December 5, 2013

RAIS WA ZAMANI WA AFRIKA KUSINI NELSON MANDELA AFARIKI DUNIA

Mandela alikuwa Rais wa zamani wa Afrika Kusini na ameaga akiwa na umri wa miaka 95.


Taarifa  za  kifo cha Nelson Mzee Nelson Mandela zimetolewa na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma
Rais Zuma amesema  kuwa mzee Mandela amefariki akiwa na miaka 95.

Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma amesema taifa limepoteza baba wa taifa na bendera zitapepea nusu mlingoti kufuatia msiba huo mkubwa kwa taifa hilo.Mandela amekuwa akiugua kwa muda mrefu.
Naye rais wa Marekani Barack Obama amesema nchi ya Afrika Kusini pamoja na dunia kwa ujumla imepoteza mtu muhimu

Maisha yake
Nelson Rolihlahla Mandela alikuwa mwanasiasa mkongwe na mwanaharakati aliyepambana na sera za ubaguzi za makaburu wa Afrika Kusini na hatimaye kuwa Rais wa kwanza Mwafrika nchini humo. Ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel. Mbali na tuzo hiyo, ameshatunukiwa zaidi ya tuzo 250 katika miongo minne iliyopita. 

Alizaliwa Julai 18 mwaka 1918. Ni rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia nchini Afrika Kusini. Alikuwa mwanasheria na mwanachama wa Chama cha African National Congress (ANC) aliyepinga siasa ya ubaguzi nchini Afrika Kusini.
Mandela anatokea katika ukoo wa Thembu uliokuwa ukitawala mkoa wa Transkei lililopo katika jimbo la Eastern Cape. Alizaliwa katika Kijiji cha Mvezo katika Wilaya ya Umtata na ana asili ya Kabila la Khoisan kwa upande wa mama yake.
Babu yake wa upande wa mama aliyefariki mwaka 1832 Ngubengcuka,  alikuwa mfalme wa ukoo wa Thembu na mmoja kati ya watoto wake aliitwa Mandela. Huyo ndiyo Babu yake Nelson na chanzo cha jina hilo la ukoo.
Baba yake Mandela Gadla Henry Mphakanyiswa alikuwa chifu wa mji wa Mvezo, hata hivyo baadaye aliondolewa na wakoloni katika cheo hicho na kubaki kuwa mjumbe wa baraza. Mphakanyiswa alikuwa na wake wanne ambao walimpatia watoto 13, wanaume wanne na wanawake tisa.
Mandela alizaliwa kwa mke wa tatu na kupewa jina la Rolihlahla likiwa na maana ya kuvuta tawi la mti au kwa nahau ‘msababisha matatizo’.
Rolihlahla alikuwa mtoto wa kwanza katika familia yao kwenda shule ambako mwalimu wake Mdingane alimpa jina la Nelson. Baba yake alifariki kwa ugonjwa wa kifua kikuu wakati Mandela akiwa na umri wa miaka tisa, hivyo ndugu yake aitwaye Jongintaba akawa mlezi wake.
Alisomea katika Shule ya Misheni ya Wesleyan. Alipofikisha miaka 16 alijiunga na Taasisi ya Clarkebury kwa miaka miwili ambapo alipata cheti cha awali. Mwaka 1937 alihamia katika mji wa Healdtown katika chuo kingine cha Wesleyan. Akiwa na miaka 19 alijihusisha na michezo ya masumbwi na riadha.
Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Fort Hare, ambapo alichukua shahada ya Sanaa na hapo ndipo alipokutana na Oliver Tambo ambaye aliendelea kuwa rafiki yake kwa muda mrefu.
Baada ya mwisho wa mwaka wa kwanza, Mandela alijihusisha na mgomo ulioandaliwa na baraza la wanafunzi wakipinga sera za chuo hicho. Matokeo yake alifukuzwa shule hadi pale atakapokubali masharti ya chuo. Baadaye akiwa jela, Mandela alisoma shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha London katika programu ya nje.
Baada ya kufukuzwa shule, mlezi wake Jongintaba alimtaka aoe akiwa na ndugu yake Justice. Hata hivyo, Mandela hakutaka na hivyo akakimbilia mjini Johannesburg ambako alitafuta kazi ya ulinzi kwenye migodi ya madini, kazi ambayo hakuifanya kwa muda mrefu.
Baadaye Mandela alianza kufanya kazi ya usaidizi wa ofisi katika ofisi ya sheria mjini Johanesburg. Akiwa hapo alikamilisha masomo yake ya Shahada ya Sanaa katika Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kwa njia ya posta na baada ya hapo alianza masomo ya sheria katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand  ambako alikutana na marafiki wengine waliopambana katika vita ya ubaguzi wa rangi ambao ni Joe Slovo, Harry Schwarz na Ruth First.
Siasa
www.ngarakwetu.blogspot.com
Baada ya ushindi wa chama cha Afrikaner wa mwaka 1948 kilichokuwa kikiunga mkono ubaguzi wa rangi, Mandela alianza kujihusisha rasmi na siasa. Alikiongoza chama cha ANC katika kampeni za uasi za mwaka 1952 na mkutano wa mwaka 1955 ambao ulizaa mchakato wa uhuru na kuweka msingi wa kupiga ubaguzi wa rangi. 
Akiwa amevutiwa na siasa za aliyekuwa Waziri Mkuu wa Indiawakati huo Mahatma Gandhi, Mandela alianza kufanya upinzani usio na vurugu.
Mwaka 1956, alikamatwa akiwa na wafuasi wake 150 na kushitakiwa kwa uhaini. Hata hivyo baada ya kesi hiyo kwenda hadi mwaka 1961, waliachiwa huru.
Kifungo cha maisha
Mwaka huohuo 1961 Mandela aliteuliwa kuwa kiongozi wa kikosi cha silaha kikijulikana kama ‘Umkhoto we Sizwe’. Aliratibu mapambano dhidi ya majeshi ya Serikali na kuweka mikakati ya vita vya msituni, kama hujuma za kukomesha ubaguzi zingekwama.
Agosti 5, 1962 Mandela alikamatwa na majeshi ya Serikali na kuwekwa jela ya Johannesburg baada ya kupotea kwa miezi 17.
Makundi mbalimbali yalihusishwa na njama za kukamatwa kwake kikiwemo Chama cha South African Communist Party na kitengo cha Intelijensia cha Marekani (CIA). Hata hivyo Mandela hakutilia maanani madai hayo.
Juni 12, 1964, Mandela alihukumiwa kifungo cha maisha baada ya kujitetea mahakamani kuhusu harakati zake dhidi ya ubaguzi wa rangi. Alipelekwa katika gereza lililopo katika Kisiwa cha Robben.
Februari 2, 1990 aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Fredrick de Klerk aliondoa amri ya kukipiga marufuku chama cha ANC na makundi mengine yanayopinga ubaguzi wa rangi na akatangaza kumwachia huru Mandela.  Aliachiwa rasmi Februari 11, 1990 tukio lililoonyeshwa dunia nzima.

Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu.Amina!              www.ngarakwetu.blogspot.com



No comments:

Post a Comment