July 5, 2016

Kenyatta: Karne hii hauwezi kujitenga Israel

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (Kushoto) akiwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
SOURCE:RFI KISWAHILI
Viongozi wa Kenya na Israel wametiliana saini mikataba kadhaa ya ushirikiano, huku suala la kubadilishana taarifa za kiintelijensia kuhusu watuhumiwa wa Ugaidi, likiwa sehemu ya makubaliano hayo.
Akiwa nchini Kenya, waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa, ziara yake inalenga kurejesha uhusiano wa nchi yake na mataifa ya Afrika, uhusiano ambao kwa miongo kadhaa sasa umekuwa shakani.
Nchi nyingi za Afrika na hasa kupitia waasisi waliopigania uhuru wa mataifa yao, walisitisha uhusiano na taifa la Israel, kutokana na uvamizi wake kwenye eneo la ardhi ya Wapalestina, mzozo ambao umeendelea kushuhudiwa hadi leo.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, kuhusu ushirikiano wa nchi ya Kenya na Israel, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amesema kuwa, kutokana na ukweli kuwa dunia ni kijiji kimoja, na kwamba mataifa mengi duniani yamerejesha uhusiano wao na Israel, nchi ya Kenya haiwezi kujitenga na ukweli huo.
Rais Kenyatta, anasema kuwa, suala la Israel kukubalika kwenye umoja wa Afrika, ni jambo la kihistoria, na kwamba anaamini siku moja litapatiwa ufumbuzi, na nchi nyingi zaidi kurejesha uhusiano na Israel.
Kenyatta anasema kuwa adui anayeisumbua Israel ndiye adui ambaye anasumbua dunia kwa sasa na hasa nchi za Afrika, hususani nchi ya Kenya ambayo imeendelea kukabiliana kwa nguvu zote na magaidi.
Viongozi wote wawili, wamekubaliana kukaza kamba kuhusu ushirikiano wao wa masuala ya usalama, na kwamba masuala ya kihistoria, hayawezi kuwatenga tena, wakati huu dunia ikiwa na malengo yanayofanana.
Waziri Mkuu Netanyahu, amesema kuwa nchi yake haina kitu kikubwa cha kujivunia, haina silaha nzitonzito wala zana za maangamizi, lakini Mungu amewajalia akili na moyo vitu ambavyo ndio vinalifanya taifa hilo kuwa miongoni mwa mataifa makubwa na yenye nguvu 
www.ngarakwetu.blogspot.com

No comments:

Post a Comment