October 23, 2012

Baadhi ya viongozi wa Kijiji Kasulo wilayani Ngara watishia Kujiuzuru



Baadhi ya viongozi wa Kijiji Kasulo wilayani Ngara watishia Kujiuzuru
Na:Shaaban Ndyamukama  Ngara
Baadhi  ya Viongozi wa serikali ya kijiji cha Kasulo wilaya ya Ngara mkoani Kagera wametishia kujiondoa katika serikali yakijiji hicho kwa kupinga kufanya kazi kwa shinikizo la mamlaka iliyo juu yao bali watatumia sheria kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu  ya wananchi waliowachagua
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kasulo wilayani Ngara  Yusufu Katula alisema hayo hivi karibuni wilayani Ngara katika kikao cha serikali yake kilichoitishwa kwa ajili ya kuweka mipaka kati ya kijiji na mwananchi mmoja kutoka wilayani Geita aliyeomba ardhi kwa ajili ya makazi na eneo la kufugia mifugo yake kwenye  kijiji hicho.  Katula alisema viongozi wa kijiji hicho wamekuwa wakipokea amri kutoka kwa viongozi wa wilaya ya Ngara na  halmashauri yake kupata ardhi kwa ajili ya kuwagawia  watu wao bila kupata Baraka kupitia mkutano wa wananchi wote. Alisema kwa sasa kijiji hicho hakina ardhi ya kugawa na aliyepata eneo la makazi Bw Makoye Athumani alituma maombi na kukubaliwa na wananchi baada ya kuonesha ushirikiano na jamii kwa kuchangia miradi ya  kuleta maendeleo
Awali Afisa mtendaji wa kijiji hicho  Christopher Nzoya aliwasomea barua wajumbe wa serikali ya kijiji iliyotoka kwa mkuu wa wilaya ya Ngara kuwa kijiji cha kasulo  kitoe ardhi ekari 50 kwa kampuni ya Mingo East Africa kwa ajili ya kuwekeza shughuli za kijamii. Barua hiyo ilifafanua kuwa kampuni hiyo inahitaji ekari  1000 kwa ajili ya kuwekeza shughuli za maendeleo wilayani Ngara na kwamba serikali ya kijiji cha kasulo  ifanye utaratibu wa kuiwezesha kupata eneo litakalotumika kuanzishwa miradi mbalimbali itakayowanufaisha wananchi hasa vijana kupata ajira kupitia kampuni hiyo.
 Naye  Afisa Mazingira wilayani Ngara Toba Mhina akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo alisema viongozi wa vijiji wazingatie sheria za kugawa ardhi bila kushawishiwa kwa zawadi ndogondogo kupitia mianya ya rushwa .Mhina alidai kuwa kuna viongozi wasio waaminifu wanaowazunguka wenzao katika utoaji wa maamuzi hali inayowafanya wananchi kutuma ujumbe ngazi ya wilaya ili kufuatilia kuwepo rushwa katika kutoa ardhi kwa waombaji. Mingo East Africa co. LTD  iliomba ekari 1000 katika kijiji cha kasulo wilayani Ngara lakini serikali ya kijiji hicho pamoja na  wananchi walidai ekari hizo haziwezi kupatikana na wala kijijiji hakina mamlaka ya kutoa ardhi zaidi ya ekari 50 kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999. Kufuatia hali hiyo  kampuni ya Mingo ililazimika kupeleka maombi yake ngazi ya wilaya ambapo ushauri ulitolewa kupewa ekari hamsini badala ya 1000 kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kiuchumi jambo ambalo limepingwa vikali na viongozi pamoja nawakazi wa kasulo
Katika hatua nyingine katika kikao hicho baadhi ya wajumbe walihitilafiana katika kutoa maoni ya kuweka mipaka ya kijiji na eneo la aliyeomba makazi na sehemu ya kulishia mifugo yake Bw Makoye Athumani baada ya kushawishi viongozi kwa  kujenga madarasa mawili  kwa shilingi milioni 19 .Samweli Kapalala Mwenyekiti wa wafugaji na Braiton Mmoja wa wenyeviti wa vitongoji walisema wanaopewa ardhi wanamaslahi na baadhi ya vigogo wilayani Ngara na kwamba wanatumia nafasi hiyo kuwanyanyasa wananchi wasio na uwezo kiuchumi hasa ambao si wafugaji wenye ng’ombe wengi. Maoni ya baadhi ya wajumbe wa serikali ya kijiji hicho yalimfanya Mwenyekiti wa Serikali hiyo Yusufu Katula kutishia kujiuzuru wadhifa wake baada ya kumtuhumu kujihusisha na vitendo vya Rushwa katika utawala wake na kuwanyima  wananchi haki zao za utawala bora. Alisema "Nafanya kazi na viongozi ambao baadhi yenu mnaendekeza  majungu na kukashifiana nje ya vikao rasmi hali ambayo kwa namna moja au nyingine inaweza kusababisha uvunjifu wa amani katika kijiji hiki na wananchi kukosa imani na serikali yao katika kusimamia  maendeleo yao"
Makoye Athumani (Msukuma)kutoka wilayani Geita aliye na Ng’ombe zaidi ya 700 aliomba ardhi kuwekeza ufugaji katika kijiji cha kasulo na kujenga vyumba viwili vya madarasa baada ya kuelezwa kuwa kijiji hicho kinao wanafunzi 400 walioko eneo la Ngoma wanaotembea umbali wa kilomita 27 kila siku kutafuta elimu katika shule ya msingi Njia panda iliyoko kijijini humo.
Kikao hicho  kilichohudhuriwa na viongozi waandamizi wa halmashauri ya wilaya ya Ngara ikiwemo Taasisi ya TAKUKURU mbapo mwanasheria wa halmashauri ya wilaya y angara  Kamilius Ruhinda alisema  mwenyekiti huyo hana budi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria za utawala bora na unaozingatia demokrasia wa walio wengi
Ruhinda alisema endapo kanuni na taratibu  za kugawa ardhi zitafuatwa wananchi wakahusishwa na nakala za mihtasari za maazimio au makubaliano yakawekewa Baraka na halmashauri ya wilaya hakutaweza kujitokeza kwa migogoro baina ya viongozi wa ngazi mbalimbali na wananchi. “Ni jambo la muhimu kila kiongozi ni lazima kufanya kazi kwa kuzingatia maamuzi ya waliowengi katika utawala bora kuliko kutumia ubabe katika nafasi yako  na hatimaye kuvunja sheria hili halina budi kufuatiliwa kwa ukaribu na kwa umakini”. Alisema Ruhinda
Alidai kuwa kufuatia kuhitilafiana katika utoaji wa maamuzi katika kuhimiza na kuleta maendeleo ya kijiji kuna haja ya  Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU kufanya uchunguzi dhidi ya viongozi wanaotanguliza maslahi yao kabla ya wananchi na kukiuka viapo vya kuitumikia jamii.
Hata hivyo  mkuu w wilaya ya Ngara Costantine Kanyasu alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi alisema serikali kazi yake ni kutoa maagizo katika mamlaka zake kutekeleza baadhi ya matakwa ya wananchi hivyo aliagiza kamati za ardhi kufanya upembuzi yakinifu kubaini maeneo ya kuweza kuwapatia wawekezaji  wazalendo wanaohitaji kufuga kwa njia za kisasa kwa kuhifadhi na kutunza mazingira. Kanyasu alisema serikali haiwezi kufanya kazi kwa shinikizo la wachache walio na wivu fitina na majungu na viongozi wa vijiji wilayani humo wafanye kazi kwa kutii taratibu na  kuzingatia mamlaka inayowaelekeza kwa ushauri kutekeleza baadhi ya majukumu yaliyo na maslahi kwa taifa

No comments:

Post a Comment