February 19, 2016

Besigye akamatwa tena na polisi Uganda


Wanajeshi wa Uganda wakishirikiana na maafisa wa polisi wamevamia na kuzingira afisi za chama cha upinzani za Forum for Democratic Change (FDC).
Kiongozi wa chama hicho, Dkt Kizza Besigye, ambaye amekuwa akiwania urais amekuwemo ndani ya afisi hizo na mwandishi wa BBC Patience Atuhaire anasema polisi wameondoka naye akiwa kwenye gari lao.
Kituo cha televisheni cha NBS kimeripoti kuwa Besigye na rais wa FDC Mugisha Muntu wamekamatwa katika makao makuu hayo eneo la Najjanankumbi, na wafuasi wa chama hicho wakatawanywa kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi.    BBC


Marekani yalaani kukamatwa kwa Besigye

Marekani imelaani kukamatwa na kuzuiwa kwa muda kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye, anayetumai kuifikisha kikomo miaka 30 ya utawala wa rais wa sasa wa Uganda, Yoweri Museveni
Huku kura zikiendelea kuhesabiwa nchini Uganda kufuatia uchaguzi wa rais na bunge uliofanyika hapo jana, Marekani imeilaani vikali serikali ya Uganda baada ya maafisa wa usalama kumkamata kwa muda mfupi mgombea urais wa upinzani Kizza Besigye. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani John Kirby alisema kitendo hicho kinatilia shaka uwajibikaji wa Uganda kufanya uchaguzi huru, wa haki na ulio wazi.
Besigye ambaye ni mgombea wa upinzani mwenye ushawishi mkubwa miongoni mwa wagombea saba wanaoshindana na Rais Museveni, alitiwa mbaroni wakati alipokuwa akichunguza madai ya wizi wa kura uliofanywa na chama tawala cha National Resistance Movement, NRM.
Msemaji wa chama cha Besigye, Forum for Democratic Change, FDC, Semuju Nganda, alisema kiongozi huyo alikamatwa wakati alipokuwa akifanya uchuguzi katika kituo kisicho halali kilichokuwa kikisimamiwa na maafisa wa usalama katika mji mkuu, Kampala.
Msemaji wa polisi Fred Enaga alithibitisha baadaye kwamba Besigye aliachiliwa na kupelekwa nyumbani kwake, akisema walimzuia kiongozi huyo wa upinzani kuingia eneo la usalama ambalo raia hawakuruhusiwa.
Ingawa Besigye aliachiwa huru, msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kirby alisema kuachiwa kwake hakufuti ukweli kwamba alikatwa.      DW


No comments:

Post a Comment