December 6, 2013

Mbunge wa Biharamulo Dk Mbassa amlilia Mandela





Siku chache zilizopita baada ya Ulimwengu kupata taarifa za kifo cha aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini Nelson Mandela,baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa hapa Nchini wameonesha kuguswa na kifo hicho

Miongoni mwao wametaja kifo hicho kuwa ni pengo lisilozinbika kirahisi katika harakati za ukombozi, na jitihada za kuharakisha maendeleo. Miongoni wa walioonesha kuguswa na kifo hicho ni Dk. Anthony Gervase Mbassa Mbunge wa jimbo la Biharamulo magharbi (CHADEMA) anayewataka watanzania   kila mmoja kwa nafasi yake  kutimiza wajibu wake katika majukumu aliyonayo na  kumuenzi MANDELA  kwa kuyatenda mema yote aliyokuwa akiyapigania.
Haya  ndiyo aliyosema:-

Hakika kifo ni safari tarajiwa ya kila mmoja na hakuna awezaye kuiepuka japo kwa gharama yoyote ikiwa Mwenyezi Mungu amependa kukuita kwake.
Leo tena tunashuhudia ukomo wa miaka 95 wa nyota iliyoleta nuru, upendo, mshikamano wa dhati katika kuupinga ubaguzi wa rangi ikipoteza nuru yake barani Afrika ! Hakika nuru imezimika.

Dk. Mbassa anasema Imemchukua muda kuamini taarifa hizi, japo kama si tarehe mosi April kila mwaka siku ambayo watu huitumia kudanganyana kwa muda, lakini mara nyingi taarifa ya kifo huwa haina utani wa jinsi hiyo.
“Nikakumbuka kwa kina safari ndefu mpambanaji huyu, mtetezi wa haki za binadamu jinsi alivyopitia hatua ngumu zenye kumuhitaji mtu kufanya maamuzi ya kina na ya dhati katika kupambana na harakati za ukombozi wa walio wengi.” ansema ni ngumu kuamini kutokana na umuhimu wake licha ya kuwa taarifa za kuugua kwa mzee Mandela zinafahamika

Mara nyingi watu hawa maarufu jitihada zao huonekana mapema sana katika maisha yao ya kila siku na mwisho huwa wanashuhudia kwa kiasi kidogo mafanikio ya juhudi walizo zifanya. Na hakika huo ndio ukweli wa mashujaa wengi wanaojitoa katika kuleta ukombozi.

Historia ya Madiba inaazia mbali, kama kijana pekee ambaye kwenye familia yake ndiye aliyepata bahati ya kupata elimu enzi hizo za utawala wa ki -chief ili akafanye kazi kwa chief, lakini anaponyoka mkondo huo na kujikuta akiingia chuo cha elimu ya juu katika chuo kikuu cha Fort Hire kwa watu weusi kipindi hicho, pamoja na kuchaguliwa kuwa kiongozi wa serikali ya wanafunzi alijikuta akisimamishwa chuo baada ya kuunga mkono madai ya walio wengi kutaka kuboreshewa hali ya chakula na mazingira ya chuo.
Hakika hii ni kujitoa kwa moyo wa dhati.
Kana kwamba haitoshi, baada ya kuhitimu kama mwanasheria, anaitumia elimu yake pamoja na wachache waliokuwa wamepata elimu kipindi hicho kwa manufaa ya jamii nzima, lakini kwa maksudi serikali ya kidharimu ikaamua kufunga ofisi hiyo na kuihamishia mbali watu wasikoweza kufika kwa urahisi, hii ni kuendeleza ukandamizaji wa haki za Binadamu.
Pamoja na misukosuko mingi ya kufungwa jela kisa kasafiri bila kibali, masuala yote ya kuwekewa kesi kama uhaini na mwisho kufungwa jera miaka ishirini na saba ni sadaka ndefu sana kwa maisha ya mwanadamu.
Na hakika baada ya yote hatukuwahi kusikia kesi yoyote akidai fidia kwa mateso aliyopata akipinga ubaguzi wa rangi.

Ni somo kubwa sana kwetu sisi tuliobakia, nina uhakika kama lingemtokea sasa hivi mtu ambaye hakuzaliwa na chembechembe za uzalendo hakika kulipiza kisasi ingekuwa ndiyo suluhisho la mambo yote.
Kubwa ni kila mmoja atimize wajibu wake katika majukumu aliyonayo mbele ya safari, na tumuenzi kwa kuyatenda yote aliyotuachia. Nina imani katika nyanja zote kauugusa iwe ki-imani, ki-siasa, ki-uchumi, ki-saikolojia nk. Je mimi na wewe mchango wetu katika nchi yetu ni upi? Tafakari!

No comments:

Post a Comment