February 28, 2013

YAMETIMIA-PAPA ANG'ATUKA




Safari ya miaka saba ya Baba Mtakatifu Benedict XVI inakamilika leo pale atakapong’atuka rasmi katika uongozi wa Kanisa Katoliki, ifikapo saa 2:00 usiku kwa saa za Italia (saa 4:00 usiku kwa saa za Tanzania).

 

 

Kwa siku mbili, Papa amekuwa na shughuli nyingi katika makao yake, Gandolfo Castel, Vatican akijiandaa kimwili kuondoka, akiweka sawa nyaraka zake binafsi na zile za kanisa ambazo zitawekwa katika kumbukumbu.

 

 

Kwa upande mwingine Vatican, nchi ambayo ipo ndani ya Jiji la Rome iliyozungukwa na ukuta, ikiwa na ukubwa wa hekta 44 na wakazi 832 pekee, imekuwa katika hekaheka nyingi.

Jana, waumini zaidi ya 50,000 na wengine wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiwamo makardinali, maaskofu, mapadri na walei walialikwa kwa shughuli rasmi ya kumuaga kiongozi huyo.

 

 

Tofauti na kanuni yake, leo Benedict hatavaa viatu vyekundu kama ilivyozoeleka na badala yake amechagua viatu rahisi vya ngozi vilivyobuniwa Mexico. Alipewa viatu hivyo ikiwa ni zawadi wakati wa ziara nchini humo 2012.

 

 

Tangu alipotangaza uamuzi wake wa kung’atuka Februari 11, mwaka huu, utata umegubika nafasi yake katika maisha mapya ndani ya Vatican, akiitwa Papa Mstaafu.

 

 

Waumini, wataalamu na hata viongozi mbalimbali wa Kikatoliki wameanza kuhoji ni jinsi gani viongozi wawili (Papa) wataishi, huku wote wakivaa mavazi meupe wakiitwa Papa, wakiishi umbali mdogo kati yao, wakiwa na wasaidizi wengi wanaowahudumia.

 

Vatican

Nje ya Gandolfo Castel, ulinzi umeimarishwa na vibali vya kuingia Vatican vimesitishwa.

Juzi, Vatican ilitangaza kwamba Papa Benedict XVI atajulikana kama ‘Emeritus Pope’, yaani Papa Mstaafu mwenye cheo cha heshima, akiendelea kuitwa, ‘mtakatifu’ na ambaye ataendelea kuvaa nguo nyeupe.

 

 

Mavazi na hata jina lake jipya ni masuala ambayo yamezua uvumi mwingi, huku suala la mrithi wake mpya pia likiwa gumzo, kwani tukio kama hilo lilitokea miaka 600 iliyopita.

Ni uamuzi uliolishtua kanisa hilo lenye waumini 1.2 bilioni duniani na wengi wanasema awali, haikushauriwa Papa kustaafu kwani kwa kufanya hivyo kunaacha mizozo na minong’ono ya kuwania madaraka.

 

 

Hata hivyo, uongozi wa Vatican umesisitiza kuwa uamuzi huo wa Papa Benedict XVI ni wa kipekee na hakuna mzozo ambao utatokea baina yake na mrithi wake ambaye mchakato wa kumpata unatarajiwa kuanza ndani ya wiki mbili zijazo.

 

 

“Kulingana na mabadiliko katika kanisa letu, kuna Papa mmoja. Ni dhahiri kwamba katika hali ya sasa hakutakuwa na tatizo,” anasema Mhariri wa Gazeti la L’Oservatore Romano linalomilikiwa na Vatican, Giovanni Maria Vian.

 

Hofu iliyopo

Hata hivyo, wakosoaji wa mambo hawakubaliani na hoja hiyo na baadhi ya makardinali walioko Vatican kwa usiri mwingi, wanazungumzia suala hilo wakieleza kwamba litazua tatizo kubwa kwa Papa ajaye, hasa ikiwa mtangulizi wake, Benedict akiwa bado hai.

 

 

Mtaalamu wa tauhidi (theolojia), raia wa Uswisi, Hans Kueng ambaye amekuwa mtu wa karibu wa Papa Benedict XVI, ingawa kwa sasa ni mkosoaji wake amesema:

“Kwa sasa, Benedict XVI akiwa bado hai, kuna hatari ya kuwa na Papa kivuli, mwenye mamlaka kamili ambaye kwa chinichini anaweza kumshinikiza mrithi wake kufikia uamuzi.”

Hans Kueng alisema hayo alipozungumza na Gazeti la Der Spiegel la Ujerumani.

 

 

Msemaji wa Vatican, Padri Federico Lombardi alisema Papa Benedict XVI kwa upande wake aliamua aitwe Papa Mstaafu au ‘kiongozi mstaafu wa Roma.’ Anasema haelewi ni kwa nini ameamua kuacha jina lake la sasa la Askofu wa Rome.

 

 

Kwa wiki mbili zilizopita, maofisa mbalimbali wa Vatican wamekuwa wakifikiri kwamba Papa angeanza kuvaa mavazi meusi na kutumia jina la Askofu Mstaafu wa Rome ili kuepuka mkanganyiko na mrithi wake.

WAKATI HUO HUO, PAPA ANASEMA ILIKUWA DHORUBA


Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Benedict XVI, alijitokeza jana kwa mara ya mwisho mbele ya maelfu ya waumini wake katika viwanja vya Mtakatifu Petro na kuzungumzia uongozi wake huku akieleza kwamba ulikuwa na nyakati za dhoruba na furaha.

Papa Benedict XVI aliwahutubia maelfu ya Wakatoliki katika mkesha wa kihistoria wa kujiuzulu kwake kama kiongozi wa Wakatoliki bilioni 1.2 kote ulimwenguni.

Mbele ya umati wa watu Papa Benedict XVI alizungumzia nyakati za mapambano na pia za furaha wakati wa hotuba yake ya mwisho kwa umma katika viwanja vya Mtakatifu Petro.
Katika ujumbe wake binafsi usiyo wa kawaida, alisema kuwa kumekuwa na “siku nyingi za nuru” lakini pia “nyakati za dhoruba kali”.

“Hata kama kanisa likipita kwenye bahari yenye dhoruba kali kiasi gani, Mungu hawezi kuliacha lizame,” alisema Papa ambaye anajiuzulu rasmi leo na kutoa nafasi kwa makardinali wa kanisa hilo kuanza mchakato wa kumpata mrithi wake.

Maneno hayo yametafsiriwa na wengi kama maoni yake juu ya kashfa ya unajisi wa watoto na madai ya rushwa ambayo yaliibuka wakati wa uongozi wake.

“Ilikuwa ni sehemu ya safari ya kanisa kwamba limekuwa na nyakati za furaha na nuru, lakini pia wakati ambao haukuwa rahisi,” alisema.

Papa aliwashukuru makardinali, makasisi katika Roma, maofisa wa Vatican na mapadre duniani kote kwa kazi zao, pamoja na sharika zao na kueleza kuwa alichukua uamuzi wa kustaafu ‘kwa amani ya ndani ya akili yake’.

“Kupenda kanisa pia ina maana ya kuwa na ujasiri wa kufanya uamuzi mgumu,” alisema na kuomba waumini hao wasali kwa ajili yake na Papa mpya.

Alisema maisha yake baada ya kustaafu yatarudi mahali binafsi na kusema: “Siyo maisha ya kusafiri, kuhudhuria mikutano na makongamano wala kufuta cheo cha Papa.”
Mahujaji walianza kukusanyika katika viwanja hivyo mjini Vatican mapema jana, ili kumuaga Papa mwenye umri wa miaka 85 ambaye alitangaza nia ya kujiuzulu Februari 12, mwaka huu kwa kusema kuwa alikuwa mdhaifu sana kuendelea na uongozi wake katika ulimwengu wa sasa.

Makao makuu ya kanisa Katoliki yamesema takribani watu 50,000 wamenunua tiketi za kuhudhuria hafla hiyo, lakini wengine wengi huenda wakajitokeza na hivyo maofisa wamejiandaa kuwakaribisha watu 200,000.

Vifaa vya ukaguzi vimewekwa katika eneo hilo, pamoja na walenga shabaha na kuweka maeneo ya kliniki.

Hafla hiyo ilianza kwa Papa kuzuru mji wa Vatican akiwa ndani ya gari maalum nyeupe, na kutoa hotuba yake ya mwisho kwa waumini wake wa jimbo la Roma na ulimwengu mzima.
Makardinali kutoka kote ulimwenguni wataanzisha mikutano kujadili kuhusu masuala muhimu ya kanisa Katoliki, kuweka tarehe ya mkutano wa kumchagua Papa mpya na kutathmini orodha ya wagombea wanaoweza kuchukua nafasi ya Papa Benedict XVI.

Mapema mwezi huu Papa alipotangaza kustaafu, alisema atajishughulisha zaidi na sala.
Misa yake ya mwisho ya jana ilihudhuriwa na zaidi ya waumini 150,000 kutoka kila pembe ya dunia.

Wakazi wa jimbo la Kusini mwa Ujerumani Bavaria anakotokea kiongozi huyo wa kanisa Katoliki ulimwenguni walihudhuria kwa wingi kumuaga jamaa yao. Katika misa yake hiyo ya mwisho ya hadhara kama kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni, Papa Benedict XVI akiwa ndani ya gari maalum la Vatican aliusalimia umati wa waumini uliojitokeza katika viwanja vya Mtakatifu Petro muda mrefu zaidi kuliko kawaida yake kabla ya kuwakaribisha kwa mazungumzo baadhi ya viongozi ikiwa ni pamoja na Rais Ivan Gasparovic wa Jamhuri ya Slovakia.

Miongoni mwa waumini hao kuna wale wanaotokea katika jimbo la Kusini la Bavaria, wakibeba bendera za jimbo hilo na kupiga muziki wa Bavaria ambao mwenyewe Joseph Ratzinger (Papa) anapenda kuusikia ukichezwa.

Siku kadhaa zilizopita, umati wa waumini kutoka Ujerumani wamekuwa wakimiminika mjini Roma. Wenyewe wanasema hata akiacha wadhifa huo ataendelea kuwa muhimu kwao.
Tobias Eichinger, aliyekwenda Roma pamoja na mchumba wake Cornelia alisema:
“Tunataka kumuombea Papa mtakatifu ambaye ni wa kutoka Bavaria na pia ni mwenzetu, kila la kheri.”

Mshika bendera wa kundi la waumini wa Bavaria, Helmut Jawurek, anahisi uamuzi wa Papa Benedict XVI kimsingi ni sawa. Anasema ataendelea kuwa mtiifu kwa kiongozi mwingine wa kanisa Katoliki ulimwenguni atakayechaguliwa na makardinali mwezi ujao.
“Kanisa Katoliki ni kanisa la dunia na uraia si muhimu, la muhimu zaidi ni imani,” alisema.

Baada ya uamuzi wa Papa Benedict XVI kutangaza nia ya  kujiuzulu, Kanisa Katoliki limejikuta katika hali ambayo halijawahi kuwamo kwa kipindi cha takribani miaka 700.
Ni washauri wachache tu walio karibu na Papa, ambao walijua mpango wake wa kujiuzulu kabla ya kutangazwa hadharani. Hata vigogo katika uongozi wa Vatican walishtushwa na uamuzi huo.

Kitendo cha kuamua kujiuzulu kwa Papa kumeibua maoni mbalimbali kwa Wakatoliki huku wengine wakieleza kwamba uamuzi wake ni wa kishujaa na utaleta nguvu mpya katika kanisa hilo na pengine kumaliza mtindo wa kuwachagua wakongwe kuliongoza kanisa hilo.

NI VIGUMU KUTABIRI MRITHI
Baada ya ibada ya jana ya Papa kuwaaga waumini wa kanisa hilo, mchakato wa kumtafuta mrithi wake utaanza kupitia utaratibu ule ule unaotumika pindi Papa anapofariki. Kwa sasa nafasi ijulikanayo kama kiti cha Petro itakuwa wazi na kanisa litakuwa na siku kati ya 15 na 20 kumchagua Papa mwingine.

Uvumi kuhusu nani anaweza kuchaguliwa kuwa Papa mpya ulianza mara tu baada ya Papa anayeondoka kutangaza uamuzi wake. Lakini, hata wale wenye uzoefu mkubwa katika masuala ya Vatican wametoa tahadhari kwamba si rahisi kutabiri nani atachaguliwa.

Vatican imesema inatarajia kuwa Papa mpya atajulikana kabla ya siku kuu ya Pasaka, ambayo ni Machi 31, ingawa kila kitu kitategemea mkutano wa faragha wa makardinali.

Inakadiriwa kwamba takribani makardinali 115 kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni watapigakura ya kumchagua mrithi wa Papa Benedict XVI.

Aidha, uongozi huo umesema kwamba atabakia na cheo chake cha Papa Benedict XVI na kwamba hatarejea kwenye jina lake la ubatizo la Joseph Ratzinger. Pete yake ambayo ni nembo ya wadhifa huo itaharibiwa mara tu atakapokabidhi ofisi.

Uongozi wake wa miaka minane aliyoushikilia wadhifa wa Papa ni moja ya vipindi vifupi katika historia ya wadhifa huo.  Hata hivyo, kipindi hicho kilitosha kumpatia Papa Benedict XVI maadui wengi, wakiwamo mashoga na wanaharakati wa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi. Katika kipindi hicho pia kashfa nyingi za visa vya mapadre kuwanajisi watoto zilifichuliwa

No comments:

Post a Comment