November 10, 2014

Kikwete afanyiwa upasuaji Marekani

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Dk Edward Shaeffer alipowasili katika hospitali ya Johns Hopkins Marekani kwa ajili ya upasuaji. PICHA|IKULU
Dar es Salaam. Rais, Jakaya Kikwete amefanyiwa upasuaji wa tezi dume (prostate) katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu kwa vyombo vya habari jana imesema Rais Kikwete amefanyiwa upasuaji huo juzi alfajiri baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa afya yake kujiridhisha kuwa alikuwa anahitaji matibabu ya aina hiyo.
“Upasuaji huo uliofanyika alfajiri na kuchukua kiasi cha saa moja unusu, umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa,” ilisema taarifa hiyo na kubainisha kuwa hali ya Rais Kikwete inaendelea vizuri na bado yuko wodini akiendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na kupatiwa tiba.
Taarifa hiyo iliyoambatana na picha mbili moja ikimwonyesha Rais Kikwete akiwa anazungumza na daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali hiyo, Dk Edward  na nyingine akiwa ameketi pamoja na daktari huyo pamoja na daktari wake, Profesa Mohamed Janabi ilisema wananchi wataendelea kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais kwa kadri zitakavyokuwa zinapatikana.
Wiki iliyopita, Kurugenzi hiyo ya mawasiliano Ikulu ilitoa taarifa za safari ya Rais Kikwete kwenda Marekani kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake na kuwa angekaa huko kwa siku 10.
    Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment