July 26, 2015

Rais wa UKAWA hadharani

Viongozi wa UKAWA wakitia saini makubaliano yao waliyokubaliana


JUMUIKO la vyama vinavyounda muungano wa kutetea katiba ya Wananchi (UKAWA), linatarajiwa kumtangaza mgombea wake urais jioni hii, jijini Dar es Salaam. Anaandika Saed Kubenea
Taarifa kutoka ndani ya umoja huo zinasema, mgombea urais wa UKAWA aweza kupatikana leo, baada ya mashauriano ya kina yaliyofanyika baina ya viongozi wakuu wa vyama vinavyounda umoja huo.

“Jioni hii ya leo, tutakuwa na mkutano na waandishi wa habari kwa lengo la kumtangaza mgombea wetu wa urais. Tutatangaza moja kwa moja mgombea au tutakitangaza chama ambacho kitatoa mgombea,” ameeleza mmoja wa viongozi wakuu wa UKAWA kwa sharti la kutotajwa gazetini.
Amesema, “ikiwa tutakitangaza chama, basi kitakachofuata, ni kukiruhusu kuendelea na mchakato wake wa ndani. Lakini katika hayo mawili, moja lazima litafanyika – tutangaza mgombea au chama kitakachotoa mgombea.”
Mkutano wa viongozi wakuu wa UKAWA unaotarajiwa kutangaza mgombea wake urais, umepangwa kufanyika katika hoteli ya Bahari Beach.
Vyama vinavyounda muungano wa UKAWA, ni NCCR- Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na National Democrat Party (NLD).
Kwa mujibu wa mtoa taarifa wa gazeti hili, chama ambacho kitatoa mgombea urais wa Muungano, kimetajwa kuwa Chadema. Mgombea urais wa Zanzibar, atatoka CUF.
Anasema, makubaliano kuwa Chadema ndicho kitoe mgombea urais wa Muungano tayari yameridhiwa na Baraza Kuu la Uongozi la CUF, lililokutana mjini Zanzibar jana Jumamosi.
Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, hatua ya CUF mmoja wa washirika wakubwa katika umoja huo kuridhia Chadema kutoa mgombea urais, limekuwa pigo kubwa kwa wapinzani wa muungano huo.
“Haya mawili ya rais wa Muungano na rais wa Zanzibar, tayari tumekubaliana. Chadema kitatoa mgombea urais wa Muungano na CUF kitatoa mgombea mwenza. Mbali na mgombea mwenza, CUF kitatoa pia mgombea urais wa Zanzibar,” anaeleza kiongozi huyo.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya Chadema zinasema, chama hicho kinaweza kuzuia kumtangaza mgombea wake wa urais katika mkutano wa leo na waandishi wa habari, ili kukamilisha mazungumzo yake ya ndani.
Kinachoitwa na chama hicho, “mazungumzo ya ndani,” kimetajwa na afisa mmoja wa Chadema kuwa ni  suala la kuchelewa kupatikana jina la mgombea mwenza kutoka CUF.
Aidha, taarifa zinasema, kushindwa kwa chama hicho kumtangaza mgombea wake urais wa Muungano, kunatoka pia na kutokamilika kwa “mashauriano” kati yake na mmoja wa watu muhimu nje ya chama hicho.”
Lakini kwa zaidi ya wiki mbili sasa, vyombo vya habari vimenukuu vyanzo mbalimbali vya taarifa vikieleza, anayesubiriwa na Chadema kutoka nje ya chama, ni mbunge wa Mondoli (CCM), Edward Lowassa.
Taarifa kuwa Lowassa, mmoja wa wanasiasa machachari nchini, anataka kujiunga na Chadema, zimepamba moto katika wiki za hivi karibuni baada ya jina lake kuenguliwa katika hatua za awali katika kinyang’anyiro cha urais kupitia CCM.
Tayari madiwani 20 na viongozi wengine mbalimbali wa CCM wamekihama chama hicho na kujiunga na Chadema, jambo ambalo limeashiria kukamilika kwa safari ya kiongozi huyo ndani ya Chadema.
SOURCE: http://mwanahalisionline.com/rais-wa-ukawa-hadharani/

No comments:

Post a Comment