May 18, 2017

Habari njema:Ujenzi wa barabara ya Murugarama,Rulenge-Nyakahura

Hivi Karibuni katika vikao vya Bunge,Mh.Alex R.Gashaza Mbunge wa  Jimbo la Ngara aliuliza  swali:-

SWALI

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Naitwa Alex Raphael Gashaza, Mbunge wa Jimbo la Ngara.
Kwa kuwa barabara ya Murugarama – Rulenge – Nyakahura yenye kilometa 85 ni barabara ambayo iliahidiwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2008 kwamba itaweza kujengwa kwa kiwango cha lami na miaka miwili iliyopita wananchi wa Jimbo la Ngara walikuwa wakielezwa kwamba tayari upembuzi yakinifu wa barabara hii umeanza.
Naomba kumuuliza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ni lini mkandarasi atakuwepo site kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii? 


MAJIBU

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata taarifa kutoka kwa Waziri mwenyewe wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano juu ya upatikanaji wa fedha za kulipa madeni ya wakandarasi, kama jana mlimsikia alisema ni karibu shilingi bilioni 419 zimeshatolewa. Kwa hiyo, katika lile deni la shilingi trilioni 1.268 sasa tumeshuka tuko kwenye shilingi bilioni 800 na zaidi. Naomba kuchukua nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mara fedha zitakapopatikana kwa mradi huo, barabara yake itashughulikiwa kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
source:http://www.parliament.go.tz
www.ngarakwetu.blogspot.com

No comments:

Post a Comment