July 5, 2015

Zitto aanika majina ya walioficha mabilioni Uswisi

Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mwembeyanga, Dar es Salaam Julai 4,2015.
SOURCE: MWANANCHI,

Dar es Salaam. Kiongozi mkuu wa chama chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe Julai 4 mwaka huu  alianika orodha ya majina ya watu wanaotuhumiwa kuhodhi akaunti zenye mabilioni ya fedha nje ya nchi, lakini akasita kuyataja kutokana na sababu za kisheria.
Zitto aliwapa waandishi wa habari orodha hiyo akisema waende kufanyia kazi kwa kuwahoji wahusika kulingana na taaluma yao.
Orodha hiyo ina majina yenye asili ya kiasia isipokuwa wachache ambao wanaonekana wana majina ya kibantu.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, Zitto alisema: “Majina ninayo haya hapa niwataje nisiwatajee! Ni wengi sana wengine wanamiliki kampuni kubwa.”|
Alisema Zitto alisema wamejaribu kuishinikiza Serikali ichukue hatua, lakini inaonekana kutotaka kufanya hivyo na kwamba anaamini waandishi wa habari kwa kutumia taaluma yao wataweza kuwaanika wahusika.
Wakati maofisa wa ACT wakigawa orodha ya majina hayo, wananchi walionekana kuwa na shauku ya kupata nakala ya karatasi hiyo yenye majina 99 ya wafanyabiashara hao maarufu ndani na nje ya nchi, lakini kiongozi huyo hakuwa tayari kuwapatia na badala yake akiwaambia wasome magazeti ya kesho (leo).
Zitto alisema kwamba kati ya majina ya raia hao wenye mabilioni ya fedha nchini Uswisi, kuna wengine wanamiliki kihalali lakini wengine wamejirundikia isivyo halali.
‘’Nimeamua leo kuiweka orodha hii wazi kama shinikizo kwa Serikali kutoa taarifa ya uchunguzi kabla ya Bunge kuvunjwa wiki ijayo. Kila mwandishi wa habari aliyepo kwenye mkutano huu nimempatia nakala yenye majina 99 ya Watanzania au watu wenye uhusiano na Tanzania ambao wana akaunti HSBC ya Uswisi. Jumla ya akiba katika akaunti benki hii pekee ni Dola 114 milioni za Marekani,’’ alisema.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa ametawazwa kuwa chifu wa mkoa na wazee wa Dar es Salaam na kuitaka serikali kuhakikisha inawarudishia wananchi chenji zinazotokana na ufisadi wa Escrow , EPA na Richmond. Akizungumza katika kongamano hilo la wazee la kutafakari uchaguzi wa mwaka 2015, Dk Slaa alisema ingawa wazee waliungana na Hayati Mwalimu Nyerere kupambana na maadui wa tatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi lakini kwa sasa ameongezeka adui wa nne ambaye ni ufisadi.
“Ujinga alioupinga Mwalimu na wazee umeondoka? Lakini ujinga, umaskini na maradhi na kuna adui wa nne ambaye ni ufisadi,” alisema.
Alisema hakuna Mtanzania ambaye atakwenda dukani na Sh10,000 kununua chumvi na kibiriti halafu akaacha chenji yake dukani kwa makusudi na hivyo Watanzania bado wanadai fedha zao zilizopotea kutokana na ufisadi.
Kadhalika Dk Slaa alisema kitendo cha wazee hao kukutana katika kongamano hilo kinaashiria kuwa wana kiu, njaa na matumaini ya kutaka mabadiliko

No comments:

Post a Comment