November 5, 2012

Leo ndio Leo,Obama, Romney nani kuwa rais wa Marekani?

Waombea kiti cha Urais marekani-Barack Obama na Mitt Romney
WASHINGTON, Marekani
WANANCHI  wa Marekani leo wanaelekea kwenye vituo vya kupigia kura katika uchaguzi wa Rais huku wagombea, Rais Barack Obama(Democrat)  na Mitt Romney (Republican) wakichuana vikali katika majimbo yanayojulikana kwa Pendulum ( Swing States) ambayo ndiyo yanayotarajia kutegua kitendawili cha mchuano huo.

Obama( 51) na mpinzani wake Romney( 65) wanazidiana kidogo kwa mujibu wa maoni yanayochapichwa na vyombo vya habari na hapo jana kila mmoja alipanda jukwaani kuwashawishi wapigakura ambao bado hawajaamua nani wamchague.

Jimbo la Ohio ndilo linalotajwa kuwa moja ya majimbo muhimu ambalo lina nafasi kubwa  kubadilisha upepo wa kisiasa kwa wagombea wote. Obama na Romney walitumia siku ya mwisho wa kampeni zao kuzungukia maeneo ya jimbo hilo kuwashawishi wapigakura ambao bado walikuwa hawajafanya maamuzi.

Maoni yamekuwa yakiwaonyesha wawili hao wakikaribiana kwa sana, lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema Obama bado ana nafasi ya kushinda.

Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa,Edward Wycof William anasema maoni yamekuwa yakibadilika kutoka wiki moja hadi nyingine, lakini kilichoonekana ni kwamba Romney hajaongoza kabisa katika maoni yoyote katika majimbo muhimu.

Obama anatafuta awamu ya pili, huku kiwango cha ukosefu wa ajira kikiwa asilimia 7.2 na mpinzani wake ametumia karata hiyo kuwashawishi wapiga kura.

Ripoti zinasema kuwa katika historia ya Taifa la Marekani, hakuna Rais aliyefanikiwa kupata muhula wa pili tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia kukiwa na kiwango cha ukosefu wa ajira kilicho juu ya asilimia 7.2.

Kulingana na takwimu za wanauchumi, uchumi wa Marekani bado unakua kwa chini ya asilimia 2, lakini Obama amewakumbusha wapigakura juu ya mazingira ya mgogoro alimochaguliwa miaka minne iliyopita.

Takriban watu milioni 27 wamekwishapiga kura katika uchaguzi wa mapema akiwemo Rais Obama mwenyewe.

Katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2008 watu waliojitiokeza kupigakura katika uchaguzi wa mapema ilikuwa milioni 130.

Wapiga kura wanatarajiwa kuamua hatma ya viti vyote 435 vya Bunge la wawakilishi ambalo linatarajiwa kuendelea kudhibitiwa na chama cha Republican na theluthi moja ya viti vya bunge la Seneti lenye viti 100, ambako chama cha Democrats kinatarajiwa kuendeleza udhibiti mdogo.

Uchaguzi wa mwaka huu unafanyika wakati sehemu ya Kaskazini Mashariki inakabiliana na madhara ya kimbunga Sandy kilichoharibu maelfu ya makazi na kuua watu zaidi ya 100.

Obama anaendelea kuwa na faida dhidi ya Romney katika majimbo yenye maamuzi, ambayo ndiyo yanaamua mshindi wa urais.

 Ili kushinda kiti hicho, mgombea lazima apate kura 270 za majimbo(Electoral Collage). Obama anahitaji kujihakikishia kura 243 za majimbo yanayoegemea chama cha Democrats, wakati Romney anaweza kujihakikishia kura 206.

Baadhi ya duru zimesema kuwa pande zote mbili zimeweka matumaini ya kuwa na mvutano wa muda mrefu na inaaminika kuwa huenda kukashuhudiwa uamuzi wa ushindi katika baadhi ya majimbo yenye ushindani mkubwa ukafanywa na mahakama.

Hali ya vuta nikuvute ilijitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2000 ulioshuhudia mahakama ikimpa ushindi George W. Bush dhidi ya mpinzani wake Al Gore.

Katika uchaguzi huo, George W. Bush alishindwa na mgombea wa Democrat katika kura za moja kwa moja za wananchi lakini alipata kura nyingi za "Electoral College" ambayo ndiyo taasisi inayomchagua rasmi Rais wa Marekani.

Mgogoro huo wa uchaguzi ulidumu kwa kipindi cha wiki tano bila ya kupatikana ufumbuzi wowote, huku mawakili wa wagombea hao wawili wakitumbukia kwenye vita vikubwa vya kisheria.

Hatimaye ulitatuliwa kwa uingiliaji kati wa Mahakama Kuu ya Marekani ambayo ilimtangaza Bush kuwa mshindi katika uchaguzi huo, licha ya kushindwa na mgombea wa upinzani katika kura za wananchi.

Kituo cha Televisheni ya Marekani  CNN kwa upande wake imekiri kuweko hali hiyo na kuripoti kuwa wananchi wengi wa Marekani hawapendezwi na mfumo wa kutochaguliwa rais wa nchi hiyo kwa kura za moja kwa moja za wananchi na wametaka sheria hiyo ifutwe  katika katiba ya Marekani.

Mfumo wa kuchaguliwa rais wa Marekani na wawakilishi wa majimbo maarufu kwa jina la Electoral College ulianza kufanya kazi nchini humo katika karne ya 17 wakati yalipofikiwa makubaliano maalumu ya kisiasa.

Wakosoaji wa mfumo huo wanasema kuwa, hivi sasa hakuna sababu zozote za kuhalalisha kuendelea kutumika kwani wanadai kuwa majimbo ya Marekani hivi sasa hayana tena nguvu kubwa zilizoshuhudiwa awali wakati wa kutungwa kwa sheria hiyo.

Katika historia ya Marekani, imeshatokezea mara nne ambapo mgombea wa urais alipata kura nyingi za wananchi lakini akashindwa kwa kura za Electoral College.

 Katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2000, mgombea wa Democrat alimshinda  Bush wa Republican kwa karibu kura 500, lakini Bush alikuwa rais kutokana na kupata kura 271 za Electoral College ikilinganishwa na 266 za mgombea wa Democrat.

Ili kushinda katika uchaguzi huu mgombea analazimika kujikusanyia kura za  electoral Collage zisizopungua 270 na tayari Obama amejikusanyia kura 237 wakati mpinzani wake Romney akifikisha kura 206. Kitendawili kimesalia katika majimbo ambayo wapiga kura wake bado hawajashawishika yanayoshikilia kura 95.

Uchaguzi unaofanyika leo

Katika uchaguzi unaofanyika leo ripoti za awali zinaonyesha kuwa Obama anaongoza kwa asilimia sita dhidi ya Romney katika jimbo la Ohio na kwa asilimia mbili katika jimbo la Florida.

Katika jimbo la Florida, Romney amebanana na Obama kwa kuwa wakazi hao wanasema kuwa Romney anaonyesha ana uwezo wa kusimamia uchumi, lakini baadhi yao wameeleza kuwa Obama ataweza kufanya kazi nzuri zaidi na ndiyo maana anaongoza kwa asilimia mbili.

Kati ya watu kumi waliokuwa wakihojiwa katika majimbo haya mawili  kuhusu wagombea hao, saba kati yao walieleza kuwa Obama amefanya kazi nzuri katika kupambana na kimbunga cha Sandy.

Katika utafiti uliotolewa na kituo cha utafiti cha Pew unaonyesha kuwa Obama anaongoza kwa asilimia tatu dhidi ya Romney katika kura za awali.

Inaonyesha mchuano ni mkali kati ya wagombea hao wawili kutokana na kubadilika badilika, lakini Obama anaonekana kuwa na asilimia zinazomlinda hasa kwa kuyashika majimbo ya Iowa, Ohio na Florida huku kukiwa na mchuano mkali kati yao katika jimbo la New Hampshire.

Katika jimbo la Iowa, Obama anaongoza kwa asilimia 47 dhidi ya 42 za Romney kwa mujibu wa utafiti wa Des Moines Register Poll uliochapishwa juzi na kwamba Romney ameongoza kwa alama tatu kutokana na wanaume waliopiga kura huku  Obama akipata alama 12 kutokana na kura zilizopigwa na wanawake.

Katika jimbo la New Hampshire inaonekana Obama na Romney wamekabana koo kwa kuwa kura za awali zinaonyesha wote wana asilimia 47.
 Wiki mbili zilizopita Obama alikuwa akiongoza kwa alama nane katika jimbo hilo kwa mujibu wa utafiti wa kituo cha utafiti cha Chuo cha New Humpshire.

Jimbo la Pennsylvania linaonyesha kuwa wagombea hao wawili wanapambana vikali huku Obama akiongoza kwa asilimia tatu dhidi ya Romney.

Kwa mujibu wa utafiti wa Chuo cha Muhlenberg unaonyesha kuwa Obama ana asilimia 49 huku Romney akiwa na asilimia 46 hiyo inaonyesha sura nzuri kwa Obama ambaye utafiti wa awali uliofanyika katikati ya Oktoba katika jimbo hilo ulionyesha Romney akiongoza kwa asilimia 4.

Tafiti zilizotolewa mwishoni mwa wiki zinaonyesha wagombea hao wawili wanakabana koo katika majimbo ya Colorado, North Carolina na Virginia huku Obama akiongoza Michigan, Minnesota, Nevada na Wisconsin.

Kwa mwenendo huo Obama anaonekana kuongoza katika maeneo mengi kutokana na tafiti hizo mbalimbali zilizotolewa.

Hata hivyo chama cha Republican kimeeleza kuwa tafiti hizo haziko sawa kwani waliohojiwa na wanaotoa matokeo ya tafiti hizo wengi ni wafuasi wa Democrat.
          Source:-Mwananchi news paper

No comments:

Post a Comment