Wasomi wataka wanasiasa waondolewe Bunge la Katiba
SOURCE:-Mwananchi
Dar es Salaam. Wasomi na wataalamu mbalimbali
wameshauri kuangaliwa upya kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili
kuwabana wajumbe wanaotumia vikao vya Bunge Maalumu kujijenga kisiasa
kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu 2015, badala ya masilahi ya wananchi.
Wamesema Bunge hilo linakosa maridhiano kwa kuwa
wajumbe wake wanatetea masilahi yao ya kisiasa badala ya maoni ya
wananchi ambayo waliyapendekeza wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ikikusanya maoni.
Agosti 2, mwaka huu wakati wa mdahalo uliohusu
mivutano ya makundi katika mchakato wa Katiba Mpya, Mkurugenzi wa Shule
ya Sheria ya Kenya (KSL), Profesa Patrick Lumumba alisema katika maeneo
mengine, sheria huwabana wajumbe wanaoteuliwa kuingia kwenye Bunge la
Katiba kuwania nafasi za kisiasa hadi baada ya miaka mitano, ili kuepuka
kupitisha mambo kwa masilahi binafsi.
Akizungumzia hoja hiyo jana, Rais wa zamani wa
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Felix Kibodya alisema: “Wanasiasa
wameuweka rehani mchakato wa kupata Katiba Mpya. Kosa la kwanza
tulilofanya ni kuruhusu wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Baraza la
Wawakilishi kuwa wajumbe wa Bunge hilo.”
Alisema wawakilishi wa taasisi mbalimbali zisizo
za kiserikali na kutoka makundi mbalimbali (si ya kisiasa) ndiyo
waliotakiwa kuwa wajumbe wa Bunge hilo.
“Mwakani ni uchaguzi na wajumbe wengi wanalenga
zaidi jambo hilo. Hata ukitazama mchakato wenyewe, utaona haujahusisha
zaidi wanasheria kama ilivyo kwa nchi kama Kenya,” alisema Kibodya.
Mtaalamu wa lugha na falsafa nchini, Faraja
Christoms alitaja makosa matatu yaliyofanyika kuwa ni kuruhusu Rais
kuteua wajumbe wa Bunge hilo, wanasiasa kuwa sehemu ya wajumbe na
kuruhusu mchakato huo kutawaliwa na wanasiasa.
“Nadhani Rais Kikwete angevunja Bunge la Katiba
ili fedha za kuwalipa wajumbe wake kwa muda wote watakaokaa Dodoma
zipelekwe kuwalipa walimu na watumishi wengine wa Serikali,” alisema.
Alisema sifa za mjumbe wa Bunge hilo kwanza ni
kutokuwa mwanasiasa na hata akiwa, sheria ieleze kuwa hataweza kugombea
uongozi kati ya miaka mitatu hadi mitano na kwamba mjumbe huyo
asiruhusiwe kuwa na ajenda ya chama au kundi alilotoka.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Balozi Job Lusinde
alisema: “Tatizo lilianza baada ya kuchagua wajumbe wa Bunge la Katiba
na kuwachanganya na wajumbe wengine ambao ni wabunge wa Bunge la Jamhuri
na Baraza la Wawakilishi.
“Tulitakiwa kuwa na wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka makundi mengine, lakini si wanasiasa wala wabunge.”
Balozi Lusinde alisema idadi kubwa ya wajumbe hao
wanatetea masilahi yao yanayolenga uchaguzi mkuu ujao na kwamba kwa
mtindo huo ni vigumu Katiba Mpya kupatikana kwa sasa.
No comments:
Post a Comment