January 21, 2013

Tuzungumzie Kili,Kilimo ni Mali 

 

 


 

 

 

 


 

 

KILIMO CHA VIAZI MVIRINGO

 

 

 

  

 

 

 
UTANGULIZI

Viazi mviringo ni zao muhimu la chakula na biashara katika nchi nyingi zilizoendelea na zinazoendelea. Viazi husitawi vizuri sehemu za miinuko, kati ya meta 1300 na 2700 juu ya usawa wa bahari. Hukomaa katika kipindi cha miezi mitatu hadi mitano. Viazi mviringo vina asilimia kubwa ya chakula chenye asili ya wanga. Pia vina kiasi cha kutosha cha protini, madini, vitamini na maji.

Mbegu bora za viazi:  Zinatakiwa kuwa na sifa zifuatazo
·        Zenye kutoa mazao mengi zaidi kutoka kwenye shina moja
·        Ziwe zimechipua vizuri na ziwe na machipukizi mengi (zaidi ya manne)
·        Zisiwe na wadudu au magonjwa
·        Zitoke kwenye aina ambayo haishambuliwi na magonjwa kama vile ugonjwa wa ukungu na ugonjwa wa mnyauko bakteria
·        Zenye ukubwa wa wastani (yaani zisiwe ndogo au kubwa sana) unaolingana na ukubwa wa yai la kuku wa kienyeji

Aina bora za viazi

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo uyole, mpaka sasa imetoa aina sita za mbegu bora za viazi mviringo nazo ni : Baraka, Sasamua, Tana, Subira (EAI 2329), Bulongwa [(K59a (26)], Kikondo (CIP    720050)

Muda wa kupanda viazi: August hadi Septemba na Novemba hadi Decemba


Kupanda

Tumia sentimeta 60 (futi 2) hadi 75 (futi 2.5) kutoka mstari hadi mstari,  nafasi kati ya kiazi na kiazi iwe sentimeta 30

Mbolea

Ili kupata mazao mengi kutoka shambani mkulima anashauriwa kutumia mbolea, aina ya   samadi, mboji, majani mabichi na za viwandani (au za chumvi chumvi).

Kwa mbolea za viwandani tumia: Kilo 300 (au mifuko 6) ya mbolea ya TSP kwa hekta moja, na kilo 300 (mifuko 6) za mbolea ya CAN au kilo 400 (mifuko 8) ya SA au kilo 175 (mifuko 3.5) za Urea.

Palizi: Palilia viazi wiki mbili au tatu baada ya kuchomoza. Inulia udongo ili kufanya tuta zuri ili pawepo na unyevu wa kutosha na kufunika viazi kutokana na mwanga wa jua.

Magonjwa na wadudu waharibifu: Ili kuzuia ugonjwa wa ukungu tumia Ridomil. Changanya gramu 100 za dawa ya Ridomil katika lita 20 za maji, na nyunyizia mara baada ya viazi kuchomoza na baadaye kila baada ya wiki mbili au tatu kutegemea na hali ya hewa. Nyunyizia dawa kama Karate kiasi cha mililita 20 mpaka 40 za dawa katika lita 20 za maji ili kuzuia wadudu kama inzi weupe na wengineo. Tumia mbinu bora za kilimo kama usafi wa shamba au kilimo mzunguko kama mbinu shirikishi katika kuzuia magonjwa na wadudu. 

Kuvuna na mavuno: Viazi huwa tayari kuvunwa baada ya miezi 3 hadi 5 kutoka kupanda. Muda wa kuvuna utategemea madhumuni ya zao na aina iliyopandwa.  Usiache viazi shambani bila kuvifunika (kwa nyasi au udongo) kwa muda mrefu kwa sababu zifuatazo:
·        Viazi vikipigwa na jua hubadilika rangi na kuwa na rangi ya kijani ambayo inavifanya visifae kwa chakula.


·        Wadudu kama vile nondo hutaga mayai juu yake, yanapoanguliwa viwavi hutoboa na kuingia ndani ya viazi na kuviharibu
·        Iwapo vitanyeshewa na mvua vitaharibika wakati wa kuvihifadhi ghalani.

Aina bora kama Kikondo yaweza kutoa gunia 70 hadi 100 kwa ekari ikilimwa na kutunzwa vizuri.

Kuhifadhi: Viazi vya chakula vihifadhiwe kwenye ghala yenye hewa ya kutosha, pasiwe na unyevu, joto kali. Unapohifadhi viazi vya mbegu, aina mbalimbali zitengwe kwa kutumia vichanja au masanduku (maalum ya kuhifadhia)  tofauti.

Shukrani za dhati kwa mtaalamu wa Kilimo mifugo na mazingira&Mratibu wa program ya CHEMA jimbo katoliki la Rulenge-Ngara padre Anthony Ndikumulimo na Mtaalam Jonas B..Kizima kutoka Chuo Kikuu cha SOKOINE SUA .

No comments:

Post a Comment