September 9, 2014

Uamuzi mgumu,Rais hataongeza muda Bunge la KatibaUamuzi mgumu,Rais hataongeza muda Bunge la Katiba


Source:Mwananchi

Dodoma. Makubaliano baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kutaka Bunge Maalumu lifikie ukomo Oktoba 4, mwaka huu yamezua sintofahamu mjini hapa huku uamuzi huo ukionekana kuwachanganya viongozi wa Bunge hilo.
Kutwa nzima ya jana, viongozi wa Bunge Maalumu walishinda kwenye vikao vya mashauriano huku wabunge wa CCM wakitarajiwa kukutana jana usiku kwenye makao makuu ya chama hicho kupewa taarifa rasmi za uamuzi huo.
Katika makubaliano baina ya TCD na Rais Kikwete, imeamuliwa kuwa uamuzi wa Rais kupitia Tangazo la Serikali (GN) 254 la kuongeza siku 60 hadi Oktoba 4 uheshimiwe na baada ya tarehe hiyo Bunge liahirishwe.
Uamuzi huo ni kinyume cha azimio la Bunge Maalumu la Agosti 5, 2014 ambalo lilirekebisha Kanuni ya 14 (4) na kuifuta Jumamosi katika siku zilizotajwa kuwa za kazi, pia sikukuu na siku za Jumapili.
Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alikaririwa akiwaambia wajumbe wa Bunge hilo kwamba Rais alikuwa ameridhia kwamba siku 60 alizotoa hazingejumuisha Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu.
Ni kwa msingi huo, Bunge hilo likapanga kwamba lingeendelea na shughuli zake hadi Oktoba 31, wakati Mwenyekiti wa Bunge atakapokabidhi Katiba inayopendekezwa kwa Rais Kikwete.
Hata hivyo, makubaliano yaliyofikiwa baina ya viongozi wa TCD na Rais yanaonekana kuvuruga kabisa ratiba ya Bunge hilo ambalo jana na juzi, Kamati ya Uongozi ilikutana mara kadhaa kuona jinsi ya kunusuru mchakato huo.
Ingawa haikufahamika mara moja kama vikao hivyo vya kamati ya uongozi inayoongozwa na Sitta mwenyewe vinajadili nini, lakini taarifa zimedai huenda kukawa na mabadiliko makubwa ya ratiba.
Habari nyingine zinadai kwamba mabadiliko hayo huenda yakapunguza muda wa baadhi ya shughuli za kazi za Bunge hilo ili liweze kukamilisha kazi yake ikiwamo wajumbe kupiga kura ya uamuzi.
Katika kikao cha jana asubuhi, kamati hiyo ilishindwa kurekebisha ratiba yake ili iendane na siku zilizosalia, hivyo kuahirishwa kwa kuwapa kazi wataalamu wake kuleta mapendekezo ambayo yangejadiliwa jana mchana.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alithibitisha jana kwamba ratiba ya Bunge imebadilika kutokana na hoja nyingi kukubalika ndani ya kamati.
“Kamati ya uongozi itakutana baadaye (jana) kuangalia vipengele ambavyo hawakukubaliana kwenye kamati ndivyo wavipangie muda na ratiba itajulikana baada ya kikao hicho,” alisema Hamad

No comments:

Post a Comment