October 30, 2014

RAIS WA ZAMBIA AFARIKI DUNIA


           
RAIS WA ZAMBIA AFARIKI DUNIA
Serikali ya Zambia imesema Rais wa nchi hiyo Michael Sata amefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu kwa maradhi ambayo hayakutajwa.

Rais Sata, 77, alifariki katika hospitali ya King Edward VII jijini London, Uingereza Jumanne usiku.
Vyombo vya habari vimesema alifariki baada ya "mapigo ya moyo kwenda kasi ghafla".
Haijafahamika mara moja nani atachukua nafasi yake ya urais. Suala hilo huenda likajadiliwa na baraza la mawaziri la Zambia litakalokutana Jumatano asubuhi.

"Kwa moyo mzito natangaza kifo cha rais wetu mpendwa," imesema taarifa ya waziri Roland Msiska iliyosomwa kwenye TV ya taifa."Nawaomba muwe watulivu, muungane kwa amani katika kipindi hiki kigumu," ameongeza kusema Bwana Msiska.


Mapema mwezi huu taarifa nchini Zambia zilisema Rais Sata alikuwa amekwenda nje ya nchi kwa matibabu, huku kukiwa na tetesi kuwa alikuwa taabani.


Baada ya kuondoka nchini humo, waziri wa ulinzi Edgar Lungu alitajwa kukaimu urais.
Makamu wa rais Guy Scott mara nyingi hukaimu urais. 


Hata hivyo ana asili ya Scotland na wazazi wake hawakuzaliwa Zambia, hivyo hatoweza kuchukua urais kutokana na vipengele ndani ya katiba.

Akijulikana kama "King Cobra" kutokana na matamshi yake makali, Bwana Sata alichaguliwa kuwa rais wa Zambia mwaka 2011.




          SourcE: BBC

No comments:

Post a Comment