October 2, 2013

KAULI YA CHADEMA KUHUSU KUFUNGIWA KWA MAGAZETI








CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO Idara ya Habari ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), tangu ilivyopokea kwa masikitiko na mshituko mkubwa taarifa za Serikali ya CCM, kufungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, imeendelea kufuatilia kwa ukaribu hatua zinazochukuliwa na kauli mbalimbali zinazotolewa na pande zote mbili, serikali na wadau wa uhuru wa habari na vyombo vya habari.

Ni wazi bila shaka yoyote kuwa kwa mara nyingine tena, serikali hii, imeendelea kutumia sheria mbaya, kutumia madaraka vibaya kufanya uamuzi mbaya, kila inapokosa hoja na uwezo wa kukabiliana na sauti mbadala au maoni kinzani.
Suala hili limekuwa dhahiri zaidi baada ya Serikali kuamua hata kuanza kuingilia uhuru wa habari na maoni kwenye mitandao ya kompyuta (on line) na pia kutishia kulifungia Gazeti la Rai, linalotolewa na Kampuni ya New Habari (2006) Limited, kwa sababu limeanza kuchapiswa kila siku.
Wakati wamiliki wa gazeti hilo wametoa ushahidi unaotokana na nyaraka za serikali hiyo hiyo iliyotoa idhini kwa chombo hicho kuchapishwa kila siku, Serikali yenyewe kwa upande wake imetoa utetezi wa ajabu juu ya tishio lake hilo ikijitetea kuwa kibali hicho kilitolewa kwa Kampuni ya Habari Corporation iliyouza hisa zake kwa Kampuni ya New Habari (2006) Limited.
Katika hili serikali inajichanganya. Hii ni dalili ya wazi kwamba uamuzi wake huo ni mwendelezo wa maamuzi ya kibabe, yasiyofanywa kwa masilahi ya Watanzania, ndiyo maana yanaanza kuipatia tabu jinsi ya kujibu na kujenga hoja za kutetea uovu wake.
CHADEMA, inapinga na itaendelea kupinga kwa kauli na vitendo, hatua hii ya serikali yenye lengo ovu dhidi ya umma wa Watanzania.

Ni suala linalohitaji tafakuri yetu sote, kwa nini serikali imeamua kuchukua hatua hii wakati huu ambapo nchi nzima iko kwenye mjadala wa Katiba Mpya ambayo ni fursa adhimu ya taifa kujiumba upya na kuachana na sheria mbovu kama hiyo ya mwaka 1976 inayompatia mamlaka waziri husika kufungia gazeti kadri anavyoona 'yeye' inafaa.

Hoja si maudhui
Kama kawaida yake, serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Asa Mwambene, imeamua kuja na hoja ya 'maudhui' kuwa ndiyo uwe msingi mkubwa wa kuhalalisha kitendo hicho kibaya cha kufungia magazeti kwa kutumia Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.
Tunasema hapa hoja haiwezi kuwa maudhui yaliyosababisha magazeti hayo kufungiwa kama ambavyo serikali ya CCM siku zote imejaribu kuonesha kila inaposhughulikia vyombo vya habari, suala la msingi ni utaratibu unaotumiwa kuvifungia.
Serikali haiwezi kuwa hakimu wa kesi yake yenyewe. Halikadhalika haiwezi kufanya kazi zote; kulalamika, kutuhumu, u-polisi (kupeleleza), kuendesha mashtaka na kisha kuhukumu. Hii ni kinyume kabisa cha misingi ya haki ya asili. Ni ukiukwaji mkubwa wa haki.
Kama serikali ilifikiri vyombo hivyo vya habari vimekosea au vimesema uongo, ilipaswa kusema ukweli ni upi, la sivyo ilipaswa kufungua mashtaka kwa vyombo huru vinavyoweza kushughulikia masuala hayo; ama ingepeleka malalamiko yake Baraza la Habari Tanzania (MCT), kama haina imani nalo (kinyume na imani waliyonayo Watanzania wengi juu ya baraza hilo) basi ingeenda kushtaki mahakamani.
Kinyume cha hapo ni kuendeleza uharamia dhidi ya uhuru wa habari, vyombo vya habari na utoaji wa maoni.
Kitendo cha kutisha na kufungia vyombo vya habari kimekuwa ni moja ya mbinu ya serikali hii kupambana na sauti mbadala, uhuru wa habari na maoni. Safari hii, kimekuja wakati nchi na umma wote wa Watanzania, kupitia taasisi, asasi na makundi mbalimbali ya kijamii, ukiwa umeungana kuhoji dhamira ya watawala kutaka kuharibu na kukwamisha mchakato wa Katiba Mpya.
Hivyo hapa kuna masuala kadhaa;
• Vyanzo vyetu vya taarifa vimedokeza kwamba zipo njama za baadhi ya watendaji wa serikali kufanya vitendo vya kutaka kuzuia sauti mbadala zinazojaribu kupiga kelele kuuhabarisha umma juu ya uchakachuaji unaofanyika kwenye mchakato wa katiba mpya.
• Hatua ya kufungia vyombo vya habari sasa hivi ni jaribio la kuleta Kutia hofu vyombo vya habari visiripoti kwa uhuru mchakato wa Katiba Mpya, hasa habari zenye mwelekeo wa kusema ukweli dhidi ya serikali au watawala wanaotaka kukwamisha na kuharibu mchakato wa katiba mpya.
• Kutaka kuhamisha mjadala (diversion of discussion) mkali wa katiba mpya unaoendelea kwa sasa, ili wananchi na taifa zima lianze kujadili suala jingine, badala ya kuibana serikali, kisha watawala wapate ahueni ya kupita katikati kutekeleza dhamira yao kwenye mchakato huo nyeti.
• Pia kitendo hiki kinakwenda sambamba kabisa na msimamo wa CCM kwenye Rasimu ya Katiba Mpya, ambapo chama hicho, kimekuwa kikipinga masuala mengi ya msingi na muhimu kwa wananchi, likiwemo suala la haki za binadamu lisiwe jambo la muungano na uwazi usiwe miongoni mwa tunu za taifa kwenye katiba mpya.
Serikali ilipaswa kuonesha au kuiga mfano katika uwajibikaji. Mathalani, itakumbukwa kuwa Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya CHADEMA, ndiyo taasisi pekee ya kisiasa nchini iliyosaini Azimio la Dar es Salaam Juu ya Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji, lililopitishwa na Baraza la Habari la Tanzania (MCT). Pamoja na ubora na upekee wa azimio hilo, barani Afrika na dunia nzima kwa ujumla, si serikali wala viongozi wake ambao wameonesha kuunga mkono, ili kuepuka vitendo kama hivi vya kidhalimu.
Idara ya Habari ya CHADEMA inapenda kutoa wito kwamba;
 Makundi na wadau mbalimbali walioathirika na kufungiwa kwa magazeti haya wajitokeze wazi, wapaze sauti zao kuungana na makundi mengine ya kijamii, asasi za kiraia na kitaaluma zinazopinga vitendo hivi. Hasa yale ambayo habari zilizoandikwa na Magazeti hayo ya Mwananchi na Mtanzania, zilikuwa zikiyahusu, mathalani;
• Vyama vya wafanyakazi (Habari ya Mwananchi).
• Madhehebu ya dini (Habari picha ya Mwananchi).
• Wale wote walioathirika na vitendo ambavyo vyombo vya dola vinatuhumiwa kuvifanya au kuzembea kuchukua hatua kubaini ukweli (habari ya Gazeti la Mtanzania).
Mjadala huu wa kuitaka serikali kuacha kutumia sheria mbovu na kandamizi na kuyafungulia magazeti haya mawili, utiwe uzito na uende sambamba na ule wa kulifungulia Gazeti la Mwanahalisi ambalo serikali hii iliyoamua kugeuka kuwa tishio kwa uhuru wa habari na vyombo vya habari, iliamua kulifungia kwa muda usiojulikana.
 Makundi mbalimbali ya kijamii ambayo yameungana kwa dhati kwenye mchakato wa Katiba Mpya hasa kupinga dhamira ya serikali na CCM, kutaka kuuharibu na kuukwamisha, kuzidi kuunganisha nguvu zao, kwani mchakato bora utatupatia katiba mpya bora, ambayo itaondoa sheria mbovu kama hii ya magazeti ambayo serikali imeendelea kuitumia kukandamiza umma wa Watanzania.
Tutalaani na kuchukua hatua
Watawala baada ya kufungia vyombo vya habari kadhaa na jamii kukaa kimya, mfano Gazeti la Kulikoni, Redio Imani, Redio Kwa Neema Fm, vingine kwa muda usiojulikana mf; Gazeti la Mwanahalisi, sasa wamefikia mahali wanafikiri wanaweza kuendelea na jamii ikakaa kimya.
Tutachukua hatua. Tutapinga kwa kauli na vitendo. Wakati tukilaani na kutoa wito kwa makundi mengine ya wadau wote wa masuala ya habari kushikamana kwa dhati kupinga jambo hili kwa namna wanazoona zinafaa, CHADEMA kwa upande wake, kwa kuanzia, kinaunga mkono wabunge wake (Zitto Kabwe na John Mnyika) ambao wameonesha nia ya kuchukua njia za kibunge, ili kufuta sheria yote ya magazeti ya mwaka 1976 au baadhi ya vifungu vyake vinavyotoa mamlaka mabovu yanayotumiwa vibaya na watawala kwa ajili ya malengo mabaya.
Hivyo, katika kufanikisha hatua hiyo, tunatoa wito kwa watu wote walioguswa na kitendo hiki cha ukandamizaji, wakiwemo wabunge waunge mkono njia itakayochukuliwa na wabunge wa CHADEMA.
Imetolewa , Oktoba 2, 2013, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene, Ofisa Mwandamizi wa Habari
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)

No comments:

Post a Comment