November 10, 2014

Kikwete afanyiwa upasuaji Marekani

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Dk Edward Shaeffer alipowasili katika hospitali ya Johns Hopkins Marekani kwa ajili ya upasuaji. PICHA|IKULU
Dar es Salaam. Rais, Jakaya Kikwete amefanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostate) katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu kwa vyombo vya habari jana imesema Rais Kikwete amefanyiwa upasuaji huo juzi alfajiri baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa afya yake kujiridhisha kuwa alikuwa anahitaji matibabu ya aina hiyo.
“Upasuaji huo uliofanyika alfajiri na kuchukua kiasi cha saa moja unusu, umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa,” ilisema taarifa hiyo na kubainisha kuwa hali ya Rais Kikwete inaendelea vizuri na bado yuko wodini akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na kupatiwa tiba.
Taarifa hiyo iliyoambatana na picha mbili moja ikimwonyesha Rais Kikwete akiwa anazungumza na daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali hiyo, Dk Edward  na nyingine akiwa ameketi pamoja na daktari huyo pamoja na daktari wake, Profesa Mohamed Janabi ilisema wananchi wataendelea kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais kwa kadri zitakavyokuwa zinapatikana.
Wiki iliyopita, Kurugenzi hiyo ya mawasiliano Ikulu ilitoa taarifa za safari ya Rais Kikwete kwenda Marekani kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake na kuwa angekaa huko kwa siku 10.
    Source:Mwananchi

November 5, 2014

Timu ya Idhaa ya Kiswahili

Wengi wetu, mitaani,maofisini na Mitandaoni tumekuwa tukisikiliza matangazo ya Radio deutch welle na kupata shauku ya kuwafahamu watangazazji. Kutokana na Ombi Maalum ......nimepata hii

Kutoka Bonn, hiki ndiyo kikosi cha Idhaa yako ya Kiswahili kinachokuletea moja kwa moja taarifa za habari, ripoti, uchambuzi na makala motomoto zilizotafitiwa vyema, zilizopimwa na zisizoegemea upande wowote.

Kutoka kushoto: Mohammed Khelef, Mohamed Dahman, Oummilkheir Hamidou, Elizabeth Shoo, Nyamiti Kayora, Abdul Mtullya, Nina Markgraf, Grace Kabogo, Daniel Gakuba, Amina Abubakar, Mohamed Abdul-Rahman, Zuhura Hussein, Batoul Kidadi, Saumu Mwasimba, Iddi Ssessanga, Samia Othman, Sudi Mnette, na Andrea Schmidt.

TUJIKUMBUSHE:-Mpambano wa masumbwi kati ya Mohamed Ali na George Foreman

Magazeti ya Ujerumani wiki yameandika taarifa kuhusu ushindi wa Mohammed Ali dhidi ya George Foreman
Source:http://www.dw.de/mpambano-wa-ali-na-foreman-wakumbukwa/a-18031908
Wiki hii imetimia miaka 40 tangu mabondia mashuhuri Mohammed Ali na George Foreman walipopambana katika uwanja wa kitaifa mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Rumble in the jungle. Ni mpambano ulioingia katika vitabu vya historia na Mohammed Ali aliwashangaza wengi kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Foreman ambaye mpaka wakati huo alikuwa hajawahi kushindwa ulingoni. Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" linakumbusha namna ambavyo dunia nzima ilijaa na shauku kabla ya mpambano huo.
Mpambano huu ulikuwa mchanganyiko wa maonesho na propaganda. Dikteta Mobutu Sesse Seko alikuwa miongoni mwa wale waliowezesha tukio hilo kufanyika nchini mwake. Kwa namna hiyo alijipatia umaarufu dunia nzima. Lilikuwa moja ya matukio yaliyofuatiliwa na watu wengi zaidi katika televisheni. Hapa Ujerumani, ilibidi watu waamke saa tisa usikui ili wasipitwe.
Makala hiyo inaendelea kuelezea namna ambavyo ushindi wa Mohammed Ali uliwahimiza maelfu kuwa mabondia. Mmojawao ni Biko Botowamungu kutoka jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Alipata uraia wa Austria na mwaka 1988 kushiriki katika michezo ya olimpiki. Safari yake ya kuwa mwanandondi ilianza siku alipushuhudia mpambano kati ya Foreman na Ali kwa macho akiwa kijana wa miaka 17.

Utawala wa raia kurejea Burkina Faso?

Rais wa Ghana,Nigeria na Senegal wanatarajiwa kuwasili nchini Burkina Faso hii leo kwa ajili ya kutoa msukumo kwa Jeshi la nchi hiyo lirudishe utawala wa kiraia.
Kiongozi wa Burkina Faso Isaac Zida
Kiongozi wa mpito Luteni Kanali Isaac Zida amesema jeshi litaachia madaraka ndani ya majuma mawili,muda uliopangwa na Umoja wa Afrika.
Zida ameahidi kuanzisha serikali ya Umoja ili kuepuka vikwazo ambavyo vinaweza kutolewa dhidi yao.
Jeshi lilichukua madaraka baada ya kutokea machafuko na maandamano yaliyoshinikiza kujiuzulu kwa Rais Blaise Compaore.

November 4, 2014

WATEMBEA KWA MGUU BARABARANI,TEMBELEENI KULIA

Mkuu wa kitengo cha usalama Barabarani,Mkaguzi wa Magari na Mtahini wa MaderevaJehi la Polis wilaya ya Biharamulo Gilbert Rutayuga

washiriki wa mafunzo 1

washiriki wa mafunzo 2
WATEMBEA KWA MGUU BARABARANI,TEMBELEENI KULIA

Na, juventus Juvenary-BIHARAMULO

Jeshi la polis kitengo cha usalama Barabarani wilayani Biharamulo Mkoani Kagera kutembelea upoande wa kulia barabarani, pamoja na kuvuka barabara katika maeneo maalum yaliyotengwa ili kuepuka ajali

Rai hiyo imetolewa na Mkaguzi wa magari na mtahini wa madereva wa jeshi hilo Bw.Gilbert Rutayiga wakati akitoa mafunzo kwa wasaidizi wa kesheria  wilayani humo

Bw. Rutayuga amesema watenbea kwamguu wawapo upande wa kulia Barabarani ni rahisi kuona na kubaini mwendo wa gari au chombo chochote kinachopita barabarani

Aidha amewataka watembea kwa mguu wanapovuka kuhakikisha wanazingatia sheria kwakugeuka kushoto na kulia kuhakikisha usalama wao pamoja na kuepuka kuvuka barabara kwa haraka wala kutembea mwendo wa pole sana.       

na wakati huo huoWatembea kwamguu katika barabara,wametakiwa kuepuka matumizi ya vyombo vya muziki masikioni(Headphones) wanapokuwa barabarani ili kuepuka ajali na kuwa makini

Hayo yameelezwa na Mkuu wa kitengo cha Usalama Barabarani katika jeshi la Polis wilayani Biharamulo Bw.Gilbert Rutayuga wakati akitoa mafunzo kwa wasaidizi wa kisheria kutoka kata za Biharamulo

Amesema kama ilivyo marufuku kwa waendesha vyombo vya moto kutosikiliza muziki wakiwa safarini au kupiga na kupokea simu,vivyo hivyo tahadhari hiyo inatakiwa kuchukuliwa na watembea kwa mguu

Aidha,amesema ni sheria kwa watembea kwa mguu kuzingatia alama za ]barabarani,licha kuwa kuna udhaifu wa sheria kwakuwa hakuna mafunzo yanayotolewa kwa watembea kwamguu tofauti na madereva.    


October 30, 2014

RAIS WA ZAMBIA AFARIKI DUNIA


           
RAIS WA ZAMBIA AFARIKI DUNIA
Serikali ya Zambia imesema Rais wa nchi hiyo Michael Sata amefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu kwa maradhi ambayo hayakutajwa.

Rais Sata, 77, alifariki katika hospitali ya King Edward VII jijini London, Uingereza Jumanne usiku.
Vyombo vya habari vimesema alifariki baada ya "mapigo ya moyo kwenda kasi ghafla".
Haijafahamika mara moja nani atachukua nafasi yake ya urais. Suala hilo huenda likajadiliwa na baraza la mawaziri la Zambia litakalokutana Jumatano asubuhi.

"Kwa moyo mzito natangaza kifo cha rais wetu mpendwa," imesema taarifa ya waziri Roland Msiska iliyosomwa kwenye TV ya taifa."Nawaomba muwe watulivu, muungane kwa amani katika kipindi hiki kigumu," ameongeza kusema Bwana Msiska.


Mapema mwezi huu taarifa nchini Zambia zilisema Rais Sata alikuwa amekwenda nje ya nchi kwa matibabu, huku kukiwa na tetesi kuwa alikuwa taabani.


Baada ya kuondoka nchini humo, waziri wa ulinzi Edgar Lungu alitajwa kukaimu urais.
Makamu wa rais Guy Scott mara nyingi hukaimu urais. 


Hata hivyo ana asili ya Scotland na wazazi wake hawakuzaliwa Zambia, hivyo hatoweza kuchukua urais kutokana na vipengele ndani ya katiba.

Akijulikana kama "King Cobra" kutokana na matamshi yake makali, Bwana Sata alichaguliwa kuwa rais wa Zambia mwaka 2011.
          SourcE: BBC

October 28, 2014

Kiwanda cha matrekta kujengwa Tanzania

Kiwanda cha matrekta kujengwa Tanzania
Source:www.mwananchi.co.tz
 Warsal, Poland. Kampuni ya Ursus ya Poland imesema ina mkakati wa kujenga kiwanda cha kutengeneza matrekta Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya Suma JKT.
Rais wa Bodi ya Ursus, Karol Zarajczyk alisema hayo jijini Warsaw jana wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokutana na wafanyabiashara wenye nia ya kuwekeza Tanzania.
Zarajczyk alisema wanataka kujenga kiwanda hicho kwa kuwa wametambua Tanzania ina fursa ya kufungua milango ya kibiashara kwa nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati.
Alisema lengo jingine la kampuni hiyo inayotengeneza matrekta ni kutoa mafunzo kwa wakulima ya jinsi ya kutunza matrekta hayo, ili waone umuhimu wake katika sekta ya kilimo.
“Barani Afrika tulianza kupeleka matrekta Ethiopia, Ghana na Guinea. Sasa hivi tumeamua kwenda Tanzania na Zambia.
“Nia yetu siyo kujenga tu kiwanda, bali pia kutoa huduma kwa wakulima juu ya uendeshaji na utunzaji wa matrekta hayo,” alisema.
Alisema wako tayari kutoa mafunzo kwa vijana wa Tanzania waliopo vyuoni ili waweze kuunganisha matrekta hayo, kuyafanyia ukarabati na kutengeneza vipuri vyake wakati kunapokuwa na ulazima wa kufanya hivyo.
“Tunapenda kujenga kiwanda mahali ambapo itakuwa rahisi kupata vijana wa kuajiriwa ili iwe rahisi kuwafundisha teknolojia tunayoitumia kutengeneza matrekta,” alisema.
Kwa upande wake, Pinda alisema atawasilisha maelezo hayo kwa waziri anayehusika na sekta hiyo ili mawasiliano rasmi ya kujenga kiwanda hicho yafanyike.

October 17, 2014

Bil 18/- kutumika kwa chanjoBIHARMULO
Idara ya fya wilayani Biharamulop Mkoani Kagera inatarajia kutoa chanjo ya Surua na Lubera kwa wakazi wa wilaya hiyo wanaokadiriwa kuwa laki 1 na elfu 90 sawa na nusu ya wananchi wilayani humo ambao wanakadiriwa kufikia laki 3 na elfu 20

Hayo yameelezwa na mganga mkuu wa wilaya hiyo Dk. Tumpale Akim wakati akizungumza na Radio Kwizera kuhusu chanjo hiyo inayotarajiwa kuanza kesho

Dk. Tumpale ameeleza kuwa walengwa ni watoto kuanzia miezi 6 hadi miaka 14,ambapo Chanjo hiyo itawaepusha na ulemavu vifo na matatizo ya mimba kwa akina mama

Ameyaainisha maeneo itakapotolewa chanjo hiyo kuwa ni pamoja na zahanati,vituo vya afya,Hospitali,shuleni na baadhi ya makanisa yaliyoainishwa na kuridhiwa na baadhi ya viongozi wake

Aidha,mganga mkuu huyo amewataka wananchi kujitokeza kuwapeleka watoto wao katika chanjo kwaajili ya kuepuka madhara yatokanayo na ukosefu wa chanjo hiyo.  

...........................................................................................................................................
  Serikali inatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 18 kwa ajili ya chanjo ya surua na ribela inayotarajiwa kutolewa Oktoba 18 mwaka huu nchini kote.
Hayo yalisemwa na Ofisa mafunzo na mawasiliano wa idara ya kinga na chanjo wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Ibrahim Maduhu wakati wa mkutano wa kamati ya huduma ya afya ya msingi wa jiji la Tanga.
Alisema kuwa uwekezaji huo ni mkubwa kufanywa na serikali kwa wananchi wake kwa lengo la kuwapatia afya bora.
Dk Maduhu alisema, kuwa ni jukumu la kamati za afya nchini nzima
kuhakikisha wanaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo.
“Ni vema mkahakikisha watu wanajitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo kwani limelenga kwa watoto kuanzia umri wa miezi tisa hadi miaka 15,” alisema
Naye mganga mkuu wa jiji hilo, Dk Asha Mahita alisema, kuwa asilimia 15 ya watoto waliopatiwa chanjo ya surua katika jiji hilo hawajajenga kinga kamili.
Alisema kuwa kampeni hiyo itawahusisha hata watoto waliopatiwa chanjo ya surua awali.
Alisema jiji hilo litakuwa na vituo 600 kwa ajili ya kutoa chanjo hiyo kwa wananchi wote

October 1, 2014

Mabondia Mayweather na Pacquaio wawindana

Source:DW ......Mpiganaji ngumi nyota kutoka Ufilipino Manny Pacquiao amepuuzia majigambo ya Floyd mayweather , akisema anamuonea huruma hasimu wake huyo Mmarekani na anamtaka kusoma biblia.

Mpiganaji ngumi nyota kutoka Ufilipino Manny Pacquiao amepuuzia majigambo ya Floyd mayweather , akisema anamuonea huruma hasimu wake huyo Mmarekani na anamtaka kusoma biblia.
Pacquiao amewahakikishia mashabiki wake pia kwamba atacheza kwa dakika chache mchezo wa mpira wa kikapu wakati msimu mpya utakapoanza mwezi ujao hata kama anajifua kwa ajili ya mchezo mjini Macau mwezi Novemba dhidi ya Mmarekani ambaye hajawahi kushindwa Chris Algieri.
Katika vituko vya hivi karibuni, Mayweather , ambaye hajawahi kushindwa katika mapambano yake 47, ameweka picha kadhaa katika mtandao wa kijamii , akimuonesha Pacquiao akiwa ameangushwa chini katika mapambano yaliyopita. Ameongeza kuwa Pac Man amechacha hana kitu mfukoni anasubiri malipo.

 

 

Waliopiga kura ya hapana walalamika kutishwa


Source:Mwananchi

Dodoma/Dar. Baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba waliopiga kura za hapana wamelazimika kuondoka Dodoma na kurudi Zanzibar kwa madai ya vitisho walivyopata kutoka kwa wenzao.
Mmoja wa wajumbe hao, Salma Said alisema jana jioni kuwa yeye na wajumbe wenzake wamekataa kuitikia wito wa Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta kwenye Kamati ya Mashauriano ili kuhojiwa kuhusu kura hiyo na kutokana na vitisho wanavyopata kutoka kwa wajumbe wenzao wameamua kuondoka Dodoma.
Vitisho hivyo vimeripotiwa muda mfupi baada ya Sitta kuunda Kamati ya Mashauriano ya watu tisa inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan kushughulikia kura hizo zilizopigwa na wajumbe saba zinazoweka njiapanda uwezekano wa kupatikana akidi ya kupitisha Katiba inayopendekezwa.
Wajumbe waliopiga kura za wazi za hapana kwa ibara zote ni Adil Mohamed Adil, Dk Alley Soud Nassor, Fatma Mohamed Hassan, Jamila Ameir Saleh, Salma Hamoud Said, Mwanaidi Othman Twahir na Ali Omary Juma.
Kwa upande wa Tanzania Bara aliyepiga kura ya hapana kwa rasimu nzima ni Mbunge wa Mpanda Kati (Chadema), Said Arfi na wajumbe 30 kutoka Zanzibar wakipiga kura ya siri.
“Baada ya kupiga kura za hapana leo (jana), walijitokeza wajumbe akiwamo (jina tunalihifadhi kwa sasa) wakaanza kutuzongazonga,” alisema Salma.
“Walituambia kuwa tumebaki hadi dakika ya mwisho halafu tunasema hapana kwa rasimu nzima ili kula fedha za bure, wanasema bora tungeondoka na Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi).”
Hata hivyo, alipopigiwa simu yake ya mkononi mmoja wa watuhimiwa, alipokea na baada ya mwandishi kujitambulisha alikata simu na alipopigiwa mara ya pili alijibu alisema; “Mimi ni mheshimiwa mwana na niko Sudan.”
Salma alisema miongoni mwa wajumbe hao wakiwamo baadhi ya mawaziri waliwafuata hadi nje ya ukumbi wakiwatishia kuwa watawafanyia hujuma kwa kukataa kuunga mkono rasimu hiyo.
“Sisi tumeamua kuondoka kurudi kwetu, hatutaingia tena bungeni maana hivi vitisho vimezidi sasa,” alisema Salma.
Juhudi za kuwapata wajumbe wenzake kuzungumzia vitisho hivyo hazikuzaa matunda, lakini Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad alikiri kupokea malalamiko hayo na kwamba amelichukulia kama suala la kisiasa.
Alisema wajumbe hao hawajasema wametishiwa kufanyiwa kitu gani, bali walimweleza kuwa wameambiwa kuwa wamekaa pale (bungeni) kwa ajili ya kupata pesa.

September 11, 2014

Tume ya kuchunguza Tokomeza Ujangili kuanzia mkoani Kigoma

Fredrick Manyanda
SOURCE:NIPASHE
Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Ujangili imetangaza ratiba ya kwanza ya ziara yake katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na Mbeya inayoanza Septemba 17, hadi Oktoba 6, mwaka huu.

Ziara hiyo inayolenga kukusanya taarifa na kupokea malalamiko yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili inaanza katika mkoa wa Kigoma ambako itakuwapo huko kwa muda wa siku nane (Kigoma Septemba 17, Kibondo Septemba 18, na  Septemba 19, Kasulu Septemba 20 na 22 na Uvinza Septemba 23 na 24).

Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume hiyo iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Tume Fredrick Manyanda, tume itakuwa katika mikoa ya Rukwa na Katavi kuanzia Septemba 25 hadi 30.

Alisema, Septemba 25 hadi 27, tume itakuwa Mpanda na Septemba 28 hadi 30, itakuwa mjini Sumbawanga.

Aidha Tume itakuwa katika mkoa wa Mbeya ambapo itatembelea katika wilaya za Mbozi, Mbeya na  Mbarali kuanzia Oktoba Mosi hadi 6.

Itakuwa katika wilaya ya Mbozi Oktoba Mosi na 2, Mbeya mjini Oktoba 3, na itamalizia ziara yake katika wilaya ya Mbarali Oktoba 5 na 6.

Aidha pamoja na ziara hiyo, Manyanda amesema tume inaendelea kupokea taarifa na malalamiko kwa njia ya barua, simu na barua pepe

September 9, 2014

Uamuzi mgumu,Rais hataongeza muda Bunge la KatibaUamuzi mgumu,Rais hataongeza muda Bunge la Katiba


Source:Mwananchi

Dodoma. Makubaliano baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kutaka Bunge Maalumu lifikie ukomo Oktoba 4, mwaka huu yamezua sintofahamu mjini hapa huku uamuzi huo ukionekana kuwachanganya viongozi wa Bunge hilo.
Kutwa nzima ya jana, viongozi wa Bunge Maalumu walishinda kwenye vikao vya mashauriano huku wabunge wa CCM wakitarajiwa kukutana jana usiku kwenye makao makuu ya chama hicho kupewa taarifa rasmi za uamuzi huo.
Katika makubaliano baina ya TCD na Rais Kikwete, imeamuliwa kuwa uamuzi wa Rais kupitia Tangazo la Serikali (GN) 254 la kuongeza siku 60 hadi Oktoba 4 uheshimiwe na baada ya tarehe hiyo Bunge liahirishwe.
Uamuzi huo ni kinyume cha azimio la Bunge Maalumu la Agosti 5, 2014 ambalo lilirekebisha Kanuni ya 14 (4) na kuifuta Jumamosi katika siku zilizotajwa kuwa za kazi, pia sikukuu na siku za Jumapili.
Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alikaririwa akiwaambia wajumbe wa Bunge hilo kwamba Rais alikuwa ameridhia kwamba siku 60 alizotoa hazingejumuisha Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu.
Ni kwa msingi huo, Bunge hilo likapanga kwamba lingeendelea na shughuli zake hadi Oktoba 31, wakati Mwenyekiti wa Bunge atakapokabidhi Katiba inayopendekezwa kwa Rais Kikwete.
Hata hivyo, makubaliano yaliyofikiwa baina ya viongozi wa TCD na Rais yanaonekana kuvuruga kabisa ratiba ya Bunge hilo ambalo jana na juzi, Kamati ya Uongozi ilikutana mara kadhaa kuona jinsi ya kunusuru mchakato huo.
Ingawa haikufahamika mara moja kama vikao hivyo vya kamati ya uongozi inayoongozwa na Sitta mwenyewe vinajadili nini, lakini taarifa zimedai huenda kukawa na mabadiliko makubwa ya ratiba.
Habari nyingine zinadai kwamba mabadiliko hayo huenda yakapunguza muda wa baadhi ya shughuli za kazi za Bunge hilo ili liweze kukamilisha kazi yake ikiwamo wajumbe kupiga kura ya uamuzi.
Katika kikao cha jana asubuhi, kamati hiyo ilishindwa kurekebisha ratiba yake ili iendane na siku zilizosalia, hivyo kuahirishwa kwa kuwapa kazi wataalamu wake kuleta mapendekezo ambayo yangejadiliwa jana mchana.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alithibitisha jana kwamba ratiba ya Bunge imebadilika kutokana na hoja nyingi kukubalika ndani ya kamati.
“Kamati ya uongozi itakutana baadaye (jana) kuangalia vipengele ambavyo hawakukubaliana kwenye kamati ndivyo wavipangie muda na ratiba itajulikana baada ya kikao hicho,” alisema Hamad