cha kifo kimesababishwa na njaa

 Amesema serikali ya kijiji cha Rulenge haina sehemu iliyotengwa kwa ajili ya makaburi hivyo mwili wa marehemu umezikwa karibu na kingo za barabara kuu kwani asingeachwa bure na mwili wake kuweza kuharibika
Aidha diwani huyo ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa za watu wanaoingia kwenye maeneo yao bila kujulikana wapi wanatokea ili serikali iwahoji na kuwarudisha makwao kuondokana na usunbufu unaojitokeza.

 Mji wa Rulenge wilaya ya Ngara umekuwa ukikumbwa na matukio ya kukutwa watu wamekufa pasipokujulikana makazi yao na hilo ni tukio la nne mwaka huu na kusababisha hofu kwa wananchi ambapo jeshi la Polisi limethibitisha kutokea kwa kifo cha mtu huyo.     Mwisho

No comments:

Post a Comment