October 15, 2012

Mwanafunzi aliyejifungua aondolewa chumba cha Mtihani

Mwanafunzi aliyejifungua wakati wa Mitihani ya Kidato cha nne



Na Shaaba Ndyamukama Ngara

Mwanafunzi wa kike anayesoma kidato cha nne katika shule ya sekondari Kibogora wilaya ya Ngara mkoani Kagera amesimamishwa kuendelea na mtihani wa kuhitimu elimu ya sekondari baada ya kubainika kujifungua siku chache zilizopita

Mkuu wa shule ya Sekondari kibogora wilayani Ngara Elias Gozi akiongea na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Jumanne Oktoba 9 alimtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Fausta Emanuel mwenye miaka 17 aliyejifungua siku kumi kabla ya kuanza mtihani huo ulioanza Oktoba 8 mwaka  huu

Gozi alisema mwanafunzi huyo hakugundulika mapema kwa kuwa alikuwa mtoro wa kuanzia mwezi mei lakini alisajiliwa kufanya mtihani huo wa taifa na taarifa za kujifungua zilipatikana siku ya mtihani akiwa ameshafanya somo la Civics shuleni hapo

Alisema kuwa Baada ya wanafunzi wenzake kutoa taarifa za mwanafunzi huyo kuwa na mtoto mazingira ya nje ya shule uongozi wa shule kwa kushirikiana na Afisa Elimu Sekondari wilayani Ngara Julius Nestory walimhoji kuhusu tukio hilo jambo ambalo alilipinga na kufanya somo la pili la kiingereza

“Nikueleze ndugu mwandishi mimi nina siku chache nimekabidhiwa shule hii hivyo sikuwa na taarifa yoyote kuhusu mwanafunzi huyo na inasikitisha  hata walimu wazoefu wa shule hii hawakulieleza hili mapema ili kumkataza kabla ya kusambaa wilayani”Alisema mkuu wa shule

Elias Gozi  aliongeza kuwa mara baada ya kumaliza somo la pili alitakiwa kutoa maelezo kwa maandishi ya kukana au kukubali kuwa amejifungua na anaye mtoto mchanga na baada ya kutafakali kwa kina alikiri kuwa amejifungua siku 10 zilizopita akiwa nyumbani kwa wazazi wake kijiji cha Bugarama wilayani Ngara

Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Wilayani Ngara Julius Nestory alithibitisha kusimamishwa kwa mwanafunzi huyo na kwamba atafanya mtihani mwakani akiwa ni mwanafunzi wa kujitegemea kwani sheria ya elimu nchini hairuhusu mwanafunzi wa sekondari kuendelea na shule akiwa na motto kuoa au kuolewa

Nestory alisema serikali imeanzisha mpango wa elimu ya masafa kwa walioshindwa kupata elimu ya sekondari kwa kusoma moduli za masomo kwa muda wa mwakammoja hadi mitatu na wanaweza kufanya mtihani kama wakujitegemea na kupata vyeti vya elimu ya sekondari

Alisema kuwa mwanafunzi wa shule hiyo pamoja na aliyeko katika shule ya sekondari ya kata ya kibimba wilayani Ngara wanapaswa kupelekwa katika hospitali na madaktari kuthibitisha  kujifungua kwao na taarifa zao ziambatanishwe kwenye taarifa ya mitihani

No comments:

Post a Comment