January 1, 2016

2016-TANZANIA NA SERIKALI YA MAGUFULI

Mambo 9 ya kutolea macho mwaka 2016

WATANZANIA wanauanza mwaka mpya wa 2016 leo huku wengi wakiwa na shauku ya kujua hatma ya mambo kadhaa yakiwamo ya kuanza kwa utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni zake za kuomba ridhaa ya kuingia Ikulu.
 
Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015, Magufuli aliyekuwa akipeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliibuka mshindi baada ya kuzoa asilimia 58.46 ya kura zote halali zilizopigwa na hivyo kuwaacha wapinzani wake saba, akiwamo Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyekuwa akichuana naye kwa karibu katika kipindi chote cha kampeni.
 
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kupitia mahojiano na wachambuzi mbalimbali wa masuala ya siasa, uchumi na jamii umebaini kuwa yapo mambo takriban tisa ambayo Watanzania wengi wanatarajiwa kuyafuatilia kwa karibu ili kujua kitakachotokea. Kwa kiasi kikubwa, mambo hayo yamejikita katika Nyanja za siasa, uchumi na kijamii.
 
Katika uchunguzi wake, Nipashe imeyabaini mambo hayo kuwa ni utekelezaji wa ahadi ya elimu bure kwa kila mtoto wa Tanzania kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne; mchuano wa wabunge watokao CCM na wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi;  kuendelea kwa mchakato wa katiba mpya; hatma ya Zanzibar baada ya kufutwa kwa matokeo yake ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25; athari za kuendelea kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia; kuendelea kuporomoka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani; tishio la mvua kubwa za el-nino kwa usalama wa chakula na miundombinu na pia mustakabali wa utitiri wa magari ya kifahari maarufu kama ‘mashangingi’ katika taasisi na mashirika ya umma.
 
“Kuanza kwa mwaka huu ni muhimu kwa historia ya Tanzania kwani kuna matumaini makubwa ya kuanza utekelezaji wa ahadi kubwa za serikali ya awamu ya tano ikiwamo ya utoaji wa elimu bure, ujenzi wa fly-overs, mpango wa kugawa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji na kila mtaa na pia ujenzi wa zahanati katika kila kijiji,” alisema mmoja wa wachambuzi waliozungumza na Nipashe.
 
Ahadi elimu bure, zahanati kila kijiji
Utekelezaji wa ahadi kuu za serikali ya awamu ya tano ni mojawapo ya eneo linalotarajiwa kufuatiliwa na Watanzania kwa karibu mwaka huu. Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, Magufuli aliwakuna wengi kutokana na ahadi zake kuhusiana na uboreshaji wa huduma za jamii kama elimu, afya na maji. Karibu katika kila eneo alilofika na kufanya mikutano yake ya kampeni, Magufuli alisisitiza kuwa serikali yake itabeba jukumu la kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne na kwamba, hakutakuwa na mchango wowote kwani anapoahidi elimu anamaanisha ‘ni bure kweli’ pasi na kuwasumbua wananchi kwa michango itokanayo na kisingizio chochote kile.
 
Hivi karibuni, Rais Magufuli aliamuru kuwa Sh. bilioni 136 zilizotokana na mapato yaliyovunja rekodi ya Sh. trilioni 1.3 kwa mwezi yaliyokusanywa na Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) zielekezwe katika sekta ya elimu ili kuanza utekelezaji wa ahadi ya elimu bure kuanzia Januari, 2016. Kadhalika, mwaka huu serikali inatarajiwa pia kutoa mwelekeo wa namna ya kuanza kwa utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya katika kila kata, hospitali ya wilaya katika kila wilaya na kuwapo kwa hospitali ya rufaa katika kila mkoa. Mpango wa kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji nchini kwa kasi mpya ya serikali ya awamu ya tano inayobebwa na kauli mbiu ya ‘hapa kazi tu’ ni eneo jingine linalotarajiwa kufuatiliwa kwa karibu. Ahadi nyingine maarufu zitakazofuatiliwa kwa karibu ni ya kutoa milioni 50 kwa kila kijiji na kila mtaa na pia ujenzi wa barabara za juu (flyovers) kwa nia ya kupunguza foleni za magari katika makutano ya barabara kuu kama za Mandela na Nyerere jijini Dar es Salaam.  Ipo pia ahadi ya kuanzishwa kwa mahakama ya kushughulikia ufisadi, ikibebwa na kauli ya Magufuli katika mkutano mmojawapo wa kampeni pale aliposema: “Nitasimamia uundwaji wa Mahakama ya kushughulikia mafisadi na majizi wa nchi hii ili wafungwe.”
 
Siasa za CCM, Ukawa kuhamia bungeni
Hakika, hili ni eneo jingine linalosubiriwa kwa hamu mwaka huu. Baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015, sasa joto la kisiasa linatarajiwa kuhamia katika vikao vya Bunge la 11 ambavyo vitaanza Januari 27, 2016. Kuongezeka kwa idadi ya wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, ambao sasa wamefikia 121, kunatarajiwa kuongeza mchuano baina yao na wabunge wa chama tawala, CCM. 
 
Mchakato wa katiba mpya
Baada ya kukwama kwa mchakato wa kuundwa kwa katiba mpya katika serikali ya awamu ya nne, sasa wwali kubwa linalotatiza wengi ni lile la kutaka kujua kwamba je, Serikali ya Magufuli itaendelea pale katiba hiyo iliposhia kwa kuruhusu upigaji kura wa wananchi kwa katiba inayopendekezwa au mchakato utaanza tena upya kwa kukusanya maoni nchi nzima kama ilivyofanywa na kamati maalumu iliyoongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba? Hili ni jambo linalotarajiwa kupatiwa majibu mwaka huu.  
 
 
Hatma ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar 
Tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, afute uchaguzi mkuu wa visiwa hivyo Oktoba 28, 2015, kumekuwa na mgogoro mzito wa kisiasa baina ya pande mbili kuu, yaani chama tawala (CCM) kinachosisitiza kuwa uamuzi wa Jecha uheshimiwe kwa kurudia uchaguzi huo na CUF kinachotaka mchakato wa majumuisho ya kura uendelee kwani hakukuwa na kasoro kubwa za kuufuta uchaguzi huo wote hasa baada ya kusifiwa na waangalizi wa ndani na wa kimataifa kuwa ‘ulikuwa huru na wa haki’.
 
Hadi sasa, mazungumzo yamekuwa yakiendelea baina ya CCM chini ya mgombea wake wa urais, Dk. Ali Mohamed Shein na CUF inayoongozwa na mgombea wake wa nafasi hiyo ya urais, Maalim Seif Shariff Hamad. Je, nini hatma ya mazungumzo hayo na mustakabali wa Zanzibar baada ya hapo? Wengi wanatarajia kupata majibu mwaka huu unaoanza leo.
 
Kushuka bei ya mafuta katika soko la dunia
Eneo jingine linalotarajiwa kuangaliwa kwa jicho la karibu na Watanzania walio wengi ni pamoja na athari za kiuchumi zitokanazo na kuporomoka kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia.  Wapo wanaotaka kujua kama kushuka huko kwa bei ya mafuta kutaleta matokeo ya kuonekana kwa uchumi wa nchi na pia kwa mtu mmoja mmoja.
 
Kwa mfano, wakati serikali ya awamu ya nne ya Rais Kikwete ikiingia madarakani kwa mara ya pili mwaka 2005, pipa moja la mafuta ghafi katika soko la dunia lilikuwa likiuzwa kwa wastani wa dola za Marekani 90. Hata hivyo, bei hiyo iliendelea kuporomoka siku hadi siku na hadi kufikia jana, pipa moja la mafuta ghafi, kwa mujibu wa Shirika la habari la Reuters, lilikuwa likiuzwa kwa dola za Marekani 37.18.
 
Swali kubwa linalotarajiwa kuwa vichwani mwa wengi ni kwamba je, Serikali ya Magufuli itawezesha vipi wananchi wa kawaida kunufaika kiuchumi kutokana na kushuka huko kwa bei ya mafuta katika soko la dunia? Uchumi mpana utaathiriwa vipi na anguko hilo la bei ya mafuta kila uchao?
 
Kuporomoka kwa thamani ya shilingi
Kati ya mambo ambayo yamekuwa yakitajwa kuwa na athari hasi za kiuchumi ni kuporomoka kila uchao kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
 
 Kwa mfano, wakati serikali ya Rais Kikwete ikiingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005, dola moja ya Marekani ilikuwa ikibadilishwa kwa wastani wa Sh. 1,162.23; mwaka 2010, dola moja ilikuwa ikibadilishwa kwa wastani wa Sh. 1,410.22 lakini kufikia jana, kwa mujibu wa taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), dola moja hubadilishwa kwa Sh. 2,159.21. Watanzania wengi wanatarajia kuona serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli ikitafuta njia bora ya kudhibiti kasi ya kuporomoka kwa shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
 
Tishio la mvua za el-nino
Kwa mujibu wa ripoti za mamlaka mbalimbali za hali ya hewa ikiwamo TMA, Tanzania ni miongoni mwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki zeney uwezekano wa kukumbwa na baa la mvua za el-nino. 
 
Kama hofu hiyo itakuwa ya kweli, hasa kutokana na mwelekeo wa hali ya hewa, maana yake ni kwamba serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli itakumbana na changamoto ya kuandaa mikakati ya kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na mvua za el-nino. 
 
Mvua za aina hiyo ziliponyesha mwaka 1998, taifa lilikumbana na athari kubwa za kuharibika kwa miundombinu ya usafiri kama reli na barabara, madaraja yalisombwa na majengo kadhaa kuliharibiwa. Aidha, mvua hizo kubwa huathiri uzalishaji wa chakula na hivyo kuibua hofu ya kuwapo kwa njaa. Tishio hilo la el-nino ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kufuatiliwa kwa karibu mwaka huu wa 2016.
 
Mustakabali wa ‘mashangingi’ serikalini 
Wakati akilihutubia Bunge la 11 kabla ya kulizindua Novemba 20, 2015, Rais Magufuli alisisitiza dhamira ya serikali yake kuhakikisha kuwa matumizi ya magari ya serikali yanadhibitiwa, hasa yale ya ‘kifahari’ aina ya VX-V8 maarufu kama mashangingi. Kinachosubiriwa na wengi kuanzia leo, ni kuona kama matumizi ya magari hayo yatasitishwa rasmi ama la.
 
Mchakato wa Magufuli kutwaa uenyekiti CCM
Baada ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wa CCM na baadaye kuibuka mshindi, Magufuli anatarajiwa kutwaa nafasi ya uenyekiti wa chama hicho ili kutimiza dhana ya ‘kofia mbili’, yaani Rais kuwa vilevile ndiye mwenyekiti wa chama hicho. Kwa mujibu wa katiba ya CCM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete bado anastahili kushikilia wadhifa huo hadi mwaka 2017. Hata hivyo, desturi ya chama hicho ya kuzingatia dhana ya ‘kofia mbili’ inampa Magufuli nafasi ya kuwa mwenyekiti kabla Kikwete kumaliza muda wake. Hivyo, hili ni eneo mojawapo linalotarajiwa kuangaliwa kwa karibu ili kujua mwelekeo mpya wa chama tawala chini ya uenyekiti wa Rais Magufuli.
 
WASEMAVYO WANASIASA KUHUSU MWAKA MPYA
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliiambia Nipashe kuwa mwaka ulioisha jana wa 2015 ulikuwa ni mzuri kwa kuwa uchaguzi ulimalizika salama pasipo kuwa na fujo na wao kuaminiwa na Watanzania kuendelea kuongoza.
Aliongeza kuwa kwa mtazamo wake, mwaka 2015 ulikuwa ni wenye matukio mengi mazuri na machache mabaya.
Mwenyekiti wa Chama Cha United Peoples Demokratic Party (UPDP),  Fahmi Dovutwa, alisema mwaka uliopita  ulikuwa ni wa changamoto  kubwa kisiasa kutokana na kuwapo kwa uchaguzi mkuu na kwamba, muhimu linalopaswa kuzingatiwa kwa mwaka unaoanza leo ni kuendelea kutunzwa kwa amani ya nchi.
Katibu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba alisema mwaka 2015 ulikuwa ni mwaka wa mafanikio kwa chama chao kwa kuwa walifanikiwa kusimamisha mgombea urais katika uchaguzi mkuu na mwishowe wakafanya vizuri kwa kushika nafasi ya tatu.
 
Katika uchaguzi mkuu, ACT ambacho ni chama kipya, kilipata mbunge mmoja, madiwani 51 nchi nzima, pamoja na kuongoza halmashauri ya Kigoma Ujiji na kupata meya.
 
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari, alisema mwaka 2015 ulikuwa ni mwaka mzuri kwao kwani walipata wabunge wengi kulinganisha na chaguzi zilizopita na hivyo, mwaka huu wataendeleza harakati zao za kujiimarisha zaidi na mwishowe kujiongezea wanachama.
 
Mbunge Waitara baada ya kusikiliza taarifa hizo kutoka kwa diwani na kwa mwenyekiti wa shule, alisema kuwa atafika Ofisi za Ilala na kesho atafanya mkutano wa hadhara ili wanakijiji wafahamu hali halisi ya eneo hilo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment