April 14, 2015

Maiti ajali ya basi wazikwa kaburi moja-MOROGORO



SOURCE:Mtanzania
MIILI ya abiria 15 walioteketea kwa moto katika ajali ya basi iliyotokea juzi katika eneo la Ruaha, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, imezikwa katika kaburi moja.
Ilizikwa jana asubuhi katika makaburi ya Msavu Ruaha wilayani humo.
Abiria hao walifariki dunia baada ya basi la Kampuni ya Nganga walilokuwa wakisafiria lenye namba za usajili T 373 DAH kugongana na lori aina ya Fuso lenye namba za usajili T 164 BKG.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, John Henjewele, alisema miili minne imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kati ya 19 ya waliopoteza maisha.
“Pamoja na miili minne kutambuliwa, iliyobaki tumeamua kuizika kwenye kaburi moja katika eneo la Ruaha baada ya kutotambuliwa na ndugu zao kwani wengine walitokea Wilaya za Kilosa na Kilombero.
“Ruaha ni sehemu ya katikati ya Wilaya ya Kilombero na Wilaya ya Kilosa, kwa hiyo tumeona ni sehemu mwafaka kwa watu wa pande zote mbili kuweza kufika eneo hilo kwa ajili ya maombolezo,” alisema Henjewele.
Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paul, aliwataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Hadija Legembo (35), mkazi wa Mnyamvisi, Lydia Ndongwe (16) mkazi wa Kilombero ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mtakatifu Francis ya Mbeya na Ester Mgimba (30), mkazi wa Njombe.
Wengine ni Nelson Patrick (2), mkazi wa Njombe, Marietha Mbimbi (19), mkazi wa Kilombero na Mengo Njagaje (30), mkazi wa Mbeya.
Aliwataja majeruhi ni Majaliwa Elisha (21) ambaye ni mwananfunzi wa Shule ya St Mary Mbeya, Linda Jonathan (26), mkazi wa Mbeya, Rose Seth, mkazi wa Kilombero, Elias Augustino (36), mkazi wa Kilombero, Batista Emmanuel, mkazi wa Mbeya na Abubakari Athumani (36), mkazi wa Ruaha, Kilombero.
Wengine ni Emmanuel Omarino (18), mkazi wa Kilombero, Theresia Kusila (25), mkazi wa Ruaha, Kilombero, Shafii Musa (25), mkazi wa Kilombero na Anyindwile Elia (30) ambaye ni kondakta wa basi hilo, mkazi wa Majengo, Mbeya.
Akizungumzia mazingira ya ajali hiyo, Kamanda Paul alisema ilisababishwa na uzembe wa dereva wa basi kwani alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, abiria walisema baada ya dereva huyo kushindwa kulimudu basi hilo, alihama upande wake na kulifuata lori ambapo magari hayo yaligongana.
Wakati huo huo, Hadia Khamis na Mwantumu Saadi, wanaripoti kuwa
majeruhi 10 walionusurika katika ajali ya mabasi mawili ya Ratco na Ngorika yaliyogongana maeneo ya Mkata mwishoni mwa wiki iliyopita, wamehamishiwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi) jijini Dar es Salaam.
Meneja Uhusiano na Ustawi wa Moi, Almas Jumaa, alisema majeruhi hao wamefikishwa juzi wakitokea katika hospitali za Mkoa wa Pwani.
Alisema majehuri hao wameumia viungo mbalimbali vya mwili, ikiwamo kichwa, mikono, miguu pamoja na michubuko.
Jumaa aliwataja majeruhi hao kuwa ni Hamis Rajab (31), Robert Mavase (46), John Olutu (76), Mwanamtama Mafuta (32), Eli Swai (31) na Bilhuda Mkwaro (51).
Wengine ni Aisha ambaye hakujulikana miaka yake kutokana na umri wake kuwa mkubwa sana, Said Salim (41), Mohammed Mkindi (24) na Said Mrutu (48).
Alisema hali ya majeruhi zinaendelea vizuri na timu ya madaktari bingwa wa mifupa wanajitahidi kuhakikisha wanarudi katika hali ya kawaida.

No comments:

Post a Comment