June 28, 2014

Jicho kumtambua mpiga kura


TUME ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) itatumia vifaa vya kisasa vya kumtambua mpiga kura aliyepoteza kitambulisho kwa kutumia mboni ya jicho lake, wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Damian Lubuva mkoani hapa jana kwenye mkutano na waandishi wa habari juu ya maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa ukusanyaji taarifa za wapiga kura kwa njia ya elektroniki (Biometric Voter Registration – BVR).
Lubuva alisema katika chaguzi zilizopita kumekuwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo za baadhi ya watu kukosa haki zao za kupiga kura kutokana na majina yao kutoonekana kwenye daftari la kupiga kura, huku wengine wakijiandikisha mara mbili na kufanya udanganyifu katika chaguzi hizo.
Alisema kutokana na kasoro hizo, sasa tume yake imeagiza vifaa vya kitaalamu vya kumtambua mpiga kura kwa mboni ya jicho lake.
Lubuva alisema vifaa hivyo vitachukua taarifa ya mtu kibaolojia na kuhifadhi kwenye kumbukumbu kwa ajili ya kumtambua mpiga kura na kumtofautisha na mwenzake.
Ofisa Elimu ya Mpiga Kura, Salvatory Alute, alisema lengo la uboreshaji wa daftari hilo la kudumu la wapiga kura awamu ya kwanza ni kuondoa majina ya watu waliopoteza sifa kwa kufariki.
“Wapiga kura wapya na wa zamani ambao watakuwa na kadi za kupigia kura watatakiwa kwenda kwenye vituo vyao vya kujiandikisha ili kuchukuliwa taarifa zao, hasa alama za vidole, picha na saini zao ambazo zitaingizwa kwenye mfumo mpya wa Biometric Voter Registration na kupewa vitambulisho vipya,” alisema
Source:Tanzania daima

No comments:

Post a Comment