August 15, 2013

MAJAMBAZI WAUAWA MWANZA,INASADIKIKA KUWA WENGINE NI WA NGARA


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu

WATUHUMIWA watatu wa ujambazi wameuawa baada ya kurushiana risasi na polisi katika eneo la Igogo jijini Mwanza, katika jaribio la kuvamia Kituo cha Mafuta cha GBP.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, alisema jaribio hilo lilifanyika juzi kati ya saa 2 na 3 usiku, katika kituo hicho cha mafuta kilichopo katika barabara ya Kenyata.

Alisema majambazi ambao idadi yake haikufahamika mara moja, baada ya majibizano ya risasi na polisi, wengine walitoroka lakini askari Polisi walifanikiwa kukamata bunduki moja aina ya SMG, yenye namba ya usajili 2916 pamoja na risasi saba.


Akifafanua, Mangu alisema walipokea taarifa kutoka kwa raia wema juu ya kuwepo kwa majambazi kutoka Ngara yaliyopanga njama ya kuvamia kituo hicho cha mafuta.

Alisema majambazi hayo yalipofika katika eneo la tukio na kujiandaa kuvamia kituoni hapo, polisi nao walijitokeza, ndipo walipoanza kurushiana risasi na majambazi hao, ambapo watuhumiwa watatu waliuawa huku wengine wakitokomea kusikojulikana.

Katika eneo la tukio kwa mujibu wa Kamanda Mangu, yaliokotwa maganda ya risasi 22 huku miili ya watuhumiwa ikihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando na Polisi mkoani hapa linaendelea na uchunguzi.

Kamanda Mangu ametoa mwito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri kwa jeshi hilo, ili lizuie matukio ya uhalifu.

Katika tukio lingine, watu wasiojulikana wameteketeza kwa moto nyumba tisa za nyasi za familia moja katika kijiji cha Nyehunge wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
  SOURCE:Habari Leo

No comments:

Post a Comment