March 3, 2015

Wimbo wa Komba wamliza Kikwete

Rais Jakaya Kikwete akiwa katika hali ya majonzi wakati wasanii walipokuwa wakiimba wimbo maalumu wa kumuaga Mbunge wa Mbinga Magharibi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Marehemu John Komba katika Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Spika wa Bunge, Anne Makinda. Picha ndogo ni jeneza lililobeba mwili wa Komba. Picha na Anthony Siame 
SOURCE: MWANANCHI
Dar es Salaam. Wimbo wa John Komba aliouimba katika msiba wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999, jana uliibua majonzi na kusababisha viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, kutoa machozi ulipoimbwa kumuaga mbunge huyo.
Wimbo huo uliobadilishwa maneno yanayohusu Mwalimu Nyerere na kuingizwa yanayomtaja mbunge huyo wa Mbinga Magharibi, mbali na Rais Kikwete ulimliza pia Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba na waombolezaji wengine.
Sehemu ya mashairi ya wimbo huo uliokwenda kwa jina la “Nani Yule” ulioimbwa na wanamuziki mbalimbali wa bendi nchini, na kuwatoa watu machozi iliimbwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
“Kapteni Komba familia yako umeiacha na nani, chama chako umekiacha na nani, nenda baba msalimie Mwalimu, mweleze hali ya Watanzania ilivyo hivi sasa, mweleze hali ya nchi yetu ilivyo hivi sasa hasa wakati huu, msalimie Mzee Kawawa Simba wa Vita”
Baadhi ya wanamuziki walioshiriki kuimba wimbo huo ni King Kiki, Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata, Jose Mara ambaye ni mwanamuziki wa bendi ya Mapacha Watatu na Luiza Mbutu wa African Stars.
Wakati wanamuziki hao wakiendelea kuimba wimbo huo, idadi ya watu wanaolia ilizidi kuongezeka, hasa wanafamilia ndugu na jamaa wa marehemu.
Waombolezaji walisikika wakilia huku wakisema, “Jamani alikuwa akitunga nyimbo kuwaimbia wenzake waliofariki dunia, sasa leo anaimbiwa yeye.”
Alipofariki Mwalimu Nyerere Oktoba 14, mwaka 1999, aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Komba akiwa na bendi ya TOT alitunga nyimbo za maombolezo ukiwamo wa “Nani Yule’, ‘Kwaheri Mwalimu’, ambazo jana zilitumiwa na wanamuziki kumuimbia yeye, wakibadilisha baadhi ya maneno.
Mwili wa mbunge huyo (61) aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita kwa ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, uliagwa katika viwanja vya Karimjee ambapo salamu mbalimbali za rambirambi zilitolewa kabla ya mwili huo kusafirishwa kwenda Songea mkoani Ruvuma.
Hata wakati wa kuagwa mwili huo, idadi kubwa ya wabunge wenzake waliohudhuria walishindwa kujizuia kulia huku wakikumbushana ucheshi aliokuwa nao Komba enzi za uhai wake.
Pengine msiba huo utakuwa umewagusa wengi wanaomfahamu kwa mambo mengi, na kwa kuwa kipindi hiki nchi inajiandaa kupata rais mpya, kwa kuwa kazi yake kubwa ilikuwa ni kuipigia debe CCM kupitia uimbaji wake.
Kulingana na maelezo ya waombolezaji, Mwanajeshi huyo aliyestaafu akiwa na cheo cha kapteni alikuwa ni mtu ambaye hakusita kueleza kile alichokiamini, jasiri asiyekubali kushindwa, mcheshi wakati fulani na mtu wa kutoa misaada

No comments:

Post a Comment